Home Habari za michezo YACOUBA KUANZA KUUWASHA UPYA YANGA SC…NABI AMPA MAPINDUZI CUP….

YACOUBA KUANZA KUUWASHA UPYA YANGA SC…NABI AMPA MAPINDUZI CUP….

Yanga imesaliwa na mechi tatu tu kabla ya kufunga mwaka 2023, kisha kusafiri kwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, huku Kocha Nasreddine Nabi akiamua kumpa kazi mshambuliaji Yacouba Songne kabla ya kumrejesha rasmi kikosini.

Yacouba aliyekuwa kinara wa mabao wa Yanga misimu miwili iliyopita, aliumia katikati ya msimu uliopita na kushindwa kuitumikia timu hiyo, ila alibakishwa nchini licha ya kutosajiliwa msimu huu na yupo kwenye mipango ya benchi la ufundi la timu hiyo.

Nyota huyo kutoka Burkina Faso, aliumia Novemba 2, 2021 akicheza kwa dakika 31 kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya kufanyiwa upasuaji na sasa amepona na amekuwa akijifua na timu hiyo wakati akitengenezewa mazingira ya kusajili kupitia dirisha dogo.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema Kocha Nabi ameamua kumpa muda wa wiki mbili Yacouba kwa ajili ya kupima kiwango chake kupitia michuano ya Mapinduzi inayoanza Januari 1-13.

“Jina lake ni miongoni mwa mastaa watakaoenda kushiriki mashindano ya Mapinduzi, ni pendekezo la Kocha Nasreddine Nabi na ni matumaini yetu mara baada ya kuonyesha uwezo wake kwenye mashindano hayo ndio itakuwa tiketi yake ya kurudishwa kikosini,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Uwepo wake ndani ya Yanga tangu anaugulia na kufanyiwa matibabu akiwa chini ya uangalizi wa uongozi ni wazi uongozi bado unamhitaji na alikuwa akifanya mazoezi na timu uwezo wa kucheza mashabiki na wanachama watatoa tathimini kwa sababu dirisha hili ni ngumu kupata wachezaji.”

Mwanaspoti lilimtafuta nyota huyo ili kuzungumzia maendeleo yake na kushiriki mashindano hayo na alisema ni suala la muda yeye kuonekana uwanjani, hivyo mashabiki na wadau wasubirie ili kuona kiwango chake baada ya kumkosa kwa msimu mmoja na nusu.

“Nipo pamoja na timu na mashindano hayo kwa kuwa yanashirikisha hadi wachezaji walio nje ya mkataba natumaini ni fursa yangu kuyatumikia kama nitapata nafasi hiyo, siwezi kuzungumza mengi kwani nafasi hiyo ni ya viongozi mimi kazi yangu ni kucheza,” alisema Yacouba aliyemaliza na mabao manane katika msimu wa 2020-2021 akiwa ndiye kinara wa Yanga msimu huo.

Yacouba alisema kwa sasa yuko sawa na anasubiri maamuzi ya mabosi wa klabu yake juu ya kurejea kundini baada ya kuondolewa katika usajili wa msimu huu.

SOMA NA HII  BASHIRI NA MERIDIANBET MECHI ZA EURO LEO....ODDS ZA USHINDI ZIKO HAPA...