Home Geita Gold FC BAADA YA MPOLE KUISUSIA GEITA…NTIBAZONKIZA NAYE AKIWASHA..ASUSA KUJIUNGA NA TIMU…

BAADA YA MPOLE KUISUSIA GEITA…NTIBAZONKIZA NAYE AKIWASHA..ASUSA KUJIUNGA NA TIMU…

Geita Gold FC

Kikosi cha Geita Gold kinaendelea kupukutika baada ya idadi ya wachezaji muhimu kudaiwa kujiweka pembeni kutokana na madai yao ya kimaslahi na sasa kufikia saba huku uongozi ukisisitiza kuwa hakuna mchezaji anayewadai.

Geita Gold ambayo ipo chini ya kocha Fredy Felix ‘Minziro’ inacheza na KMC Novemba 17, inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi. Mechi 10, imeshinda tatu, sare nne na kufungwa tatu.

Mastaa hao ni George Mpole, Said Ntibazonkiza, Oscar Masai, Ramadhan Chombo, Hussein Bakari na Sebusebu Sebusebu wachezaji hao wote kwa asilimia kubwa wapo kikosi cha kwanza. Baadhi ya wachezaji hao walisema wameamua kujiengua kutokana na madai hayo na hawatarudi hadi viongozi watakapotimiziwa haki zao huku wakisisitiza kuchoshwa na ahadi zisizo timia tangu msimu huu kuanza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema ni kweli wapo nje ya timu sio kwa ruhusa maalum kama viongozi wanavyosema wameondoka kwasababu wanaidai timu wengine mishahara na baadhi ya ada za usajili.

“Sipo pamoja na timu sifahamu nini kinaendelea kuhusiana na maandalizi yao dhidi ya KMC, nipo nyumbani, majibu wanayo viongozi,” alisema mmoja wa wachezaji ambaye yupo nje ya kikosi.

“Nina madai na timu sipo kambini nimeamua kutoka ili waweze kunitimizia mahitaji yangu, huwezi kuamini mimi sijapata hata kiasi kidogo cha fedha yangu ya usajili najikimu vipi nina familia naiendesha vipi maisha.”

KOCHA AFUNGUKA

Minziro alisema ni kweli kuna baadhi ya wachezaji hawapo kambini na hafahamu sababu ni nini lakini hilo halimfanyi akashindwa kuendelea kufanya maandalizi ya timu kuwakabili KMC ana imani na wachezaji alionao atawaandaa kwaajili ya ushindani.

“Timu imesajili wachezaji wengi lengo ni kutoa nafasi kwa kila mmoja apate nafasi ya kucheza waliopo wana nafasi pia ya kucheza kutokucheza muda mrefu haina maana kwamba hawana wanachofahamu kuhusu mpira nahitaji matokeo na wao wanajua timu inataka ushindi hivyo tusubiri dakika 90 zitaamua nini,”

VIONGOZI WAJAJUU

Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu hiyo, Constantine Morandi alidai taarifa za wachezaji kuidai klabu hiyo hazina ukweli wowote huku akikiri kuwa majina ya wachezaji aliotajiwa na Mwanaspoti ni kweli hawapo na timu lakini ni kwa ruhusa maalum na si vinginevyo.

Pia alitumia nafasi hiyo kumtaka Mpole kurudi kwenye timu haraka ili aweze kutumikia ajira yake kwani ameondoka ndani ya timu bila taarifa yoyote na hana madai na timu hivyo anahitajika kurudi haraka kambini.

“Ni kweli kuna baadhi ya wachezaji hawapo kambini lakini wana ruhusa maalum mara baada ya mchezo wetu na Yanga waliomba kwenda makwao tunatarajia wataungana na timu kabla ya mchezo wetu na KMC ili kuongeza nguvu,” alisema na kuongeza;

“Mpole hatuna taarifa za yeye kuwa nje ya timu na ni mchezaji wa Geita Gold anahitajika kambini haraka na taarifa za yeye kuwa na madai na sisi sio za kweli hakuna anachotudai na hawezi kuwa mkubwa zaidi ya klabu anahitajika uwanjani aonyeshe kuwa ni mchezaji mzuri kwa kucheza sio kutumia alichokifanya msimu uliopita,”alisema huku viongozi wa chama cha soka cha Geita wakidai hawajapata malalamiko rasmi kinachoendelea ndani ya timu hiyo iliyokuja kwa kasi msimu uliopita.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUSEPESHWA YANGA...KONKONI AENDELEA KUANIKA YA MOYONI...AITAJA SIMBA...