Home Habari za michezo SIMBA vs AZAM…NI ZAIDI YA MECHI..REKODI HIZI MPYA HUENDA ZIKAWEKWA AU KUVUNJWA…

SIMBA vs AZAM…NI ZAIDI YA MECHI..REKODI HIZI MPYA HUENDA ZIKAWEKWA AU KUVUNJWA…

Simba vs Azam

Kuna madeni mawili ambayo mojawapo linaweza kulipwa au kuendelezwa katika Ligi Kuu wakati Simba itakapovaana na Azam FC leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Deni la kwanza ni Simba kulipa kisasi cha kuchapwa bao 1-0 na Azam FC katika mchezo wa kwanza baina yao uliochezwa uwanjani hapo, Oktoba 27, mwaka jana na iwapo watapokea kichapo au sare maana yake wamekubali kuwa vibonde wa Azam msimu huu.

Lakini deni la pili ni Azam FC ambalo ni utumwa wa muda mrefu dhidi ya Simba kutokana na kupoteza idadi kubwa ya mechi timu hizo zikutanapo.

Licha ya kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba ina historia ya utemi dhidi ya Azam FC na kuthibitisha hilo, katika mechi 10 zilizopita imeibuka na ushindi mara tano, Azam mara moja na sare nne.

Ni nadra mchezo baina ya timu hizo mbili kumalizika bila bao kufungwa na takwimu zinaonyesha mabao 23 yamefungwa katika mechi 10 ikiwa ni wastani wa mabao 2.3 kwa kila mechi.

Wakati wenyeji Simba wakiingia wakiwa na mwendelezo bora wa matokeo katika mechi za ligi ambapo wameshinda tano mfululizo zilizopita, Azam FC imekuwa ikisuasua ambapo katika mechi tano zilizopita imeshinda mara mbili na kupoteza tatu.

Kila upande unalazimika kupambana kwa machozi, jasho na damu ili upate ushindi ambao utaufanya ujiweke katika nafasi nzuri ya kutimiza malengo.

Ushindi kwa Simba utaifanya ifikishe pointi 56 na kuzidi kujichimbia katika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu pungufu ya vinara Yanga, hivyo kuendelea kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Kwa Azam FC ushindi utaisogeza hadi nafasi ya tatu kwa pointi 45, moja zaidi ya Singida Big Stars.

Kocha msaidizi wa Azam, John Matambala alisema watawakosa wachezaji wawili.

β€œTumejiandaa vizuri na tulikuwa na wiki mbili za maandalizi ya mchezo wa kesho (leo). Katika mechi hii tutawakosa Bruce Kangwa na Idrissa Mbombo ambao wanatumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kupata kadi tatu za njano,” alisema Matambala.

Simba ina furaha ya urejeo wa kiungo Sadio Kanoute.

β€œJana nimezungumza na wachezaji wangu nikawaambia wasahau yaliyopita na Simba ina mwendelezo mzuri wa matokeo mazuri kwenye ligi. Hii ni fursa nzuri kuendeleza ushindi kwenye ligi,” alisema kocha wa timu hiyo, Robertinho.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA NYUMA GAZETI LA CHAMPIONI IJUMAA