Home Habari za michezo OKWA : MO DEWJI ALINITAKA NIJE SIMBA…KWA MAISHA YA HAPA KLABUNI…NI DENI...

OKWA : MO DEWJI ALINITAKA NIJE SIMBA…KWA MAISHA YA HAPA KLABUNI…NI DENI TU…U

BAADA ya kuonyesha kiwango bora kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita michezo miwili hatua ya awali akiwa na Rivers United, Nelson Okwa dhidi ya Yanga aliwavutia mabosi wa Simba.

Okwa aliyekuwa nahodha wa Rivers United ya Nigeria alionyesha kiwango bora ikiwemo kuwasumbua mabeki wa Yanga kwenye michezo yote miwili na kuivusha timu hiyo ya Afrika Magharibi hatua inayofuata.

Mabosi wa Simba walivutia wa huduma yake hadi kupambana kukamilisha usajili wake kwenye dirisha kubwa la usajili msimu licha ya kwamba bado alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Rivers United.

Gazeti la Mwanaspoti lilikutana na Okwa nyumbani kwake na kuzungumza mambo mengi ikiwemo yale aliyokutana nayo kabla ya kutoa Simba na hata baada ya usajili wake kukamilika kwenye klabu kubwa aliyokuwa akitamani kuichezea katika historia yake ya maisha.

KUTUA SIMBA

“Nakumbuka kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya uongozi wa Simba na Rivers United ila ulikuja kumalizwa na Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ na jambo langu halikuwa na ugumu tena,” anasema Okwa na kuongeza;

“Mo Dewji alikuwa karibu na mmoja wa kiongozi wa juu wa Rivers United waliongea hao wawili na walikubaliana kwahiyo hawa wa chini walikosa nguvu ya kunizuia na kuniacha nikajiunga na Simba,”

KWA NINI HACHEZI?

“Simba nilimalizana nao muda ambao timu ipo Misri kwenye maandalizi ya msimu na nilitakiwa kwenda huko moja kwa moja kwa ajili ya kufanya mazoezi pamoja na wachezaji wenzangu,” anasema Okwa na kuongeza;

“Kwetu Nigeria kuna ugumu kupata visa ya kuingia Misri kutokana na sababu za kinchi ilinichukua zaidi ya wiki mbili na bado ilishindikana kupata nikajikuta hadi muda wa maandalizi ya msimu kule Misri umepita,”

“Ikabidi nifanye tu taratibu za kuja Tanzania kujiunga na timu huku na hiyo ilikuwa changamoto kubwa hadi kushindwa kuwepo ndani ya kikosi kwa wakati.”

“Ili kufanya vizuri kwenye maisha ya soka inahitaji kufanya maandalizi ya kutosha kuandaa mwili kuwa katika utimamu na ushindani hilo kwangu lilikosekana pengine ndio maana nakutana na majeraha ya mara kwa mara,” anasema Okwa na kuongeza;

“Wakati wenzangu wapo Misri kwenye maandalizi ya msimu huu nilikuwa nafanya mazoezi yangu binafsi mbalimbali lakini si bora kama yale ambayo niliyotakiwa kufanya na wachezaji wenzangu tena chini ya benchi la ufundi.

“Miongoni mwa eneo muhimu kwa mchezaji kufanya maandalizi ya msimu ni Pre- season kukosekana kwake kwangu imenibidi wakati huu mechi za kimashindano zikiendelea huku nafanya mazoezi mengi binafsi ili kutengeneza utimamu wa mwili kuwa kama wenzangu.”

NAMBA KIKOSINI

Okwa anasema nafasi zote za ushambuliaji ambazo anacheza kuna wachezaji wenye uwezo wanafanya vizuri hivyo analielewa hilo na ndio maana ameamua kuwa mtulivu. “Ili timu iweze kufanya vizuri na kuwa kubwa inahitaji wachezaji wenye uwezo kwenye kila nafasi moja ili washindane na yule ambaye atakuwa bora zaidi ya mwenzake kupewa nafasi ya kuiwakilisha timu kulingana na mechi husika,” anasema Okwa.

