Home Habari za michezo KWA HILI LA MANULA HAPANA AISEE…ISHAKUWA ‘TO MUCH’ SASA…..

KWA HILI LA MANULA HAPANA AISEE…ISHAKUWA ‘TO MUCH’ SASA…..

Habari za Simba SC

Aishi Manula ni kipa mzuri sana. Ana vitu vingi ukilinganisha na makipa wetu wazawa wengine waliopo Ligi Kuu.

Kuanzia kwa kina Metacha Mnata, Aboutwalib Msheri, Beno Kakolanya na kadhalika. Kwa muda sasa amekuwa akilinganishwa na kushindanishwa na makipa wazawa na hata wa kigeni, lakini amekuwa kinara na kuwaacha akibaki kuwa namba moja kuanzia Simba hadi timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Kulikuwepo na makipa wengi siku za nyuma waliofanya mambo makubwa kuanzia kwa kina Steven Nemes, Mohammed Mwameja, Juma Kaseja na hata Juma Pondamali ‘Mensah’ lakini baada ya kuibuka Manula miaka ya 2010 akiwa kijana mdogo kutoka Mtibwa Sugar na kujiunga na Azam FC na mpira wa Tanzania.

Nje ya kuitwa ‘Tanzania One’ lakini kwa sasa pia anaitwa ‘Air Manula’ wajuzi wa mambo wakilinganisha uwezo wake wa kuruka akiwa langoni wakati wa kuokoa michono. Manula ana vitu vingi vya kumuelezea kwa kuwa ana mafanikio mengi na makubwa katika soka kuanzia Azam FC hadi Simba na ameshinda mataji mbalimbali pamoja na tuzo binafsi za ubora.

Tangu akiwa Azam FC kabla ya kutua Simba miaka ya nyuma aliwahi kushinda tuzo za kipa bora mara nne mfululizo kabla ya kusimamishwa na kipa wa Yanga, Djigui Diarra msimu uliopita.

Lakini nje ya mazuri yote aliyokuwa nayo Manula kuna eneo ana udhaifu na unaweza kusema labda makocha wa makipa Simba na timu ya taifa wanashindwa kuutibu. Tatizo alilo nalo ni la kufungwa mashuti ya mbali.

Kila kipa ana upungufu wake ambao kuwepo kwa benchi la ufundi linalohusisha kocha wa makipa moja kwa moja ni jukumu lao mama kumsaidia kipa au makipa kuondokana na changamoto zinazowakabili ili wawe bora zaidi

Kuna kipindi kwenye klabu ya Chelsea kipa ghali zaidi duniani, Kepa Arrizabalaga alikuwa anachomesha sana kwa kufungwa mabao ya kizembe tena mepesi na Chelsea wakaenda mbali zaidi na kumsajili Edouard Mendy ambaye naye pia alikuja kuwa shati, lakini walichofanya eneo la makipa kwa maana ya makocha Chelsea walienda moja kwa moja kutibu tatizo la Kepa kufungwa mabao mepesi.

Katika hilo walizungumza mara kwa mara na mabeki wake huku akiambiwa kuwa anatakiwa kuwa makini muda wote wa mchezo, hali inayompa kiwango kizuri kwa sasa. Nje ya Kepa wakati wa ujio wa David De Gea kwenye timu ya Manchester United 2011 moja ya tatizo alilokuwa nalo lilikuwa la kukosa nguvu ya mikono kucheza mipira inayopigwa kwa kasi kwenda golini kwake na kutoona kwa ukaribu likisababisha kufungwa mabao kirahisi.

Lakini makocha wa makipa walifanya kazi na baadaye De Gea alikuja kuwa kipa hatari licha ya sasa kuwa na changamoto ya kuwa na kiwango cha maji kupwa na maji kujaa.

Lakini tukirudi kwa kipa wetu wa nchi, Manula, nje ya ubora wake amekuwa na tatizo la kufungwa mabao ya mbali. Msimu huu tu mpaka sasa katika mabao manne ambayo Simba wameruhusu kwenye ligi, Manula ameshafungwa matatu ya mbali, ukiliacha bao la juzi juzi tu la Prince Dube wa Azam katika zile dakika za 35 za kuupiga mpira kwa umbali mrefu na kumfunga Tanzania One.

Kuna mabao mawili ambayo Manula amefungwa kwa mashuti ya mbali ambayo ni kwenye sare ya 2-2 dhidi ya KMC – kipa huyo alifungwa bao la mbali na kiungo George Makang’a na pia kwenye dabi ya Kariakoo ya hivi karibuni alifungwa kwa shuti la mbali na Stephane Aziz Ki kwa mtindo wa ‘free kick’ baada ya Aucho kufanyiwa madhambi jirani na eneo la 18 la Simba

Pia kiungo huyo wakati akiwa Asec Mimosas alimfunga Manula kwa shuti la mbali katika ushindi wa timu hiyo wa mabao matatu wakiwa kwao na bado kuna mabao ya mbali aliyofungwa dhidi ya Caostal Union, RS Berkane, AS Vita na Alliance ile ya 2018/19

Ukiangalia mabao yote hayo kwa wenzetu hii lingekuwa faida kubwa kwa timu pinzani hasa wakati wanacheza na Simba, lakini bahati mbaya sana klabu zetu huwa hazitumii udhaifu wake kwa kuwa hazina watu bora kuizidi Simba. Lakini wasiwasi wangu upo katika michuano ya kimataifa ya Afrika iwe ngazi ya klabu au taifa pindi linapotafuta tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa wanaweza wakawa na nafasi kubwa ya kutumia udhaifu wa Manula kufungwa mabao mengi ya mbali na kumfunga kwa urahisi.

Hii ni mbaya sana Simba. Haraka sana waendelee kuleta makocha wa makipa ili watibu changamoto alinayo Manula maana sasa Simba ni wakubwa kwa kiasi chake Afrika, hivyo klabu nyingi huifuatalia na zikiona zina faida ya kushinda mchezo kupitia eneo la kipa itakuwa njia rahisi kupata matokeo.

Inawezekana Simba hawajui au wanamuonea aibu ama ni mazoea tu na wameamua kumuacha aendelee kama alivyo. Kuwa na changamoto ya kuruhusu mabao ya mbali, lakini hili lingekuwa suala la kuambiwa anula na kupewa mazoezi binafsi zaidi ili kutibu changamoto aliyonayo

Najiuliza kama kipa wa nchi ana upungufu huo hawa makipa wengine wana hali gani? Kwa sasa ili kukiokoa kipaji chake hakuna namna zaidi ya kumsaidia kiufundi ili Simba wakati wanashiriki michuano ya kimataifa kusiwe na wasiwasi wa kufungwa mabao ya mbali kama ambavyo wanafungwa sasa. Kadri siku zinavyozidi kwenda hii changamoto kwa Manula inazidi kuwa kubwa.

Kule kwenye uwanja wa mazoezi kuwe na kazi kubwa inayotakiwa kufanywa ili kumpunguzia changamoto aliyonayo au kuiondoa kabisa ya kufungwa mabao ya mbali maana kina Aziz KI, Makang’a na Prince Dube kwenye michuano ya kimataifa wapo wengi sana.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA LIGI NA AZAM FC...MASTAA SIMBA WAPEWA 'HONEY MOON' YA SIKU 10...