Home Habari za michezo UKWELI MTUPU….RATIBA LIGI KUU YAISHIKA PABAYA SIMBA…WAKIJITINGISHA TU..YANGA BINGWA TENA…

UKWELI MTUPU….RATIBA LIGI KUU YAISHIKA PABAYA SIMBA…WAKIJITINGISHA TU..YANGA BINGWA TENA…

Kikosi cha Simba SC Msimu huu wa 2022/23

Historia ya kutofanya vizuri katika viwanja vya mikoani katika miaka ya hivi karibuni, inailazimisha Simba kuchanga vyema karata zake katika mechi sita mfululizo zijazo za Ligi Kuu ili isipate matokeo yanayoweza kuweka rehani malengo yake kutwaa ubingwa msimu huu.

Mechi hizo sita zinazofuata za Simba ambazo zitachezwa ndani ya siku 34, zitakuwa katika viwanja vitano vilivyopo katika miji tofauti ambayo timu zitakazokabiliana na Simba zinatumia kama vituo vya mechi kwa mechi zao za nyumbani.

Simba imekuwa na historia ya kutofanya vyema sana katika mechi zao za nje ya Uwanja wa Mkapa, ambao wanautumia kwa mechi zao za nyumbani.

Katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu ambazo Simba imecheza nje ya Dar es Salaam, imepata ushindi mara mbili tu, ikitoka sare sita na kupoteza mechi mbili.

Ratiba hiyo ngumu kwa Simba itaanzia kesho katika mchezo baina ya Simba na Mbeya City itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na baada ya hapo itakuwa na siku nne za kusafiri na kujiandaa na mechi dhidi ya Polisi Tanzania itakayochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro, Novemba 27.

Desemba 3, Simba itakuwa mkoani Tanga kumenyana na Coastal Union na baada ya hapo itakwenda Mwanza kukabiliana na Geita Gold, Desemba 18, kisha siku tatu baadaye itakabiliana na Kagera Sugar ugenini.

Baada ya kumalizana na Geita Gold na Kagera Sugar, Simba itakuwa na kibarua kingine Desemba 26 dhidi ya KMC, ambao mechi zao za nyumbani dhidi ya Simba wamekuwa wakicheza nje ya Dar es Salaam.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu aliliambia gazeti hili kuwa wamejipanga kukabiliana na ratiba iliyo mbele yao na hawako tayari iwe kisingizio kwao.

“Ratiba ni ngumu kweli, lakini mwisho wa siku hatuko peke yetu wenye hiyo ratiba, hivyo hatupaswi kuanza kuilalamikia. Tunatakiwa twende tukakabiliane nayo maana si sisi pekee, hata wengine pia nao inawabana.

“Changamoto ipo kiukweli, ligi ngumu na muda hautoshi lakini hatuna namna, inabidi tupambane kwa kweli ili ufanye vizuri,” alisema Rweyemamu.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema wamejiandaa na ratiba ngumu iliyopo mbele yao.

“Kama timu tunalazimika kuheshimu na kufuata kile kinachopangwa na mamlaka inayosimamia ligi, hivyo kwa vile ratiba tayari ipo, tutajipanga kuhakikisha tunakabiliana nayo na kuona ni kwa jinsi gani tutapata matokeo mazuri,” alisema Mgunda.

Ugumu wa ratiba ambao Simba watakabiliana nao, ni kama ule ambao walikutana nao Oktoba, walipocheza mechi sita za mashindano tofauti ndani ya siku 29, ambazo waliangusha jumla ya pointi nne kwa kupoteza mmoja kati ya hiyo na kutoka sare moja.

Ilikuwa na mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola ambazo ilishinda zote, lakini pia ikawa na mechi nne za Ligi Kuu Tanzania Bara.

SOMA NA HII  KUMBE HIKI NDIO CHANZO CHA SIMBA KUFUNGWA NA YANGA...ISHU NZIMA A-Z HII HAPA