“Hadi Simba ilinisajili basi kuna uwezo waliona kwangu na waliamini naweza kuongeza nguvu ya timu naamini huu ushindani wa nafasi ya kucheza utaniongezea hali ya kushindana na nitapata nafasi ya kucheza bila shida yoyote kwani naamini kwenye uwezo wangu.

“Si rahisi kwetu Nigeria kupata nafasi ya kuitwa timu ya taifa kwa wachezaji wa ndani, kuwa nahodha wa Rivers United kuna kitu cha zaida nilikuwa nacho naamini hata hapa Simba naweza kukionyesha kwani ukiangalia sijaanza msimu vibaya.”

ZORAN AMCHEKI

Wakati Okwa anasajiliwa na kutambulishwa kuwa mchezaji mpya wa Simba kikosi kilikuwa chini ya kocha, Zoran Maki ambaye hakudumu kwenye kwa kushindwa kufanya vizuri pamoja na mambo mengine, lakini Okwa anasema kabla ya kutambulisha akiwa Nigeria alipokea simu ya Zoran aliyemuelezea kuvutiwa na ubora wake baada ya kuambia watafanya kazi pamoja.

“Hata baada ya kuwasili hapa nchini Zoran alifurahi na kunieleza anaamini kwenye ubora wangu na kunitaka nionyeshe kiwango kilichokuwa bora zaidi ya kile cha Rivers ili kuisaidia timu,” anasema Okwa na kuongeza;

“Jambo hilo la kuwasiliana na kocha kabla ya kujiunga na timu hata nilivyofika alinipokea vizuri niliamini nipo kwenye mazingira salama ya kufanya kazi na yote aliyoniambia nilipanga kuyatimiza uwanjani,”

“Haikuwa bahati nzuri kwetu kwani ndani ya muda mfupi baada ya msimu kuanza alikuja kambini kutuaga wachezaji wote kuwa amepata changamoto kwenye timu nyingine na hatakuwa nasi tena.”

YANGA ILIVYO

Anasema Yanga msimu huu imeonekana kuimarika na kikosi chake kinaweza kuleta ushindani kwenye mashindano ya ndani na sio yale ya kimataifa.

“Kwenye mashindano ya CAF, si rahisi kufanikiwa kwa mara moja kunahitaji kupitia hatua kwa hatua na Yanga lazima iwe hivyo kwani hata Simba haikufanikiwa na kuwa wakubwa kwa mara moja,” anasema Okwa na kuongeza;

“Kwenye mashindano ya ndani wachezaji wa Simba kabla ya msimu kuanza na tumekuwa tukihamasishana wenyewe kwa wenyewe hatutakubali kuona wanatawala kama ilivyokuwa msimu uliopita,”

“Wachezaji wa Simba tutakwenda kutoa ushindani ya kutosha kufanya vizuri kuliko Yanga na timu nyingine yoyote kwenye mashindani ya ndani pamoja nja Ligi ya mabingwa Afrika tulikotimiza lengo la kwanza kucheza hatua ya makundi.”

UBORA WA AZAM

Okwa anasema hakuwa anaifuatilia Azam, lakini baada ya kufika hapa nchini alipata muda huo ikiwemo kuijua timu hiyo vizuri kutokana na anavyoiona pamoja na kuelezwa wakati wanajiandaa kucheza nayo.

Anasema Azam timu nzuri yenye wachezaji bora wanaoweza kuleta ushindani kwenye michezo ya ligi kwani hata mechi waliyopoteza dhidi yao haikuwa kazi rahisi kama wasingekuwa na ubora.

“Naamini Azam ni miongoni mwa timu bora inayoweza kuleta ushindani katika mashindano ya ndani kutokana na uimara wao kwenye baadhi ya michezo niliyopata muda wa kuwaangalia,” anasema Okwa.

BENCHI LA UFUNDI

Simba baada ya kuondoka kwa Zoran pamoja na wasaidizi wake imefanya maboresho kwenye benchi la ufundi kumleta, Juma Mgunda anayeonekana kupata matokeo bora kwenye mashindano yote tangu alipoanza kazi hiyo.

