Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda ametoa msimamo mkali wa kusimama na wachezaji wake kwa matokeo yoyote yale huku akiwaonya mashabiki kuacha kuwashambulia badala yake wawape sapoti.
Simba ilirejea Dar es Salaam juzi Jumatano usiku ikitokea jijini Mbeya ilipotoka sare ya bao 1-1 na Mbeya City na jana iliondoka kwenda Moshi kwaajili ya mechi dhidi ya Polisi Tanzania.
Baada ya mchezo na Mbeya City mashabiki mitandao na kwenye eneo la klabu ya Simba Kariakoo Jijini Dar es Salaam, walionyeshwa kutoridhishwa na kiwango lakini Mgunda amewataka kutulia na kuacha kuwatupia lawama wachezaji kwani bado ligi ni ndefu na hawapaswi kubabaika.
“Hakuna kocha yeyote asiyependa kuona timu yake ikishinda, hivyo mashabiki wanapaswa kulitambua hilo na kuacha kuanza kuwatoa wachezaji kwenye mstari,” alisema Mgunda ambaye muda wowote kuanzia sasa anaweza kuwasili bosi wake, raia wa Ureno.
“Ni kweli mabeki wangu waliruhusu bao jepesi kwa sababu kwa kaliba na uwezo wao sio watu wa kufanya vile lakini ndio mchezo wa mpira wa miguu unapofanya makosa utaadhibiwa tu,” aliongeza kocha huyo wa zamani wa Coastal Union na Taifa Stars.
Kitendo cha Simba kukosa ushindi kinaiweka kwenye mazingira magumu ya kutwaa ubingwa wao kutokana na kasi ya wapinzani wao, Yanga lakini pia ratiba ngumu inayowakabili kwa mechi za ugenini.
Pia, kuumia kwa nyota wake, Augustine Okrah kumeongoza hofu kwa mashabiki wa Simba kutokana na majeraha kuongezeka kikosini hapo akiungana na Peter Banda, Sadio Kanoute, na Nelson Okwa sambamba na Jimmyson Mwanuke na Israel Mwenda ambao hawajawa tayari kwa mchezo.
Kuumia kwa Okrah, kunaifanya timu hiyo kukosa mawinga asilia kwani mwingine ni Banda naye hatakuwa sehemu ya kikosi hadi mwezi wa pili mwakani akiuguza majeraha aliyoyapata kwenye mechi na Namungo iliyomalizika kwa sare ya 1-1 huku akifunga bao la kusawazisha.
Pamoja na hayo Mgunda amefunguka kuumizwa na majeraha yanayotokea mara kwa mara kwa wachezaji wake lakini anaamini ujio wa kocha wa viungo, Kelvin Mandla utaongeza utimamu wa wachezaji na kupunguza shida hiyo.
“Tumepata kocha wa viungo atatusaidia licha ya kwamba amekuja kipindi ambacho ligi inaendelea, naamini kwa jinsi alivyoanza kazi atapunguza tatizo hilo kwani kabla ya hapo wachezaji wengi walipungukiwa utimamu wa mwili jambo lililopelekea majeraha ya mara kwa mara,” alisema Mgunda ambaye amemuongeza Mussa Mgosi kwenye benchi lake kama kocha msaidizi baada ya Seleman Matola kwenda kusoma kozi ya CAF Diploma A, visiwani Zanzibar.
Simba itacheza mechi zijazo tano ugenini (mikoani), ikiendelea leo na Polisi Uwanja wa Ushirika, kisha Coastal Union pale Mkwakwani Tanga.
Baada ya hapo itaenda Mwanza itakapocheza mechi mbili CCM Kirumba dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar na mechi nyingine itakuwa na KMC ambayo pia Wana Kinondoni hao wanaweza kuipeleka mkoani kwa sababu za kimasilahi.