Home Habari za michezo HUU HAPA MUONEKANO MPYA WA UWANJA WA AMAAN ZANZIBAR

HUU HAPA MUONEKANO MPYA WA UWANJA WA AMAAN ZANZIBAR

MASHABIKI wa soka visiwani Zanzibar kwa sasa akili na hamu yao kuu ni kushuhudia michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 inayotarajiwa kuanza rasmi Alhamisi ijayo.

Michuano ya msimu huu imenogeshwa kwa kuongeza idadi ya timu shiriki kutoka tisa za msimu uliopita hadi 12, huku timu nne kati ya hizo zikiwa ni za kigeni na nane zikitoka Tanzania Bara na visiwani hapa.

Timu za nje zilizoalikwa ni Vital’O ya Burundi, APR ya Rwanda, URA ya Uganda na Bandari Kenya, huku Bara ikiwakilishwa na vigogo Simba, Yanga, Azam na wanafainali ya msimu uliopita, Singida Fountain Gate, wakati za visiwani ni watetezi Mlandege, Jamhuri, Chipukizi na KVZ.

Achana na ongezeko la timu, lakini utamu zaidi ni kuwa, michuano ya msimu huu inachezwa tena kwenye Uwanja wa Amaan, lakini ukiwa na muonekano mpya kabisa baada ya kukarabatiwa na kuonekana wa kisasa zaidi, huku mashabiki watakaohudhuria kwa sasa hawatalowa na mvua au kuchomwa na miali ya jua kutokana na kuzibwa juu kwa maeneo yote ya majukwaa tofauti na ilivyokuwa zamani.

SH 13 BILIONI

Ukarabati huo wa awamu ya tatu baada ya ule wa mwaka 2010 umeelezwa umefanywa na Serikali wa Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na umegharimu zaidi ya Sh 13 Bilioni na unatarajiwa kuzinduliwa wiki ijayo baada ya kukamilika kwake.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajabu aliliambia Mwanaspoti kuwa, fedha za ukarabati zilizotumika kwenye uwanja huo zimetoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na hakuna aina ufadhili wowote kutoka nje ya nchi wala shirikisho lolote la soka lililowapiga tafu.

Fatma anasema SMZ inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi iliona kuna haja kuboreshwa kwa sekta ya michezo visiwani hapa na ndio maana akawa tayari kutoa fedha hizo na ukarabati umefanywa na Kampuni ya Orkun Group kutoka Uturuki.

Anasema ukarabati huo uliodumu kwa miezi sita umefanywa kwenye maeneo mbali mbali ikiwamo kuboreshwa na kufanywa upya kwa sehemu nyingine ili kuufanya uvutie zaidi, pia kukidhi matakwa ya michezo ya kimataifa.

Katibu huyo anasema eneo kubwa lililofanywa upya ni kuzungusha mapaa uwanja mzima, tofauti na awali paa lilikuwa eneo la moja pekee la jukwaa kuu tu la viongozi (VIP).

“Kwa sasa mashabiki hawatasumbuka tena mvua ikinyesha au wakati wa jua kutokana na uwanja mzima kuzungushiwa paa na pia kuwekwa viti vya kisasa,” anasema.

Anasema kukosekana kwa mapaa kuliufanya uwanja huo kuonekana wa kizamani na usiokuwa na hadhi ya kamataifa lakini kwa sasa jambo hilo halipo tena.

“Hivi sasa ni raha tupu uwanja nzima umeezekwa mapaa ya kisasa na yaliyo bora, naamini kwenye mashindano haya ya Kombe la Mapinduzi, uwanja utajitangaza zaidi kimataifa,” anasema.

ONGEZEKO IDADI YA MASHABIKI

Katibu huyo anaendelea kufafanua zaidi kwa kusema maeneo mengine yaliyofanyiwa ukarabati huo ni sehemu zote wanazokaa mashabiki kwa kuwekwa viti maalumu vya kisasa ambavyo awali havikuwapo kuwafanya wanaotazama mpira kuangalia mechi kwa raha.

“Kwa sasa mashabiki watakaa kwenye viti maalumu vyenye hadhi ya kimataifa, huku wakifurahika soka zuri kutoka kwa timu ambazo zitakuwa zikicheza kwenye uwanja huo,” anasema Fatma na kuongeza kuwa, kuwekwa kwa viti hivyo kumeongeza idadi ya watazamaji ambao kwa sasa uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuingiza watu 15,500 tofauti na awali ulikuwa unaingiza watazamaji 12,000 pekee.

TAA ZA KISASA

Anasema marekebisho hayo pia yalihusisha uwekaji wa taa mpya na za kisasa ambazo zitamulika vyema kwa mechi za usiku na pia kuweka mazingira yavutie zaidi na kuwa salama kwa wachezaji na watazamaji ndani na nje kwa muda wote.

Pia anasema uwanja umeweka mabango ya digitali (billboard) ya kisasa ambayo yanaufanya Amaan uwe na hadhi zaidi, kwani Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na hata Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limekuwa likiagiza viwanja kuwa na mabango ya matangazo ya aina hiyo kurahisisha wadhamini kutangazwa mechi zikiendelea.

Mabango ya aina hiyo yamewekwa kwenye viwanja viwili tu, Azam Complex, Chamazi na ule wa Benjamin Mkapa vilivyoboreshwa hivi karibuni.

ENEO LA KUCHEZEA

Pamoja na hayo alisema watalamu walioboresha uwanja huo, yaani kampuni ya Orkun Group, wamefanya pia kazi ya kusanifu eneo la kuchezewa mpira (pitch) kwa kuweka nyasi bandia za kisasa (grade one) na kutoa zile zilizokuwapo awali.

Maeneo mengine ni ukarabati na kuboreshwa kwa eneo lote la kubadilishia nguo wachezaji (dressing room) sambamba na vyoo vilivyowekwa vya kisasa zaidi tofauti na zamani, huku pia kukiwekwa mabafu ya kisasa ili kuwapa raha wachezaji mara baada ya mchezo.ifupi ni kwamba Uwanja wa Amaan uliojengwa rasmi mwaka 1970 kwa msaada ya serikali ya China kwa sasa umedamshi kinoma na kilichobaki ni kuzinduliwa ikiwa ni mwanzo wa maandalizi ya Miaka 60 ya Mapinduzi.

SOMA NA HII  MWENYE NAMBA AMERUDI, AISUBIRI TIMU KAMBINI, MASTAA WAPEWA MAAGIZO