Okwa anasema mabadiliko hayo yamekuwa na maana kubwa ndani ya kikosi chao kwani kila mchezaji ameongeza nguvu ya kupambana na kuamini anaweza kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.

Anasema Mgunda amekuwa kama baba ndani ya timu na hakuna mchezaji atakubali kuona anashindwa kufanya vizuri na kumuangusha kocha ambaye mbali ya vitu vya uwanjani amekuwa pamoja na wachezaji.

“Chini ya Mgunda Simba imefungwa mechi moja tu dhidi ya Azam, embu angalia kocha ambavyo aliongea vizuri baada ya mchezo kuisha kuwa lawama zote apewe mwenyewe jambo ambalo wachezaji lilitupa matumaini mapya,” anasema Okwa.

“Kila mchezaji katika moyo wake benchi hili la ufundi lililopo wakati huu amefurahishwa nalo na amekuwa akifanya kazi kwa ukaribu bila shida yoyote.”

DENI KWA MASHABIKI

Okwa anasema bado ana deni kubwa analotakiwa kulilipa kwa wapenzi na mashabiki wa Simba kutokana na matumaini makubwa naye, lakini amekutana na changamoto ya majeraha na kushindwa kuonyesha ubora wake.

Anasema alipokea maoni mazuri kutoka kwa mashabiki wa Simba baada ya kutambulishwa ndani ya kikosi hicho na hata alipocheza mechi ya kwanza dhidi ya St George kutokea Ethiopia ilikuwa hivyo.

“Moyoni kwangu nipo na deni kubwa natakiwa kulilipa kwa mashabiki wa Simba kwani wameweka imani kubwa kwangu kwa kuamini naweza kufanya vitu vingi bora kwenye mechi za mashindano mbalimbali,” anasema Okwa na kuongeza;

“Hakuna njia nyingine ya kulipa deni hilo bali natakiwa kurejea uwanjani kwa nguvu kuhakikisha napata nafasi ya kucheza na kutoa mchango kwa timu kufanya vizuri kwa kuonyesha kiwango bora,”

“Ubora wa mchezaji unaonekana pale kwenye kutimiza majukumu ya nafasi yake kwenye michezo mfululizo.”

MAISHA MAZURI SIMBA

Okwa anasema mchezaji wa Simba kushindwa kucheza mpira na kushindwa kuisaidia timu uwanjani hilo linaweza kutokana na changamoto nyingine na si maisha wanayoishi wachezaji.

Anasema tangu amefika Tanzania amepewa nyumba nzuri ya kuishi na kupata mahitaji yote ya msingi kwa wakati maslahi aliyokubaliana na uongozi wakati anasaini mkataba yote amepatiwa.

“Deni kubwa limebaki kwangu kufanya kazi ile Simba inahitaji kuona naisaidia timu kwani nimepatiwa kila stahiki yangu na naishi kwenye maisha mazuri anayofaa kuwa mchezaji,” anasema Okwa na kuongeza;

“Simba ni timu kubwa si kwangu tu bali hata wachezaji wenzangu wengine wote wamekuwa wanaishi kwenye mazingira mazuri kama tukiwa pamoja kambini vile.”

MASHINDANO YA CAF

Okwa anasema lengo la kwanza lilikuwa kufika makundi na wamefanikiwa hilo baada ya hapo wameweka lengo lingine la kufika robo fainali ya mashindano hayo.

Anasema kulingana na hamu ya wachezaji kufanya katika mashindano hayo msimu huu wamejiwekea malengo ya kuvuka robo fainali ambayo kwenye misimu kadhaa nyuma wamefikia hatua hiyo.

“Mashindano haya ni magumu kutokana tunaenda kukutana na wachezaji na timu bora kama ilivyo kwa upande wetu kwa maana hiyo kutakuwa na ushindani wa kutosha katika kila mechi,” anasema Okwa;

“Simba ishacheza robo fainali tatu CAF, sasa ili kuonyesha hamu ya mafanikio msimu huu tutapambana ili kufika nusu fainali au fainali kabisa, sio kazi rahisi lakini inawezekana.”

SOMA NA HII  CAF YAIRUDISHA SIMBA MOROCCO...KUVAANA NA WAKALI HAWA ROBO