Home Azam FC BAADA YA KUITUNGUA TENA YANGA SC…SOPU NAYE ALIAMSHA KWA DIARRA…

BAADA YA KUITUNGUA TENA YANGA SC…SOPU NAYE ALIAMSHA KWA DIARRA…

Habari za Michezo

Licha ya chama lake la Azam FC, kupoteza mechi ya ligi juzi kwa kuchapwa mabao 3-2 na Yanga SC, kiungo mshambuliaji wa Azam, Abdul Seleman ‘Sopu’ alikuwa moja ya wachezaji waliofanya vizuri kwenye mchezo huo akifunga mabao yote mawili ya timu yake na kuwa gumzo mtaani.

Mabao hayo mawili yamemfanya Sopu kuifunga Yanga SC mabao matano katika mechi mbili alizokutana nao, na kuwa moto wa kuotea mbali kwa kipa wa Wanajangwani, Djigui Diarra.

Sopu aliifunga Yanga mabao matatu, ‘Hat trick’ akiwa na Coastal Union kwenye mechi ya Kombe la TFF (ASFC) iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 na Wanajangwani kubeba kombe kwa mikwaju ya penalti 4-1, jambo lililowavuta mabosi wa Azam FC na kumsajili haraka kwa mkwanja mrefu.

Akiwa na Azam FC alipatwa na majeraha ambayo yalimuweka nje kwa muda lakini katika mechi ya mzunguko wa kwanza Wanalambalamba hao walipokutana na Yanga SC, alitoa pasi ya bao ‘Asisti’ kwa Malickou Ndoye na mechi kumalizika kwa sare ya 2-2, hivyo kwa ujumla amehusika kwenye mabao sita dhidi ya Yanga SC kwenye mechi tatu.

Sopu amesema kazi yake ni kufunga na anaweza kumfunga kipa na timu yeyote kama akipata nafasi hivyo kuifunga Yanga mabao matano katika mechi mbili ni jambo la kawaida kwake.

“Kazi yangu ni kufunga, sio kwa Yanga tu bali kila mechi ninayocheza natamani kufunga kila nikipata nafasi na limekuwa jambo la kawaida kwangu,” alisema Sopu na kuongeza;

“Haikuwa ngumu kwangu kuifunga Yanga kwani nimeshawahi kufanya hivyo, ni timu yenye mabeki na kipa mzuri lakini najua nichezaje ili nifunge na ndio kama ilivyotokea.”

Mabao hayo mawili ya Sopu ndiyo ya kwanza kwa staa huyo wa zamani wa Simba na Ndanda kwa msimu huu kwenye ligi tangu amejiunga na Azam aliyosaini kuitumikia mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu.

AZAM YAJITOA…

Kwa upande mwingine, Azam wamesema kuwa dalili zote zinaonyesha kuwa hawawezi tena kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kutokana na gepu la pointi waliloachwa baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Yanga juzi.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Yanga ilibaki kileleni na pointi 47, na kuiacha Azam yenye pointi 37, katika nafasi ya tatu huku Simba kabla ya mechi ya jana dhidi ya KMC ikikaa nafasi ya pili na pointi 38, jambo lililomuumiza kichwa kaimu kocha Mkuu wa matajiri hao wa Chamazi Kali Ongala na kukiri kuachana na mbio za ubingwa.

Kally alisema mawazo yake yamejitoa kwenye mbio za ubingwa kutokana na kuzidiwa pointi nyingi (10) na Yanga inayoongoza ligi jambo ambalo hadi kuzifikia, Wanajangwani wanatakiwa kupoteza mechi tatu na kutoa sare moja huku Wanalambalamba hao wakihitaji kushinda zote mpango ambao umeonekana kuwa mgumu.

“Suala la ubingwa limekuwa gumu kwetu baada ya kupoteza mechi na Yanga, tayari anatuzidi alama 10 ambazo ni ngumu kuzifikia nadhani kwa sasa tunaenda kujipanga zaidi kuhakikisha tunamaliza kwenye nafasi za juu,” alisema Kally.

Aidha kocha huyo alizungumzia kukwama kwa kikosi chake kushindwa kuwa na muendelezo bora ikiwemo kupoteza mechi na Yanga ambayo walimiliki mpira kwa asilimia kubwa zaidi.

“Tuna timu nzuri lakini tumekuwa tukifanya makosa madogo madogo ambayo yanatugharimu, kwa sasa hatupaswi kulaumiana bali kurudi kujipanga kuhakikisha tunafuta makosa hayo na kuifanya timu iwe bora na kucheza kwa umoja.”

Tangu imepanda Ligi Kuu mwaka 2008, Azam imebeba ubingwa wa ligi mara moja tu msimu wa 2013-2014.

SOMA NA HII  SIMBA WAAPA...WATAJUA HAWAJUI...BARBARA AANIKA MBINU NZITO..MWANASPOTI....