Home Habari za michezo TRY AGAIN: TUKIMTAKA TENA BARBARA TUTAMTAFUTA ….KWA SASA TUNA MAMBO MENGI…

TRY AGAIN: TUKIMTAKA TENA BARBARA TUTAMTAFUTA ….KWA SASA TUNA MAMBO MENGI…

Baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Barbara Gonzalez kujiuzulu nafasi yake, hatimaye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Salim Abdallah maarufu ‘Try Again’ ambaye yupo nchini Uswisi amesema wameupokea uamuzi uliochukuliwa na haraka wanatafuta mrithi wake.

Barbara ambaye amehudumu katika nafasi hiyo tangu Septemba 2020 alitangaza kujiuzulu nafasi yake ndani ya klabu hiyo juzi kuanzia Januari mwakani.

Baada ya kutoa taarifa hiyo kumekuwa na mitazamo tofauti kutoka kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo kuhusiana na suala hilo ambapo kila mmoja amekuwa na mtazamo wake, lakini Try Again ambaye yupo barani Ulaya kwa sasa na ameonekana kupiga picha na mabosi wa Fifa, amesema ni uamuzi wa bosi huyo.

Akizungumza Try Again alisema wanaheshimu uamuzi uliochukuliwa na Barbara na wanampongeza kwa kile alichofanya ndani ya timu hiyo kabla ya kuamua kujiengua hivyo Bodi ya Wakurugenzi itakutana haraka kuanza mchakato wa kutafuta mrithi wa nafasi hiyo.

“Tumekubaliana na uamuzi wake. Kwa sasa nipo safarini nikirudi tutaitisha kikao haraka sana na viongozi wenzangu wa juu kwa ajili ya mchakato wa kumtafuta mrithi wa nafasi hiyo. Kilichotokea kinatakiwa kupokewa kwa utulivu ili kisiweze kuvuruga mwelekeo wetu,” alisema.

“Tunamtakia kila la heri kwenye majukumu yake mapya. Tutakapokuwa tunahitaji mambo muhimu kutoka kwake hatutasita kuomba ushirikiano wake. Kwa sasa tunahitaji utulivu na kuipambania timu kwenda kwenye mchakato mzuri wa uchaguzi na usajili kipindi hiki cha dirisha dogo.”

Try Again alisema utulivu utasaidia kuifanya timu hiyo kufikia malengo waliyojipangia mwanzo wa msimu na kama viongozi watafanya kile kinachotakiwa ili kuiweka timu kwenye wakati mzuri.

Mbali na Try Again, mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage alisema timu hiyo imempoteza kiongozi bora na imara kuwahi kutokea katika eneo hilo ambaye aliweza kuingia haraka kwenye mfumo.

“Ni pigo kwa Simba wameondokewa na kiongozi mzuri ambaye ameweza kufanya mambo makubwa ndani ya muda mchache alioingia ndani ya timu hiyo, japo naamini kuna baadhi ya viongozi walishindwa kuendana naye kwenye majukumu ndio wamemuondoa,” alisema Rage.

“Kwa makubwa aliyoyafanya ndani ya Simba namuona mbali sana kama sio kwenye timu, basi kwenye mashirikisho makubwa kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), hii ni kutokana na ubora aliouonyesha ndani ya Simba.”

Hata hivyo, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Simba, Swedi Nkwabi alisema kujiuzulu kwa Barbara siyo jambo baya kwani ni uamuzi wake na Simba haiwezi kuyumba kwa sababu ya mtu mmoja.

“Kwangu mimi naona hata ukiangalia uchaguzi wake wa kumpata kuwa CEO haukuwa sahihi kwani hakuwa mtu mwenye uzoefu wa kutosha wa kuwa CEO wa Simba

“Muhimu kwa sasa tupate mtu mwenye uzoefu wa kututoa hapa tulipo na anayeweza kuishauri Bodi.

“Bodi inatakiwa kuleta mtu (CEO), ambaye anaweza kufanya kazi kwa uhuru asiingiliwe na atakayetengeneza mifumo madhubuti ya uendeshaji wa klabu kisasa kama tunavyotaka, “alisema Mkwabi.

Ukiachana na Mkwabi pia aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Mzee Hamis Kilomoni, alisema lazima kutakuwa na sababu iliyopelekea Barbara kuamua kukaa pembeni na si tu kuamua mwenyewe.

“Labda kuna kitu tu kilichomfanya aondoke,haiwezekani aondoke tu hivi hivi na kujiweka pembeni, lazima kutakuwa na sababu, “alisema Kilomoni.

SOMA NA HII  LILE DILI LA STRAIKA MCAMEROON KUTUA SIMBA 'UPDATE' HII HAPA....MBRAZILI ALETA KOCHA MSAIDIZI MPYA..