Home Habari za michezo BAADA YA KUONA JAHAZI LINAZAMA….SIMBA ‘WAMPIGIA SIMU FASTA’ MATOLA…MWENYEWE KAFUNGUKA HAYA…

BAADA YA KUONA JAHAZI LINAZAMA….SIMBA ‘WAMPIGIA SIMU FASTA’ MATOLA…MWENYEWE KAFUNGUKA HAYA…

Habari za Simba

Tayari mabosi wa Simba wamemuita aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Suleimani Matola mezani kwa ajili ya mazungumzo, huku kukiwa na maswali mengi kuhusu kinachokwenda kujadiliwa.

Simba imeshindwa kufanya vizuri kwenye Klabu Bingwa Afrika baada ya kupoteza michezo miwili ya mwanzoni ya hatua ya makundi kwa kuchapwa na Horoya bao 1-0 na Raja Casablanca 3-0.

Matola alikuwa msaidizi wa Simba kwenye kipindi cha mafanikio makubwa ya timu hiyo, baada ya kufika robo fainali mara mbili kwenye Klabu Bingwa Afrika na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho lakini akiwa pia ametwaa makombe kadhaa ya Ligi Kuu Bara akiwa na makocha tofauti.

Hata hivyo, kwa sasa kocha huyo anasomea Leseni A ya CAF, lakini kwa muda mwingine ameonekana akiwa jijini Dar es Salaam, wakati timu hiyo ikiwa kwenye uwanja wa mazoezi na kwenye mechi na inaelezwa kuwa baada ya mchezo wa juzi mabosi wa timu hiyo walimuita kwa ajili ya kikao cha dharura.

Chanzo cha ndani kutoka ndani ya Simba kinasema kuwa , Matola atakwenda kwenye makao makuu ya klabu hiyo mchana kuonana na mwenyekiti wa timu hiyo, Salim Abadalah ‘Try Again’ kwa ajili ya mazungumzo huku ikielezwa kuwa anaweza kujumuishwa kwenye safari ya timu hiyo itakayokwenda nchini Uganda kuvaana na Vipers katika mchezo wa tatu wa makundi.

“Ninafahamu kuwa Matola anatakiwa kukutana na mabosi wa timu , sijui wanachokwenda kujadili lakini nafikiri wameona kuwa anatakiwa kuwa kwenye timu, unajua kwa hapa yeye ana uzoefu zaidi kwa kuwa alikuwa na makocha wote waliopata mafanikio kuanzia robo fainali mbili za Klabu Bingwa na hata moja ile ya Kombe la Shirikisho.

“Inafahamika kuwa bado yupo masomoni na ilielezwa amebadilishiwa majukumu na kuwa mkurugenzi wa soka la vijana ili apate muda mwingi wa kusoma, lakini mara nyingi ameonekana mjini na alinukuliwa akisema kuwa anasoma lugha na kompyuta hapa jijini Dar, labda uongozi unataka kumuongeza kwenye benchi, sijui ingawa umuhimu wake unaonekana pale kwa sasa kwa kuwa ana uzoefu wa kutosha,” kilisema chanzo hicho cha ndani cha Simba.

Alipotafutwa Matola ili kufahammu ukweli wa taarifa hii ambapo simu yake iliita muda mrefu na alipopokea alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa .

“Siwezi kuzungumza lolote kwa sasa, nimekuheshimu sana kupokea simu yako unajua sasa nipo darasani, kuhusu suala hilo nafikiri  siwezi kukujibu lolote,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Toto African, Supersport ya Afrika Kusini na Simba.

SOMA NA HII  BAADA YA KUBANJULIWA 3-O JANA....JEMEDARI SAID KAIBUKA NA 'DONGO' HILI KWA YANGA...