Home Habari za michezo TETESI ZA USAJILI: SIMBA WAAMUA LIWALO NA LIWE KWA NTIBAZONKIZA…WAULIZIA MKATABA WAKE...

TETESI ZA USAJILI: SIMBA WAAMUA LIWALO NA LIWE KWA NTIBAZONKIZA…WAULIZIA MKATABA WAKE NA GEITA ULIVYO…

Simba inaendelea kupiga hesabu za kusuka kikosi kimyakimya na kufanya mambo mapema na sasa mabosi wa klabu hiyo wameonyesha hawatanii kwa kumganda kiungo fundi mmoja wa Geita Gold wakiulizia mkataba wake ili kuupitia kabla ya kuamua cha kufanya kupitia dirisha dogo.

Kiungo huyo mkongwe alieyagandwa na Simba ni Saido Ntibazonkiza wakiutaka mkataba wake na Geita Gold mezani kabla ya kumbeba katika dirisha linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 16 na kufungwa Januari 15 mwakani ili kuimarisha kikosi kwa mechi za ndani na zile za kimataifa.

Simba inataka nguvu ya Saido katika kikosi hicho wakiona zile asisti zake zinawafaa katika safu yao ya ushambuliaji na sasa wamekutana na wawakilishi wa staa huyo wa Kirundi wakitaka kujua aina ya mkataba alionao pale Geita Gold.

Saido bado ana mkataba na Geita waliomsajili msimu huu baada ya mkongwe huyo kuachwa na Yanga na mabosi wa wekundu hao wanajua wanatakiwa kumalizana na klabu hiyo kisha mchezaji huyo ili kupata saini yake.

“Wanataka kwanza kujua aina ya mkataba wake na Geita ni jinsi gani wataweza kumalizana na hiyo klabu kabla ya kumalizana na mchezaji, wanahofia klabu yake isije kufanya mambo magumu baadaye,” alisema mmoja wa wawakilishi wa mchezaji huyo.

Katika mazungumzo ya awali, Saido alishawapa Simba anachotaka ili amwage wino katika klabu hiyo akiwaachia wao wajipange kisha wamfuate.

Endapo Simba itamnasa Saido wataongeza kitu katika safu yao ushambuliaji kutokana na uzoefu wa staa huyo aliyewahi kukipiga Ligi Kuu ya Ufaransa.

Jana Geita kupitia Kaimu Mtendaji Mkuu, Liberatus Pastory ameliambia Mwanaspoti ingawa bado Simba hawajawafuata kuzngumzia uhamisho huo, lakini hawana shida kama watafikia makubaliano ya kufidia mkataba wake.

“Haya ni maisha ya wachezaji hatuwezi kuwazuia kama tutaona maslahi ya klabu yamefikiwa na kuheshimika, tuko tayari kumuuza kama Simba tukiafikiana nao, ingawa sasa bado hatujawaona kuja kwetu, zaidi ya kusikia tu kama ambavyo ninyi mnatuuliza,” alisema Pastory.

Geita ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 21 huku Saido akiifungia mabao matatu na kuasisti mara nne akizidi kuipa nguvu timu hiyo iliyoshika nafasi ya nne msimu uliopita na kukata tiketi ya michuano ya CAF iking’olewa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika na Hilal Alsahil ya Sudan.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA JWANENG....AHMED ALLY AMTAJA ATAKAYEWAHUJUMU SIMBA...