Home Habari za michezo TUONGEE KIMPIRA…HI ISHU YA BARBARA KUJIUZULU SIO KUBWA KIVILEE..ILA BADO KUNA TATIZO...

TUONGEE KIMPIRA…HI ISHU YA BARBARA KUJIUZULU SIO KUBWA KIVILEE..ILA BADO KUNA TATIZO SIMBA..

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, Jumamosi alitangaza kujiuzulu nafasi yake kwa sababu ambazo hakuziweka bayana, ingawa kulishaanza kuzabaa maneno kuhusu mzozo ndani ya uongozi wa klabu hiyo kongwe.

Barbara hana muda mrefu tangu ateuliwe kushika wadhifa huo katika mazingira ambayo yaliibua maswali kuhusu mchakato wa kumpata baada ya aliyeajiriwa kushika wadhifa huo, Senzo Mazingisa kutoka Afrika Kusini, naye kujiondoa kabla ya kuibukia Yanga siku chache baadaye.

Senzo naye hakuwahi kueleza sababu za kuondoka kwake, zaidi ya kutoa taarifa kuwa wameachana na Simba kwa amani na maelewano. Na kweli hakujazuka maneno yoyote baina ya pande hizo mbili.

Lakini kuondoka kwa Barbara kumetanguliwa na uvumi kwamba alikuwa haelewani na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na hata uvumi mwingine kueleza kuwa alikuwa hawaheshimu wajumbe wa bodi na kwamba mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ndiye amekuwa akimkingia kifua.

Imeelezwa kuwa Salim amekuwa hakubaliani na uendeshaji wake wa klabu na kwamba huenda madai kuwa Barbara hamheshimu mwenyekiti wake yamechochea kuharakisha kuondoka kwake.

Kuondoka kwa Barbara pia kumetanguliwa na habari za wachezaji kutolipwa bonasi waliyoahidiwa kupewa, iwapo wangeingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, na madai kuwa kuna malimbikizo ya malipo ya wachezaji.

Binafsi nimekuwa nikifuatilia mwenendo wa mabadiliko ya Simba na Yanga na mara kadhaa nimeeleza kuwa hakuna mabadiliko ya kimsingi ya kimuundo na kiuendeshaji zaidi ya sura na majina ya nafasi na vyeo kubadilika, lakini uendeshaji umebakia kuwa uleule wa mwaka 47.

Lakini, kama kawaida yetu, kasoro zinatakiwa zisemwe pale mambo yanapokwenda mrama au ziwe zimefika kooni ndio zinaanza kujadiliwa.

Wakati Barbara anaajiriwa kuwa CEO wa Simba, kuliibuka maswali kwamba iweje mtu ambaye alikuwa anaongoza taasisi ya mwekezaji ndio apewe nafasi hiyo ambayo kwake bodi inatakiwa ifanye kazi ya ziada kabla ya kumpata mtu sahihi?

Waziri wa zamani, Hamis Kigwangalla alihoji sana suala hilo, lakini alijibiwa kwa kashfa kwamba swali lake limetokana na hasira za kunyimwa mkopo wa pikipiki. Pamoja na Kigwangalla kutochoka kuhoji, alipuuzwa kwa kuwa Simba ilikuwa inafanya vizuri, hasa kimataifa.

Lakini kulikuwa na kasoro. Mmoja wa wanahisa wa kampuni inayoendesha klabu hiyo hatakiwi kuwa na sauti kubwa kwa mtendaji mkuu. Amepangiwa nafasi zake kwenye bodi ya wakurugenzi ili ziwe sauti yake katika kufanya maamuzi makuu ya klabu.

Na kwa sababu hisa zake hazizidi asilimia 50, basi hatakiwi kuwa na nguvu kubwa zaidi ya wawakilishi wa wanahisa wengi ambao nao wamo ndani ya bodi ya wakurugenzi. Na kwa maana hiyo, wanahisa wengi ndio wanatakiwa washike nafasi ya mwenyekiti kama kweli klabu imefanya mabadiliko na kuingia katika mfumo huo wa umilkiki wa klabu na uendeshaji.

Kuteuliwa kwa mtu ambaye alikuwa karibu na mmoja wa wanahisa wa klabu hiyo ndio kuliibua shaka kwamba amewekwa pale ili kulinda taarifa muhimu za kifedha zinazomhusu Dewji. Na kubwa ikawa Shilingi 20 Bilioni ambazo Mo alitakiwa ziingize kwa ajili ya kununua hizo asilimia 49.

Hadi leo hizo fedha zimekuwa ndio swali kubwa iwapo unazungumzia mabadiliko ya Simba. Na huenda ndio zilisababisha baadhi ya wakurugenzi au hata mwenyekiti wa zamani, Sued Nkwabi kuachia ngazi.

Zimelipwa au hazijalipwa ni swali ambalo hakuna aliyelitolea jibu la uhakika zaidi ya lile tukio la kukabidhi hundi ya mfano lililoibua maswali zaidi. Lakini wakati kukiwa na maneno yote hayo, Dewji alijitokeza akaeleza jinsi alivyotumia fedha zake kusajili na ikaonekana ametumia zaidi ya shilingi bilioni 20. Kejeli na maswali yakaibuka tena.

