Kama kuitika basi waliitika kwenye Uwanja wa Liti mjini hapa. Mashabiki waliojitokeza kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Singida Big Stars dhidi ya Simba wameizidi mechi ya Dodoma Jiji na Yanga kwenye uwanja huohuo.
Kwa mujibu wa takwimu za mapato zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Singida (SIREFA), Mwendwa Kanka ni kama mashabiki wa Simba walihamasika zaidi kuitazama timu yao ikicheza na wenyeji tofauti na Yanga ingawa na kiwango cha viingilio ni tofauti.
“Mechi ya Simba na Singida ilitoa mapato takribani milioni 60 huku ya Yanga yenyewe ikiwa milioni 28 kama chama tunafuraha kwakweli na ujio wa timu hizo kubwa nchini lakini pia tunajivunia kuwa na timu ya mkoa kwenye ligi,” alisema Kanka licha ya kutoingia kiundani zaidi.
Licha ya takwimu hizo za mapato wapo ambao wanasema Dodoma walikosa idadi kubwa ya mashabiki kutokana na viwango vya viingilio ambavyo waliweka kuwa Sh. 15,000 VIP huku majukwaa mengine ikiwa Sh.10,000 jambo ambalo liliwakwaza mashabiki wengi na baadhi yao kuishia kwenye Bar zilipo jirani na uwanja.
Singida BS na Simba waliweka Sh. 10,000 kwa VIP huku cha kawaida ikiwa ni Sh. 5000, inaelezwa kuwa viingilio hivyo maranyingi ni rafiki kwa mashabiki kwenye michezo mingi.
Mchezo wa Simba umeweka rekodi uwanjani hapo kwa mapato msimu huu, ambao ulichezwa Novemba 9 ulimalizika kwa sare 1-1 wa Yanga ambao ulicheza juzi dhidi Dodoma ulimalizika kwa mabao 2-0. Usajili mkubwa uliofanywa na Singida umechochea morali ya mashabiki ambao miaka ya nyuma ilikuwa ni nadra kuona mastaa zaidi ya mmoja tena kutoka Brazil wakicheza timu za mikoani.
Yanga na Simba kwa nyakati tofauti walisifia hali ya uwanja huo lakini ya kuongeza kwamba nyasi zinapaswa kuboreshwa zaidi ili ziwe rafiki kwa wachezaji na mpira utembee. Mechi ijayo Simba watacheza Kilimanjaro dhidi ya Polisi Tanzania huku Yanga ikiwa wenyeji wa Mbeya City Jijini Dar es Salaam.