Home Azam FC BAADA YA KUANZA KUTUPIA KAMA ‘JINI’…..MBOMBO AJITANGAZIA VITA AZAM FC…

BAADA YA KUANZA KUTUPIA KAMA ‘JINI’…..MBOMBO AJITANGAZIA VITA AZAM FC…

Azam iko pale juu inaminyana na Simba na Yanga katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ikithibitisha kwamba inaitaka ndoo hiyo, huku straika wake aliye katika kiwango bora, Idris Mbombo akisema: “Mwaka huu mtajionea.”

Mbombo ambaye ana mabao sita sawa na Moses Phiri wa Simba na Reliants Lusajo wa Namungo, wakizidiwa bao moja tu na kinara wa ligi, Sixtus Sabilo wa Mbeya City (7), ameweka wazi shauku yake ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa na pia kutimiza ndoto zake binafsi.

Akizungumza Mbombo alisema anachokiangalia zaidi kwake ni mafanikio ya timu hiyo ambayo ilitwaa ubingwa wake wa kwanza na wa mwisho katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/14.

“Malengo yetu ni kuona tuna mwendelezo mzuri kwenye kila mchezo tunaocheza kwa sababu hii itatuongezea motisha ya kupambana, huu ni mwanzo mzuri hivyo tunapaswa kuendelea hivyo.”

Aidha, Mbombo alisema anaamini msimu huu ndio ambao unaweza kuwa bora zaidi kwake ndani ya kikosi hicho hivyo jambo kubwa analoliomba ni kuepuka majeraha ya mara kwa mara yatakayomrudisha nyuma.

Kaimu kocha mkuu wa kikosi hicho, Kally Ongala alimzungumzia Mbombo kama mchezaji wake tegemeo huku akiweza wazi ubora wake msimu huu unatokana na kutambua vyema thamani na malengo ya klabu.

Mbombo aliyejiunga na Azam msimu uliopita akitokea El Gouna ya Misri alisaini mkataba wa miaka miwili ingawa hakuwa akipewa nafasi sana kutokana na uwepo wa washambuliaji, Prince Dube na Rodgers Kola, ambao ni kati ya sajili za kibabe zilizofanywa na klabu hiyo ya Chamazi iliyodhamiria kurejesha heshima yake.

Sajili za nyota kama Kipre Junior, James Akamiko na kipa Ali Ahmada zimeiboresha timu hiyo.

SOMA NA HII  AL AHLY WAICHAPA AS VITA KWAO, KUNDI A NI NOMA