Home Habari za michezo RASMI…MGUNDA AKABIDHIWA JAHAZI SIMBA…ADEL ZRANE KUONGEZA NGUVU..’TRY AGAIN’ ATOA BARAKA…

RASMI…MGUNDA AKABIDHIWA JAHAZI SIMBA…ADEL ZRANE KUONGEZA NGUVU..’TRY AGAIN’ ATOA BARAKA…

Habari za Simba

Simba imeendelea kunoga baada ya juzi kuichapa Mtibwa Sugar mabao 5-0 huku kaimu kocha mkuu, Juma Mgunda akitaja majembe yake mapya ya ushindi kuwa ni Moses Phiri, Augustine Okrah, Pape Sakho, Clatous Chama na Habib Kyombo.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi mnono na kupanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 17, tatu nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 20.

Akizungumza Mgunda ambaye ni kocha wa zamani wa Coastal Union, alieleza haikutokea ghafla tu kushinda mabao matano ambayo ndio mengi zaidi kufungwa kwenye mchezo mmoja na timu moja kwenye ligi hadi sasa bali ni maandalizi makubwa waliyofanya mazoezini na kuwapongeza wachezaji wake kwa kufanikisha hilo.

Mgunda, amelitaja eneo la ushambuliaji lililo chini ya Phiri, Okrah, Sakho, Kyombo na Chama kumkosha zaidi kwa kile wanachokifanya na kuwataka kuendele kufanya vizuri zaidi.

Hadi sasa Simba ndiyo inaongoza kwa mabao mengi kwenye ligi (17) na kuwa timu iliyofungwa machache zaidi (4) huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa ndiyo inaongoza kwa kupachika mabao mengi.

Mabao hayo ya Simba, 14 yamefungwa na washambuliaji akiongoza Phiri mwenye matano, akifuatiwa na Okrah (3), Sakho (2), Kyombo (2), Chama (1) na Dejan Georgijevic aliyeondoka na bao moja huku mengine mawili yakifungwa na viungo Mzamiru Yassin na Jonas Mkude wenye moja kila mmoja na jingine likiwa ni la kujifunga kwa beki wa Dodoma Jiji, Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Mgunda alisema makali hayo ya kikosi chake, yanakuja kutokana na namna anavyokaa na mastaa wake na kuwafundisha namna ya kucheza kama timu ili kufunga zaidi na kuipa timu matokeo chanya.

“Kadri siku zinavyozidi kwenda naona mabadiliko mazuri ndani ya kikosi changu na wachezaji wanaanza kucheza vile ninavyotaka na tunavyowaelekeza mazoezini,” alisema na kuongeza:

Maeneo yote yako vizuri lakini hapo awali tulikuwa na shida ya kupata mabao mengi licha ya kutengeneza nafasi za kutosha na kushindwa kuzitumia lakini kwa sasa tumeendelea kuimarika na washambuliaji wangu wameanza kucheza kwa maelewano, jambo ambalo ni zuri kwa timu.

“Timu nzuri ni ile inayopata matokeo na kucheza vizuri, Simba kwa sasa tunafanya hivyo na tutaendelea kuboresha pale tunapokosea ili kuendelea kuwa bora zaidi.”

Mgunda aliichukua Simba Septemba 8, mwaka huu akitokea Coastal Union na kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mserbia Zoran Maki na tangu ameichukua ameiongoza katika mechi tano za ligi akishinda tatu, sare moja na kupoteza moja huku pia akishinda zote nne za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyassa Big Bullets ya Malawi na Premiero de Agosto ya Angola nyumbani na ugenini na kuipeleka Simba hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika huku ikicheza vizuri.

Mgunda anayetamba kwa sasa na kauli yake ya ‘boli litemembea’ alizungumzia pia mechi ijayo dhidi ya Dodoma Jiji itakayopigwa Novemba 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Liti Singida dhidi ya Singida Big Stars na kuweka wazi kujipanga kufanya vizuri zaidi.

“Kumalizika kwa mechi ndio mwanzo wa maandalizi ya mechi ijayo, tunarudi kambini kujipanga kwa ajili ya mechi yetu dhidi ya Singida. Tumewaona wakicheza na wana timu nzuri hivyo tukiwa kambini kwetu tutaanda mbinu na njia sahihi za kupambana nao ugenini na kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Mgunda.

KULETEWA MTAALAM

Uongozi wa Simba umempa nafasi Mgunda ya kusaka kocha wa viungo anayeona anafaa kuwaweka fiti wachezaji wake ili kuepukana na majeraha ya mara kwa mara na miongoni mwa makocha wanaotajwa ni Mtunisia Adel Zrane aliyewahi kufanya kazi ndani ya Simba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema benchi la ufundi lina utulivu mkubwa na mpango wowote wa kuliongezea nguvu Mgunda ndio mwenye uamuzi wa mwisho na imefanya hivyo ili kumpa nguvu na kuiwezesha timu ifanye vizuri.

“Kabla ya kupoteza dhidi ya Azam wachezaji na benchi la ufundi walitumia nguvu na akili kubwa kwenye dabi ila ushindi mnene na Mtibwa umerudisha hali na morali ndani ya timu na huo utakuwa muendelezo wetu kwenye mashindano yote,” alisema Try Again na kuongeza;

“Kikosi chetu kitakuwa na maboresho kwa sababu muda utaruhusu ikiwemo kutumia vyema dirisha dogo la usajili kwani kuna maeneo tutaongeza wachezaji wapya ila yote hayo mwenye uamuzi wa mwisho ni Mgunda.

“Niwaeleze mashabiki wa Simba watulie kwani mipango ya uongozi ili timu ifanye vizuri kwenye mashindano yote ni mikubwa mno kama ambavyo wachezaji wameahidi kupambana na kujitolea msimu huu ili kufikia mafanikio.”

SOMA NA HII  KUHUSU WANAOMPINGA MANGUNGU SIMBA....AHMED ALLY KAIBUKA NA 'KIJEMBE' HIKI KWAO...