Meneja wa Habari na Mawasilino wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, amefichua sehemu ya mazungumzo kati Rais wa Heshima na Mwekezaji Mwenza wa Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’, alipotinga Kambini huko Dubai juzi Jumanne (Januari 10).
Mo Dewji alizungumza na Wachezaji pamoja na Benchi la Ufundi linaloongozwa na Kocha kutoka nchini Brazil Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’.
Ahmed Ally amefichua sehemu ya Mazungumzo hayo kwa kunukuu kauli ya Mo Dewji, kwa kuandika katika kurasa zake za Mitandao ya Kijamii.
Sehemu ya nukuu ya Mo Dewji iliyotumiwa na Ahmed Ally katika andiko lake, imethibitisha mapenzi ya mwekezaji huyo na Klabu ya Simba SC, huku akisisitiza hajaondoka na hataondoka kwenye klabu hiyo ambayo amekuwa akikiri kuipenda tangu akiwa mtoto mdogo.
Ahmed Ally ameandika: “Juzi kwenye kikao cha Rais wa heshima @moodewji na kikosi aliwaambia wachezaji kuwa duniani yeye anapenda timu moja tuu Simba Sports.”