Home Habari za michezo YANGA VS WAARABU…NABI ALIFAULU KWENYE HILI…REFA HAKUWA NA MBAMBAMBA…

YANGA VS WAARABU…NABI ALIFAULU KWENYE HILI…REFA HAKUWA NA MBAMBAMBA…

NI mechi ya kiume ambayo Yanga waliicheza kiume hadi kupata ushindi wa kibabe wa bao 1-0, ugenini huko Tunisia dhidi ya Club Africain ya huko, uliowavusha na kuwapeleka katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ushindi huo ulioambatana na kiwango bora cha Yanga kwenye nyasi za Uwanja wa Olimpiki Rades, haukupatikana kirahisi bali ni matokeo ya juhudi za pamoja za kitimu kuanzia uongozi, benchi la ufundi na wachezaji kabla na wakati wa mchezo huo hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.

Stephane Aziz Ki anaweza kukumbukwa na kubaki historia kwa kufunga bao hilo pekee la Yanga lakini hakuna namna ambayo benchi la ufundi chini ya kocha Nasreddine Nabi linaweza kumwagiwa sifa kama msanifu mkuu wa mchoro na utendaji kazi wa kitimu kiujumla hadi kupelekea historia hiyo kuandikwa.

Nabi alifaulu hapa

Upangaji wa kikosi kilichoanza katika mchezo wa juzi ulionyesha wazi kuwa Yanga haikutaka kuingia kinyonge katika mchezo ule na ilipania kuwashangaza wenyeji jambo ambalo lilitimia.

Nabi alifanya mabadiliko matatu katika kikosi chake kilichocheza mchezo wa kwanza ambao ulimalizika kwa sare tasa hapa Dar es Salaam ambapo ukiondoa Djuma Shaban aliyebakia nchini kutokana na majeraha ambaye nafasi yake ilizibwa na Joyce Lomalisa, Nabi aliwaanzisha Ducapel Moloko aliyechukua nafasi ya Tuisila Kisinda na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye alianza badala ya Stephane Aziz Ki.

Hii ilimaanisha nini? Moloko, Morrison pamoja na Fiston Mayele pindi Yanga ilipokuwa haina mpira walianza kukabia katika mstari wa juu jambo lililowanyima fursa Club Africain kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma na kujikuta wakilazimika kupiga mipira mirefu ambayo iliokolewa vyema na wachezaji wa Yanga.

Kuna wakati Moloko na Morrison walivutika ndani na kuwalazimisha walinzi wa pembeni wa Club Africain kutopanda na kuachia nafasi ambazo mabeki wa Yanga wa kulia na kushoto, Kibwana Shomari na Joyce Lomalisa walizitumia vyema kupiga krosi kuelekea langoni mwa wapinzani jambo lililowapa hofu wenyeji kutopanda mbele kushambulia mara kwa mara.

Yanga walivuja jasho hasa

Ni mchezo ambao kila mchezaji wa Yanga alionekana kutimiza wajibu wake ndani ya uwanja na pengine ni vigumu kuteua mchezaji bora wa mechi kwa upande wao jana.

Yanga walikimbia kilomita nyingi pindi walipokuwa na mpira na pale ambapo hawakuwa nao, walishinda mipira mingi ya pili walipowania na wachezaji wa Club Africain, walikuwa na nidhamu ya juu ya kulinda na kushambulia na hawakuwapa mwanya wapinzani kuleta madhara langoni mwao.

Kuthibitisha hilo, hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika, Club Africain walipiga shuti moja tu lililolenga lango ambalo walipata katika dakika za mwisho za kipindi hicho.

Sure Boy, Diarra hatari

Kama kuna watu ambao watabakia vichwani mwa wachezaji wa Club Africain basi ni kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kipa Djigui Diarra na mshambuliaji Bernard Morrison.

Kiwango bora katikati mwa uwanja cha Sure Boy katika kuichezesha, kuisogeza timu mbele kwa haraka na kupiga pasi zilizofikia walengwa kwa usahihi, kilitibua mipango mingi ya Club Africain.

Diarra na Morrison waliwatoa mchezoni wachezaji wa Club Africain mara kwa mara jambo lililowaondolea utulivu wapinzani wao na kushindwa kuwa na hatari kwao katika dakika nyingi za mechi.

Refa hana baya

Mwamuzi Issa Sy wa Senegal alizitafsiri vyema na kwa haki sheria za mpira wa miguu na hakutoa aina yoyote ya upendeleo kwa timu zote mbili.

Licha ya wenyewe kutaka kumhadaa mara tatu tofauti refa huyo ili awazawadie pigo la penalti, Sy alisimama imara na kutoingia katika mtego wa wachezaji wa Club Africain. Matokeo hayo yameifanya Yanga kuweka rekodi ya kibabe Arabuni ambayo imekuwa nadra kwa timu za Afrika Mashariki.

SOMA NA HII  RASMI....SIMBA WAANIKA ISHU YAO NA BOBOSI ILIVYO....MANZOKI ATAJWA...