Home Habari za michezo A-Z JINSI YANGA WALIVYOIFANYIZIA PRISONS JANA…MZIZE AZIDI KUMPAGAWISHA NABI…

A-Z JINSI YANGA WALIVYOIFANYIZIA PRISONS JANA…MZIZE AZIDI KUMPAGAWISHA NABI…

Habari za Yanga SC

Kikosi cha Yanga bado kipo njia Kuu ikitaka kutetea mataji yake yote mawili yaliyosalia baada ya jana kuichapa Prisons ya Mbeya kwa mabao 4-1 mchezo wa hatua ya 16 Bora ya Kombe la Azam Shirikisho.

Ushindi huo unaifanya Yanga kutinga hatua ya Robo Fainali ambapo mabao ya timu zote yakifungwa kipindi cha pili Cha mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex,Chamazi.

Dakika 45 za kwanza licha ya Yanga kutawala vizuri mchezo lakini walishindwa kupata bao wakipoteza umakini kwenye kumalizia nafasi walizotengeneza huku wageni wao wakionyesha kucheza soka la kujilinda kwa utulivu zaidi.

Prisons katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza walijikuta wakipungua na kucheza pungufu baada ya beki wao wa kushoto Ibrahim Abraham kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu na kufanya timu zote kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Kipindi cha pili Prisons walirejea kwa mabadiliko wakimuingiza nahodha na beki wao mkongwe Jumanne Elifadhili akichukua nafasi ya Oscar Paul huku wenyeji wao nao wakimtoa winga Jesus Moloko akiingia mshambuliaji Clement Mzize.

Mabadiliko hayo yaliifanya Yanga kurudi na kasi na dakika ya 52 beki na nahodha wao Bakari Mwamnyeto aliifungia timu yake bao la kuongoza akimalizia kwa shuti jepesi mpira uliogongwa na beki wa Prisons kufuatia krosi ya winga Twisila Kisinda.

Prisons walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 61 likifungwa na Elifadhili akimalizia kona ya beki Doto Shaban.

Yanga waliamka na kupata bao la pili dakika ya 70 mfungaji akiwa Mzize akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Prisons Yona Amos kufuatia shuti la Stephanie Azizi KI.

Yanga wakicheza huku mfadhili wao Ghalib Said Mohamed’GSM’ akiwa uwanjani sambamba na Rais wa klabu hiyo Injinia Hersi Said walipata bao la tatu dakika ya 84 kwa bao lililofungwa na Azizi KI kwa njia ya penalti iliyotolewa dakika ya 82 baada ya kipa Amos kumchezea vibaya Mzize aliyekuwa anataka kufunga.

Mzize tena alifunga bao lake la pili dakika ya 88 akipokea pasi ya Djuma Shaban anakimbia na kuwatoka mabeki na kuingia nao ndani ya eneo la hatari na kufunga bao la kistaa kwa shuti la mguu wa kushoto likihitimisha ushindi huo wa timu yake.

Hata hivyo kinda huyo alijikuta alishindwa kufunga Hat trick yake ya pili kwenye Mashindano hayo akikosa penalti dakika ya 90 na kuinyima timu yake bao la tano

Mpaka mwisho wa mchezo Yanga ilifanikiwa kuondoka na ushindi huo wa mabao 4-1 wakiendelea kulinda heshima yao ya kutetea taji hilo.

SOMA NA HII  JEZI MPYA SIMBA NI KESHO....BEI YATAJWA MAPEMAAA...