Home Habari za michezo TWENDE MBELE TURUDI NYUMA…UKWELI MCHUNGU HATA SIMBA BADO HAIJAFANIKIWA..

TWENDE MBELE TURUDI NYUMA…UKWELI MCHUNGU HATA SIMBA BADO HAIJAFANIKIWA..

Ukiona timu inashangilia na kufanya jambo kubwa kuingia hatua ya makundi kwenye mashindano madogo ya CAF usiwacheke au kuwazuia kwa sababu wametimiza lengo au ndiyo faraja waliyoipata ambayo kujirudia tena sio leo wala kesho. Tatizo letu kubwa Watanzania kwa kiasi kikubwa tunaridhika na vitu vidogo sana.

Tunahisi kufanikiwa mapema sana. Leo hii ni kawaida tu mtu kukuambia kuwa Simba ndiyo timu pekee yenye mafanikio kwenye michuano ya kimataifa kutoka Tanzania. Ukiuliza ni kwa sababu gani? Utaambiwa Simba imewahi kucheza fainali ya Kombe la Washindi Afrika.

Utaambiwa Simba imetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili katika miaka mitano ya karibuni. Utaambiwa Simba imefika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana. Haya ndiyo Mafanikio ya Simba Afrika na watu wanafanya sherehe na kutambinana.

Ndugu zangu mpira wetu una Safari ndefu na ni lazima tuachane kwanza na haya mawazo madogo. Watu wenye mawazo madogo huwa wanachelewa kusonga mbele. Watu wenye mawazo madogo huridhika na mambo madogo madogo.

Kifupi ni kwamba Simba bado hajafanikiwa kimataifa, isipokuwa imefika kwenye hatua za juu kwenye mashindano mara nyingi kuliko mtani wake, Yanga. Haya sio mafanikio. Tambo za Simba na Yanga ni utani tu wa jadi, lakini sio mafanikio kwenye nadharia ya soka.

Ukiona bado kuna maelfu ya watu wanaweza kuacha shughuli zao na kwenda kuipokea uwanja wa ndege timu ambayo imeingia tu hatua za makundi Afrika ujue bado tuna safari ndefu sana. Ukiona mamia na maelfu ya watu wanamiminika na kiti cha mchongo uwanja wa ndege kwenda kumbeba kiongozi wao kama chifu eti kwa sababu tu amesajili wachezaji wa kigeni, jua bado mpira wetu una kazi kubwa kwenye ukuaji wake. Haya yote yanaonyesha ni kwa namna gani mpira wetu bado unahitaji siku nyigi kukua. Bado mpira una safari ndefu ya kupata mafanikio.

Kwa pesa mpira wetu unazoingiza kutoka Azam Media. Kwa pesa mpira wetu unazoingiza kutoka SportPesa. Kwa pesa tunazoingiza kutoka M-Bet. Kwa pesa tunazoingiza kutoka kwa watu binafsi kama Said Bakhresa, Ghalib Said Mohammed, Mohammed Dewji na wengineo tulipaswa kuwa mbali sana.

Tulipaswa kuwa watu wa kushangilia makombe uwanja wa ndege. Tulipaswa kuwa watu wa kupeleka maua uwanja wa ndege kuwapokea mabingwa wa Afrika. Zama za kwenda kuwapokea watu uwanja wa ndege tungeziacha siku nyingi.

Huu ni wakati wa kwenda kupokea makombe sio hatua ya makundi. Haya sio mafanikio kwa pesa waliowekeza Yanga. Huwezi kwenda kumpokea kocha Juma M-gunda uwanja wa ndege eti kisa ameifunga De Agosto ya Angola. Haya mambo madogo yanatupoteza sana.

Haya mambo madogo yanatufanya tukose mambo mengi mazuri. Tunaridhika mapema. Tunatimiza malengo mapema. Tunaweza zaidi kuja kumtambia mtani badala ya kwenda Kushiriki na kuitambia Afrika. Mawazo haya lazima yaondoke kwa viongozi wetu. Mawazo haya ni lazima yaondoke kwa wachezaji wetu.

Bado hatujazitendea haki pesa zilizowekezwa kwenye mpira wetu mpaka sasa. Kwa pesa za Azam Media, Said Bakhresa, Mohammed Dewji, Ghalib Said na wengine wengi tulipaswa kuwa na timu nne zote hatua za makundi kwenye michuano ya CAF msimu huu. Azam walipaswa kuvuka. Geita Gold walipaswa kuvuka.

Kama pesa za mpira wetu zingekuwa Kenya au Uganda ungeona tofauti kubwa sana.

Tusingewasogelea hata kidogo. Wangetuacha mbali mno. Sisi bado ni watu wa kuridhika na vitu vidogo. Yanga tayari wanaona ni kama msimu umemalizika kwa wao kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Hapo ndipo tatizo lilipo. Viongozi wa timu wana pesa. Maua kwa kufika hatua ya makundi aisee, kazi ipo. Ndugu zangu haya sio mafanikio yanayoakisi uwekezaji wa pesa uliofanyika.

Haya sio mafanikio yanayoenda na ukubwa wa timu zetu. Timu zetu ni kubwa. Timu zetu kuna pesa zinazalishwa. Timu zetu zina wadhamini wanamwaga pesa. Tuache kuridhika na vitu vidogo. Simba wanatakiwa kufika walau nusu fainali msimu huu ili mwakani mipango iwe ni kwenda kuchukuwa ubingwa.

Yanga wako Kombe la Shirikisho walau kule hakuna vigogo wengi wa Afrika. Watu wanatakiwa kuwaza nusu fainali msimu huu ili mwakani iwe ubingwa. Ndiyo akili kubwa za wenzetu zinavyowaza. Sisi kazi yetu ni kwenda uwanja wa ndege na kupokea hatua ya makundi utadhani timu imeshinda kombe.

Kenya na Uganda ilitakiwa tuwaache mbali sana kwenye ligi za ndani kwa sababu mpira wetu una uwekezaji mkubwa na mashabiki kuliko wao.

Wenzetu bado ligi za Ulaya zina nguvu sana nchini kwao, lakini sisi tulishatoka huko. Ligi Kuu Tanzania Bara inachuana kabisa na Ligi Kuu England (EPL) kwa nguvu ya ushabiki.

Ukiweka mechi ya Simba dhidi ya Yanga siku moja na England kuwe na Manchester Derby, Watanzania wengi utawakuta kwenye ile Kariakoo Derby.

Mpira wetu una nguvu sana. Mechi ya Fulham dhidi ya Newcastle United, haiwezi kuwa na nguvu nchini kuliko Singida Big Stars dhidi ya Azam.

Mpira wetu una nguvu sana. Hii kitu haipo kwa wenzetu wa Kenya na Uganda. Tunapaswa kutumia vyema wakati huu kupata mafanikio makubwa Afrika. Sio kwenda kupokea watu uwanja wa ndege wakatika hakuna kombe lolote waliloshinda. Lazima tuwe na matumizi mazuri ya neno mapokezi.

Tukienda uwanja wa ndege dunia ijue kumbe kombe la Afrika limetua nchini. Sio mambo madogo madogo kama kufika hatua ya makundi. Huko ni kutojitendea haki.

SOMA NA HII  KUHUSU AZIZ KI KUSHUKA KIWANGO NDANI YA YANGA SC....UKWELI MCHUNGU HUU HAPA....