Home Habari za michezo PAMOJA NA KUSEPESHWA YANGA…KONKONI AENDELEA KUANIKA YA MOYONI…AITAJA SIMBA…

PAMOJA NA KUSEPESHWA YANGA…KONKONI AENDELEA KUANIKA YA MOYONI…AITAJA SIMBA…

Habari za Yanga

STRAIKA Hafiz Konkoni anayejiandaa kuondoka nchini kwenda kujiunga na timu ya Dogan Tûrk Birligi ya Cyprus kwa mkopo hadi mwisho wa msimu akitokea Yanga, amefichua kwamba, anawaona mabingwa hao wa nchi, wakifika mbali katika mechi za kimataifa, huku akiichomoa Simba akidai labda itokee tu.

Konkoni aliyesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Bechem United ya Ghana kwa lengo la kuziba pengo lililoachwa na Fiston Mayele aliyepo kwa sasa Pyramids ya Misri, alishindwa kupata namba katika kikosi cha kwanza, kabla ya uongozi kuamua kumtoa kwa mkopo Birligi kupitia dirisha dogo lililofungwa juzi Jumatatu.

Akizungumza jana usiku wakati akijiandaa na safari ya kuondoka nchini, Konkoni amesema anasikitika kuachana na Yanga katika kipindi hiki, kwani alikuwa anaiona nafasi yake kikosini kama angeendelea kuaminiwa, lakini kwa vile imeshatokea hana budi kukukubali, akiitabiria pia kufanya makubwa.

Konkoni amesema Yanga inaundwa na wachezaji wenye viwango bora na wanaojituma uwanjani, ndio maana hata yeye alikuwa akipata ugumu kupenya kikosi cha kwanza na kwamba anaiona timu hiyo ikifika mbali zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kulinganisha na watani wao wa jadi, Simba.

“Niwe muwazi kuwa, Yanga ina kikosi kizuri na wachezaji bora, naiona ikifika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kuliko Simba kwani Yanga ina wachezaji wazuri sawa na Simba ila tofauti yao ni moja tu fitnesi. Yanga ina fitnesi ya hali ya juu kuliko Simba. Lakini mpira una maajabu yake wote nawatakia heri kwenye mashindano hayo,” amesema Konkoni.

Mshambuliaji huyo ameongeza kuwa, anaondoka Yanga akiwa bado anaipenda na deni kubwa la kushindwa kutimiza malengo ya usajili ndani ya klabu hiyo.

“Haikuwa muda sahihi kwangu kuondoka Yanga, bado nina deni kubwa kwa mashabiki kwa vile sikupata nafasi ya kuitumikia vya kutosha, lakini sina namna. Nimeshaenda kuwaaga wachezaji wenzangu pamoja na kocha na kuitakia kila la kheri wakati najiandaa kwenda kuanza maisha mapya katika timu nitakayoitumikia.”

Hadi anaondoka Yanga, Konkoni ameifungia timu hiyo mabao mawili tu, likiwamo moja la Ligi Kuu Bara katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya KMC na jingine kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asas ya Djibouti iliyofumuliwa mabao 5-1.

Nafasi ya mchezaji huyo mrefu ndani ya Yanga imezibwa na mshambuliaji mpya Joseph Guede kutoka Ivory Coast aliyetambulishwa muda mchache kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Jumatatu usiku, akiwa ni mchezaji wa pili baada ya Mghana Augustine Okrah aliyechukua nafasi ya Jesus Moloko aliyeachwa.

SOMA NA HII  AZAM FC WAWEKA KAMBI KILIMANJARO