Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU….SAKATA LA FEI TOTO LIMEONYESHA TASWIRA HALISI YA YANGA SC…

UKWELI MCHUNGU….SAKATA LA FEI TOTO LIMEONYESHA TASWIRA HALISI YA YANGA SC…

Fei toto atimka Yanga SC

Kuna vitu vingine kwenye soka letu vinachekesha sana. Ni kama haya mambo yanayoendelea pale Yanga SC. Ni mambo ya ajabu kuliko ajabu yenyewe.

Wiki iliyopita ilimalizika kwa sakata la Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuomba kuvunja mkataba na Yanga SC. Ulikuwa mshtuko mkubwa. Fei Toto anaombaje kuondoka Yanga SC mwenyewe? Ni jambo ambalo limeacha maswali mengi kuliko majibu. Pia limeacha maswali juu ya namna Yanga inavyoendeshwa.

Kiungo huyu alilipa na fedha anazotakiwa kulipa akitaka kuondoka. Akaweka Sh112 milioni kwenye akaunti ya klabu. Akaenda kwao Zanzibar na kujituliza.

Kwanini Feisal amefikia hatua hiyo? Ni wazi kuwa kuna shida katika uendeshaji wa Yanga SC. Sote tunakubaliana kuwa Fei Toto ndiye mchezaji bora zaidi mzawa. Je alikuwa anapata anachostahili Yanga SC?

Fei anaanza kila mechi. Anacheza vizuri kila mechi. Anawafurahisha Wananchi kila wiki. Kwanini alikuwa halipwi kulingana na ubora wake? Inafikirisha.

Kwanini viongozi wa Yanga SC walikuwa hawaoni umuhimu wa Fei? Ni swali ambalo hawawezi kulijibu hadi naingia kaburini. Ubaya zaidi ni namna Yanga SC wamekuwa wakifanya mambo yao kupambana na sakata la Fei. Mambo yanakwenda zaidi kwa mihemko na uswahili. Kwanza, walianza kwa kusema Fei hana haki ya kufanya alichofanya kwani hayupo sawa kisheria. Wakasema wamemrudishia fedha zake. Ikaonekana kama ni jambo lenye weledi ndani yake.

Nini kimetokea baada ya hapo? Mambo yakawa tofauti. Kwa mujibu wa mkataba wa Fei inaonekana ana haki ya kufanya hivyo. Ni Yanga SC wenyewe waliweka kifungu cha kumruhusu kuvunja mkataba muda wowote akiweza kulipa fedha zilizoainishwa.

Kwa akili ya viongozi wa Yanga SC waliona Fei hataweza kulipa Sh112 milioni. Hivyo walikuwa na uhakika atakaa hadi mkataba utakapomalizika. Kujisahau kulikoje. Baada ya kugundua kuwa kisheria wako kwenye kona ngumu Yanga SC wameamua kutumia wiki nzima kufanya vitisho na propaganda za ajabu kweli.

Wakaanza kwa kudai Fei amerudi kambini. Watu wakadai picha yake akiwa kambini. Wakapita hivi na kukimbia kama Tuisila Kisinda. Wakawa hawana majibu.

Wakasambaza propaganda nyingine kuwa amekuja lakini kocha amemwambia aondoke kwanza. Ataharibu hali ya kambi. Inachekesha sana.

Baada ya hapo wakataka kulizima sakata kwa njia nyingine. Wanajua Fei anahusishwa kwenda Azam, hivyo nao wakatuma barua ya kutaka kuwanunua Kipre Jr na James Akaminko. Ni vituko kweli.

Ni kama kuitisha Azam kuwa kama mnamchukua Fei na wao watachukua wachezaji wao muhimu.

Wakataka iwe mjadala kwenye mitandao ya kijamii. Wakavujisha barua waliyotuma Azam kwa waandishi ili iweze kusambaa. Imesaidia nini? Hakuna.

Baada ya kuona mambo ni magumu wakatuma wazee wao wakafanye mkutano na wanahabari. Wakaanza kuitisha Azam na kwamba watasusia bidhaa zao kama watamchukua Fei. Ushamba ulioje.

Wewe hebu jiulize kiwango cha Fei pale Yanga SC alikuwa ni mchezaji wa kuwekewa kipengele cha kuvunja mkataba wake kwa Sh112 milioni? Inashangaza sana.

Hizo fedha kwa sasa hazitoshi hata kununua kiungo wa kawaida kama Mzamiru Yassin. Ni fedha ndogo mno kwenye soka la kisasa.

Sasa makosa waliyofanya Yanga SC kuandika mkataba wa kiwango cha chini, leo wanataka kuyamaliza kwa propaganda? Ni uswahili wa kiwango cha juu sana.

Viongozi wa Yanga lazima wakubali kuwa kwenye Mkataba wa Fei walipuyanga. Hakuna namna wanaweza kuchomoka.

Wasiwasi wangu ni kuwa huenda mikataba ya kina Fiston Mayele, Djigui Diara, Aziz Ki na wengineo pengine ina upungufu kama huo. Na badala ya kuanza kupambana na udhaifu huo wameishia kutuma wazee kuitisha Azam FC. Ni mambo ya kizamani.

Kama Yanga ingekuwa inaendeshwa kwa weledi, Fei angekuwa ndiye mchezaji mzawa anayelipwa zaidi. Kila mtu analiona hilo. Kwanini Yanga hawakuliona? Kuna tatizo mahala.

SOMA NA HII  KISA KIPIGO KUTOKA COASTAL ....KASEJA AVUNJA UKIMYA...AFUNGUKA NAMNA ALIVYOCHEZA CHINI YA KIWANGO...