Mashabiki wa Simba bado wapo njia panda baada ya Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez kutangaza ghafla kujiuzulu, huku kukiwa na tetesi za chinichini kwamba mambo sio mambo Msimbazi.
Barbara alitangaza juzi jumamosi uamuzi wake huo, kwa kuandika taarifa mtandaoni, akiweka bayana mambo makuu mawili, ambayo hata hivyo yameibua maswali mengi kwa wanasimba wakiona hayana uzito mkubwa, kiasi cha kumfanya ‘Iron Lady’ huyo kujiweka kando kwa notisi ya mwezi mmoja.
Mwanadada huyo, alitangazwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Mohamed ‘MO’ Dewji Septemba 5, mwaka 2020 kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu kuchukua nafasi ya Senzo Mazingisa aliyekuwa ametimkia Yanga wakati huo.
Barbara ameitumikia nafasi hiyo kwa miaka miwili kabla ya juzi kutoa taarifa hiyo ya kujiuzulu, huku akibebwa na rekodi mbalimbali alizoweka klabuni hapo kwa kuifanya Simba iwe tishio Afrika, licha ya kuelezwa alipitia changamoto nyingi ambazo baadhi ndizo zinazotajwa kumfanya ang’atuke.
Pamoja na waraka wake kuweka bayana mambo mawili yaliyomfanya atoe notisi hiyo ya mwezi mmoja hadi Januari ikiwamo kupisha uchaguzi mkuu utakaofanyika ndani ya mwezi, utakaotoa wajumbe wapya wa Bodi ya Wakurugenzi na pia kupisha kipindi cha mpito na kukabidhi ofisi, lakini Mwanaspoti imebaini mambo saba ambayo ndio yanayoelezwa yamemfanya Barbara kubwaga manyanga kuiongoza klabu hiyo, huku mwenyewe akifunguka japo kwa ufupi.
WAJUMBE WA BODI
Inaelezwa sababu ya kwanza iliyochangia kwa Barbara kufanya uamuzi wa kuondoka Simba ni kushindwa kuelewana vizuri na mabosi wake wakiwamo Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
Inadaiwa kuna nyakati iliwahi kutokea Barbara na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kukosa maelewano mazuri hadi kushindwa hata kuongeleshana.
Kuna mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi mwenye nguvu (jina lake tunalo), aliamua kujitoa hadi kwenye kundi la (WhatsApp), kisa kushindwa kuwa na malewano mazuri na Barbara ila baada ya kipindi kirefu walikuja kusululishwa.
MASLAHI YA KLABU
Katika kipindi cha miaka miwili Barbara alichokuwa ndani ya Simba alionekana kuwa kiongozi mwenye malengo ya kuhakikisha mdhamini, Mo Dewji anatoa kiasi kidogo cha pesa kwenye uendeshaji wa timu huku akipunguza baadhi ya matumizi kwenye maeneo mengi.
Baadhi ya viongozi waliokuwa wakisimamia vitu mbalimbali kama usajili na mipango mingine walikuwa wakipeleka bajeti kwa Barbara alikuwa hakubaliani nazo na mara nyingi alikuwa akipunguza na kutoa kiasi kile alichokuwa anahisi ni sahihi kwenye jambo husika.
Katika kupunguza gharama za klabu, Barbara alipunguza hadi wafanyakazi ambao alishindwa kufanya nao kazi kwenye nyakati tofauti tangu alipopewa kazi hiyo.
Mvutano wa kimaslahi ulikuwa ni kati ya changamoto zilizokuwa zinamuweka, Barbara kwenye wakati mgumu akionekana kutoa pesa chache na nyingine kushindwa kuziruhusu zitoke kwa sababu alizokuwa akieleza.
VITA NA TRY AGAIN
Kati ya mambo makubwa yaliyochangia Barbara kuondoka ndani ya Simba ni hili, kwa kipindi kirefu sasa hakuna maelewano mazuri kati yake na bosi wake, Salim Abdallah ‘Try Again’. Try Again aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya Mo Dewji kujiondoa ili kubaki kuwa Rais wa Heshima wa klabu hiyo.
