Home Habari za michezo WAGOMBEA SIMBA WALIA NA KATIBA KUMBEBA MWEKEZAJI….WAAPA MABADILIKO…

WAGOMBEA SIMBA WALIA NA KATIBA KUMBEBA MWEKEZAJI….WAAPA MABADILIKO…

Habari za Simba

Klabu ya Simba ipo kwenye mchakato wa kufanya uchaguzi mkuu huku kampeni kwa wagombea wa uchaguzi huo zikifunguliwa rasmi juzi Jumatano lakini imeonekana kwamba kasi ya watani zao Yanga ndiyo inayowaumiza wanachama wa Simba.

Katika ufunguzi wa kampeni hizo zilizofanyika Magomeni jijini Dar es Salaam wagombea wote waliojitokeza kwenye uzinduzi huo walionekana kuumizwa na mafanikio ya Yanga na kuahidi kwamba endapo watachaguliwa basi jambo la kwanza ni kuhakikisha wanapigania kupata mafanikio hayo.

Miongoni mwa mafanikio ambayo Yanga wanaonekana kuongezekana kwa kasi ni idadi ya wanachama na mashabiki pamoja na kutofungwa na watani zao hao kwa kipindi kirefu.

Miongoni mwa wagombea walioanza kunadi sera zao ni mgombea nafasi ya Mwenyekiti, Moses Kaluwa ambaye anagombea nafasi hiyo na Murtaza Mangungu anayetetea kiti chake. Mangungu alichaguliwa kwenye uchaguzi mdogo baada ya Swedy Mkwabi aliyekuwa Mwenyekiti kujiuzulu.

Kaluwa ambaye ni Wakili aliwaambia wanachama waliohudhuria mkutano huo kuwa; “Endapo nitachaguliwa nitahakikisha tunapata wanachama na mashabiki wengi kupitia Kamati itakayokuwepo, Simba ina watu wengi lakini hawajaingia kwenye mfumo huo kwani hawajafikiwa.

“Ni lazima tuwe na utamaduni wa kutembelea matawi kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Mkoa ili kila mmoja atambue kwamba Simba ni mali yake, pia nitatambua uwepo wa makundi ya wachezaji wa zamani, wazee na akina mama, nao washirikishwe,” alisema na kuongeza;

“Uongozi wa kujifungia ndani sio uongozi sahihi, tutatoka nje kuzungumza na wanachama wetu kuhakikisha narudisha umoja ambao kwa sasa unaonekana kulegalega ili nikiondoa niache alama ndani ya Simba.”

Kuhusu mabadiliko ya Katiba ambayo awali aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo Hassan Dalali alisema inapaswa kufanyiwa marekebisho kwani ina mapungufu mengi, Kaluwa alionekana kuunga mkono.

“Katiba ni ya wanachama, kama mabadiliko yanatakiwa kufanyiwa basi wanachama wataamua na yatafanyika kwa njia zinazostahili,” alisema Kaluwa.

Suala la kushindwa kuwafunga Yanga wagombea walisema ifike mahali wakubaliane kwa pamoja kuhakikisha wanaanza kuifunga Yanga mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu hapo Machi mwaka huu.

“Inaumiza kuona kwamba tunashindwa kuifunga Yanga, kuna nini hapo kati, sasa hawa wagombea wasema wazi nini watafanya kuhakikisha tunaifunga Yanga,” alisema Dalali

Mgombea nafasi ya ujumbe, Dk Seif Ramadhan alisema; “Yanga wametuzidi pointi, ila tunaamini wana pointi tatu zetu ambazo tutazipata mechi ijayo, tutapambana kwa vitendo kuhakikisha tunawafunga, tutashinda na tutachukua ubingwa, tuna timu nzuri kwanini watani watunyanyase, sasa hatutakubali.”

Pendo Aidan, ambaye anagombea ujumbe wakiwa wawili wanawake pamoja na Asha Baraka alisema; “Nitafanyakazi kwa uadilifu mkubwa na kuisaidia klabu kuleta maendeleo na hili suala la mtani tutaungana pamoja kuhakikisha ushindi unapatikana.”

Kampeni hizo zimepangwa kufanyika kwa siku 12 ambapo uchaguzi mkuu utafanywa Januari 29 mwaka huu.

SOMA NA HII  SIKU CHACHE BAADA YA KUTIMULIWA SIMBA...PABLO KAANIKA KILA KITU WAZI...KATAJA WACHEZAJI WALIOMCHOMESHA....