Home Habari za michezo SIMBA WAFANYA KUFRU KWA SAWADOGO…MSHAHARA WAKE TU NI MIL 336….UKWELI HUU HAPA…

SIMBA WAFANYA KUFRU KWA SAWADOGO…MSHAHARA WAKE TU NI MIL 336….UKWELI HUU HAPA…

Habari za Simba

Umeisika hii, unaambiwa kiungo mpya wa Simba raia wa Burkina Faso, Hamed Ismael Sawadogo, mshahara wake ndani ya kikosi hicho unaweza kuwalipa wachezaji watatu aina ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga anayelipwa shilingi milioni nne kwa mwezi na chenji ikabaki.

Imeripotiwa kwamba, Sawadogo ameigharimu Simba shilingi milioni 300 za Kitanzania katika fedha ya usajili, huku mshahara wake kwa mwezi ukitajwa kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 14, ambazo ni sawa na shilingi milioni 336 kwa mwaka miaka miwili.

Sawadogo ambaye timu yake ya mwisho kabla ya Simba alikuwa akiicheza Difaa El Jadida ya Morocco, kupitia mshahara wa milioni 14 kwa mwezi, ndani ya mwaka mmoja ataingiza shilingi milioni 168, huku kwa wiki ikiwa ni shilingi milioni 3.5, kwa siku shilingi 466,666.7 na kwa saa shilingi 19,444.4.

Chanzo chetu kutoka Simba kimesema  kwamba, usajili wa Swadogo umeigharimu Klabu hiyo kiasi cha Shilingi milioni 300, kutokana na kuwaniwa na baadhi ya klabu kubwa Barani Afrika, jambo ambalo liliwafanya watoe kiasi hicho ili wasimkose mwamba huyo.

“Tumesajili wachezaji wawili kwa gharama kubwa sana kutokana na mahitaji yetu hasa kuelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo utaona mchezaji mmoja pekee kama Sawadogo tumetumia kama milioni 300 za usajili.

“Ila ukiangalia hata mshahara wake, analamba zaidi ya milioni 14 kila mwezi, fedha ambayo ukilinganisha na kiasi anacholipwa Fei Toto pale Yanga utaona kuna uwezo wa kulipa wachezaji watatu wa aina yake na chenji ikabaki ya kumlipa mchezaji kama Clement Mzize,” kilisema chanzo hicho.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Mimi sijui ukweli juu ya mshahara na kiasi alichopewa mchezaji huyo hadi anafika hapa, ila ninachoweza kusema Sawadogo ni miongoni mwa wachezaji wenye daraja kubwa sana Afrika, hivyo hata thamani yake kwa vyovyote haiwezi kuwa ya kawaida.”

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA JUMAMOSI DHIDI YA UGANDA...TAIFA STARS WAAPA KUIWAFANYIA UMAFIA 'THE CRANES'...MIKAKATI IKO HIVI...