Yanga haitaki masihara kabisa, baada ya kuona timu nyingi Afrika zinawamendea mastaa wake wakali imeanza kuwapa mikataba mipya ili kihakikisha hawang’oki Jangwani na kuendelea kupeperusha bendera ya kijani na njano na raundi hii wametua kwa beki kisiki, Dickson Job.
Tayari Yanga imefanikiwa kumbakiza kipa wake Mmali, Djiggui Diarra na kiungo Mganda Kharid Aucho ambao mikataba yao mipya itatamatika mwaka 2024, na baada ya hao wamegeukia kwa Job na kumwaga mpunga wa maana kumbakiza.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinaeleza baada ya Diarra na Aucho, Mabosi wa chama hilo wamechagua kuhakikisha wanampa mkataba mpya Job kutokana na sababu kadhaa lakini mbili ndio za msingi zaidi.
Mosi ni beki huyo kuwindwa kwa watani wao wa Jadi, Simba sambamba na Yanga pia pia timu nyingine kutoka uarabuni jambo Yanga inaamini ikichelewa anaweza kuondoka kikosini hapo kwani mkataba wake aliosaini akitokea mtibwa Sugar unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Tayari Simba na Azam zilikuwa zimeonyesha nia ya kutaka huduma ya Job na mazungumzo ya chinichini baina ya timu hizo na uwakilishi wa beki huyo yalikuwa yameanza kwa usiri sana jambo ambalo Yanga imestukia na kumaliza kazi.
Pili ni kiwango alichokionyesha akiwa ni beki aliyecheza mechyi nyingi zaidi za Yanga kwa msimu huu tena kwa ubora na kuwa chaguo la kwanza la kocha Nassredine Nabi kwenye eneo la ulinzi na mara nyingi amekuwa akibadilishiwa wakucheza naye kati ya Bakari Mwamnyeto, Yanick Bangala na Ibrahim Bacca.
Chanzo cheti kimethibitisha kuwa, Job kusaini Mkataba mpya utakaombakiza klabuni hapo hadi mwaka 2024 kama ilivyo kwa Aucho na Diarra na amevuta mkwanja mrefu kutokana na dili hilo.
Katika mkataba huo mpya, Job atalipwa karibu mara mbili ya mshahara aliokuwa anaupata mwanzo na sasa atakuwa anapata kati ya 7 milioni hadi 10 kwa mwezi ukijumlisha na marupurupu mengine.
Aidha chanzo chetu kimefafanua, katika mkataba mpya wa Job kutakuwa na kipengele kitakacho mruhusu kuondoka kwa makubaliano maalumu kama atapata ofa nzuri zaidi lakini pia kipo cha kuongeza mkataba zaidio Yanga kwa makubaliano maalumu.
“Amesaini muda mfupi kwa kuwa anaamini safari yake ya Soka haitaishia Yanga tu, anaweza kupata ofa nyingine bora zaidi huko mbeleni ndio maana amefanya hivyo ili ikitokea iwe rahisi kwake kuondoka Jangwani,” kilieleza Chanzo chetu.
Kwa upande wa Rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said alisema timu yao imejipanga kuwaboreshea maslahi na kuhakikisha mastaa wake wote muhimu inawabakiza kikosini kwa namna yeyote ile.
“Yanga ni timu kubwa, tunataka kuendelea kujiimarisha kwa kuwatengenezea mazingira mazuri wachezaji wetu na kuwabakisha hapa ili tuendelee kutengeneza kikosi imara zaidi,” alisema Hersi.
Ikumbukwe Job alijiunga na Yanga Januari 2021 akitokea Mtibwa Sugar kwa mkataba wa miaka miwili ambao unatamatika mwishoni mwa msimu huu.