Home Habari za michezo INJINIA HERSI: REKODI YA UNBETEAN SIO UBINGWA KWA YANGA…KAZI BADO MBICHI…

INJINIA HERSI: REKODI YA UNBETEAN SIO UBINGWA KWA YANGA…KAZI BADO MBICHI…

Kikosi cha Yanga tayari kipo Dar es Salaam, kikitokea Mbeya ilikotibuliwa rekodi yao ya kutopoteza mechi (unbeaten) katika Ligi Kuu Bara baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Ihefu, lakini vigogo wa klabu hiyo walifanya kikao kizito na mastaa kuamsha ari mpya.

Kikao hicho kilichotumia dakika 35 kikiitishwa na Rais wa klabu hiyo Injinia Hersi Said na kuwaambia mastaa wa timu hiyo kuwa, wasiumizwe na kutibuliwa rekodi yao ya kutofungwa ikicheza mechi 49 mfululizo kabla ya 50 juzi kukwama, kwa vile hakuna bingwa wa kubeba kombe la rekodi ya unbeaten.

Yanga ilikuwa haijaonja kipigo tangu Aprili 25 mwaka jana ilipofungwa na Azam na kucheza mechi hizo mfululizo ikishinda na kutoka sare tu, kabla ya Ihefu kutibua sherehe za Yanga kutimiza mechi 50 kwa mabao ya Mzimbabwe Never Tigere na Lenny Kissu.

Injiani Hersi katika kikao hicho kilichofanyika jijini Mbeya, aliwapongeza wachezaji kwa rekodi hiyo akawataka makocha na wachezaji kuinua vichwa juu na kuanza kufikiria kutopoteza pointi nyingine zitakazowapa ubingwa wa pili mfululizo katika ligi hiyo inayomalizia duru la kwanza.

“Nimewaambia hakuna taji kwa rekodi ya kutofungwa, ila kuna makombe ya ubingwa wa ligi, hii rekodi itawapa heshima kama makocha, wachezaji na klabu inawashukuru kwa hilo na wao watabaki katika kumbukumbu kubwa isiyofutika baadaye kwa walichokifanya,” alisema Hersi na kuongeza;

“Baada ya kupoteza, nimewaambia wajiulize kipi kimewakwamisha na kuangusha pointi tatu, hilo ndio kubwa, sasa ni wakati wa kuinua vichwa juu na kurudi na nguvu uwanjani kuhakikisha tunarudi katika ushindi ili tutetee mataji, hatukutengeneza timu hii kwa ajili ya kutofungwa tunataka makombe.”

Rais huyo aliyechaguliwa hivi karibuni akimpokea Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla, aliongeza kwa kusema; “Nafurahi kuona wachezaji wamesimama imara pamoja na benchi la ufundi, haya matokeo yatatupa nguvu na ari mpya katika kutambua kuna ugumu tutakutana nao na kitu bora ni kwamba tunatakiwa tusirudie makosa ya kudondosha pointi kama hivi ili tuweke malengo yetu sawa.”

Wakati Hersi akiyasema hayo, benchi la ufundi chini ya kocha Nasreddine Nabi wamerudi kitaalamu kuangalia jinsi ya kuwarudishia wachezaji wao utimamu wa mwili wakigundua kwamba kuna mchoko umewashika wachezaji wao.

Benchi hilo limekaa chini na madaktari wa timu hiyo kuanza kutafuta njia sahihi itakayowaondolea uchovu huo wakigundua kwamba wachezaji wao wamekumbana na hali hiyo kufuatia kucheza mechi nyingi mfululizo.

“Tumecheza mechi 7 katika mwezi mmoja, utaona jinsi ratiba yetu ilivyo ngumu, hatukuona mchezaji ambaye alikuwa amecheza kwa ubora wake, tunarudi kuangalia upya jinsi tutakachoweza kufanya kuwaondolea mchoko wachezaji wetu,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tunahitaji kufanya tathimini hiyo haraka, tumelazimika kuwapa mapumziko ya siku chache wachezaji wakati huu tukitafuta njia zipi za kufanya kuondoa kuwaathiri wachezaji kwa kuwa ratiba kama hiyo ngumu itaendelea.

“Tutarudi uwanjani tukiwa bora zaidi, tunajua mashabiki wetu wameshtuka lakini huu ni mchezo wa soka na haya ni sehemu ya matokeo yake, hakuna aliyefurahia kuangusha pointi hizi tunajua matokeo haya yataturudishia umakini zaidi.”

Yanga inajiandaa kuvaana na Tanzania Prisons katika mechi itakayopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA WAARABU...NABI ATAMBA YANGA KUUTIKISA M'BUYU...