Inadaiwa wawili hao wameshindwa kuwa na maelewano zaidi, kila mmoja akiona ndiye anayestahili kusikilizwa, ikiwamo suala la kuingilia hata kwenye ishu za usajili, makocha na kusimamia nidhamu ya wachezaji, kitu ambacho kinaelezwa kimekuwa pia kikiwayumbisha wasimamizi wa kambi ya timu.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Simba, Try Again amemwekea Barbara mpango kazi, ambao muda mwingine amekuwa akishindwa kufanya kama vile makubaliano yao yalivyokuwa jambo ambalo limechangia kati ya wawili hao kuwa kwenye hali ya kutoelewana mara kwa mara.
Kuna muda shughuli za klabu zilikuwa zikifanyika bila ya wawili hao kuwa na mawasiliano hata ya simu na kila mmoja kuamua lile ambalo lipo ndani ya uwezo wake kulingana na wakati husika.
Uamuzi binafsi anaofanya Barbara kama kujipa likizo ya lazima, kuondoka wakati timu ipo kwenye mechi ngumu muhimu, kutokuwepo ofisini kwenye nyakati muhimu kama za usajili ni baadhi ya mambo yaliyokuwa yanamkera Try Again na kuzalisha tofauti kati yao.
UMOJA KUYUMBA
Miaka minne iliyopita Simba ilifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na ndani ikiwemo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwenye misimu hiyo mfululizo.
Kati ya silaha zilizokuwa zikichangia mafanikio hayo ni umoja uliokuwapo kwa viongozi hao wa juu na kila mmoja alifanya majukumu ya eneo lake ipasavyo na mwishowe matunda mazuri yalionekana.
Halikuwa jambo la kushangaza kuwaona Zacharia Hanspoppe (sasa marehemu), Mohamed Nassor, Mulamu Nghambi, Barbara, Try Again, Crescentius Magori na wengineo ukiwaona kwa pamoja kwenye matukio muhimu.
Viongozi hao kila mmoja alikuwa na majukumu yake kuhakikisha timu inafanya vizuri na walifanikiwa ila kuanzia msimu uliopita kutokana na kutokuwepo maelewano mazuri kati yao umoja huo uliondoka.
Kwa mfano msimu huu Simba inaweza kusafiri kwenye mechi za ugenini kiongozi ni mmoja tu Ofisa Habari, Ahmed Ally au baadhi ya safari utamuona na Try Again tofauti na ilivyokuwa lile jopo la viongozi.
Magori ameomba kupumzika masuala ya mpira ndani ya Simba, Nassoro na Mulamu wapo mbali na timu si kama awali kwahiyo mambo mengi ya timu yanafanyika chini ya Try Again ambaye hana maelewano mazuri na Barbara.
UTENDAJI WAKE
Huku nje, wapenzi na mashabiki wa Simba wengi wao walikuwa huwambii kitu kuhusu Barbara wakiamini ni kati ya viongozi wanaofanya kazi yao nzuri ndani ya klabu kwa muda wote.
Wakati mashabiki wakiamini hilo, ndani ya uongozi wengi walikuwa na mawazo tofauti wakiamini Barbara hawezi kufiti kwenye nafasi hiyo na ameshindwa kuwa msimamizi wa shughuli za klabu za kila siku.
Jambo hilo la kutokuaminika na kuonekana hafanyi kitu ndani ya Simba lilikuwa likimkera Barbara.
UVUMILIVU ULIMSHINDA
Awali, Barbara aliweza kuvumilia masuala magumu kama sakata lake na aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba wakati huo, Haji Manara ila huku mwishoni ameonekana kuwa mwenye unyonge na hata muda mwingine kulalamika kwenye mitandao ya kijamii japo kwa kufichaficha maneno
MSIKIE MWENYEWE
Alipotafutwa Barbara, akasema: “Siwezi kuongeza maneno mengine tofauti na yale ya kwenye taarifa yangu kwa sasa, ila tusubiri mwezi mmoja ufike ili nikabidhi ofisi nadhani baada ya hapo labda naweza kuongeza zaidi.”