Kwa kawaida, klabu au taasisi inapoamua kuruhusu watu kununua hisa, huwa inakusudia kuongeza mtaji wake ili iwe na uwezo mkubwa zaidi kifedha katika uendeshaji wake.

Ungetegemea kuona kwamba baada ya hizo fedha kuingia, viongozi wale watendaji wangeacha kuzungumzia habari kwamba ‘Mo amejitolea fedha nyingi kusajili’ kana kwamba anafanya hisani kumbe ameingia kama mwekezaji aliyetumbukiza fedha nyingi akijua klabu itasimama yenyewe huku yeye akisubiri gawio baada ya klabu kuingiza fedha nyingi.

Lakini taarifa zimekuwa ni hizo. Mara Mo amegoma kutoa fedha za usajili. Anagomaje wakati masuala ya kuiidhinisha bajeti kwa ajili ya uendeshaji klabu yapo mikononi mwa bodi ya wakurugenzi? Mara Barbara amekataa kutoa fedha kwa ajili ya kumsajili mchezaji fulani; anagomaje wakati bodi ilishaidhinisha bajeti kwa ajili ya usajili?

Kujekuwa na maswali mengi ambayo binafsi nilitafsiri kuwa hakuna mabadiliko yale tunayoaminishwa kwamba yamefanyika kiasi cha baadhi ya waandishi na wachambuzi kuyapamba na hata kupendekeza kwamba Barbara ndiye CEO bora nchini.

Ndio, Roman Abramovic alikuwa anahusika katika baadhi ya usajili, lakini ni pale anapokuwa na mapenzi binafsi na anapofanya ziada ya nje ya bajeti iliyotengwa katika usajili. Stan Kroenke wa Arsenal aliwadhibiti katika kutenga fedha nyingi, lakini alikuwa na sababu; wakati huo Arsenal ilikuwa bado inalipa deni la uwanja.

Ipo mifano mingi inayoonyesha wamiliki wakiingilia usajili, lakini ni pale wanapokuwa na umiliki unaozidi asilimia 50 ndipo wanakuwa na maamuzi makubwa kama Abramovic, Kroenke au familia ya Glazer.

Lakini umiliki unapokuwa mdogo, ni lazima mambo yan edeshwe kwa uwazi na kwa taratibu zilizowekwa ili kila mtu asiwe na shaka kwa mwenzake.

Hata mamlaka ya Barbara yanaonekana yalikuwa na kiwango fulani na si makubwa kama CEO anavyotakiwa kuwa na pengine ndio maana kila alipotaka kuonyesha kuwa shughuli za utekelezaji ziko chini yake na hatakiwi kuingiliwa, ndipo alipoonekana ana kiburi.

Kwa kawaida CEO ni tofauti na katibu mkuu wa taasisi ambayo ina kamati ya utendaji na hivyo mwenyekiti kuwa mtendaji. Kwenye taasisi ambayo ina CEO, kazi ya bodi ya wakurugenzi hao ni kupanga na kuelekeza. Inapomaliza kikao cha kufanya hayo, kazi yake huwa ni kusubiri ripoti ya utekelezaji na sio kuingilia katikati na kufanya uamuzi mwingine. Kufanya hivyo ni kumuingilia CEO.

Lakini watu wa mpira wanaweza kumuacha CEO afanye mambo yake na wao wasubiri hadi miezi mitatu wakati bodi inapokutana ili wahoji? Hilo haliwezekani!

Lakini kama tunataka mabadiliko ya kweli katika klabu zetu ni lazima hilo liwezekane.

Hali ni kama hiyo upande wa pili. Namuona Hersi Said ni kama vile ndiye mtendaji mkuu badala ya yule Mzimbabwe. Bado hajakubali kukaa mbali na utendaji wa shughuli za kila siku na kwa sababu Yanga inaendelea kuwa na matokeo mazuri, hayo hnayawezi kuzungumzwa sasa.

Lakini dalili kwamba mambo hayaendi vizuri zinajionyesha katika mambo machache ambayo kwa sasa hayawezi kukuzwa hadi tatizo halisi lijitokeze. Wimbi la kuondoka kwa watendaji limekuwa kubwa na kama vikao vinafanyika kila mara kuridhia kuondoka kwao au kuondolewa, maana yake kamati ya utendaji inakutana kila mara badala ya menejimenti.

Kwa kifupi tunahitaji mabadiliko ya kweli kufikia huko wenzetu waliko. Kubahatishabahatisha na kusubiri matokeo ya timu ndiyo yatulinde, hakuna muda mrefu. Mabadiliko ya kweli yanahitajika na mabadiliko hayo hayawezi kutuhakikishia mwendo wa amani kwa sababu yana milima na mabonde.

SOMA NA HII  HUKUMU YA AVEVA YAAHIRISHWA,YAPANGIWA SIKU NYINGINE