Wakati Taifa Stars ikiwa kwenye maandalizi ya mwisho huko Misri kwa ajili ya mchezo wa leo, Ijumaa wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda, nyota wa kikosi hicho wameapa kufanya kweli kwenye mchezo huo.
Taifa Stars ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi F ikiwa na pointi moja nyuma ya Niger yenye pointi mbili na Algeria ambao wanaongoza wakiwa na pointi sita, Uganda ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huu, wanaburuza mkia wakiwa hawana pointi.
Kulingana na hali ya kundi hilo, mshambuliaji wa kikosi hicho, Simon Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Saudi Arabia, alisema wanapaswa kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo ili kuweka hai matumaini yao ya kwenda Ivory Coast.
Msuva anaamini Taifa Stars inawachezaji wenye uwezo wa kushindana na aina ya wapinzani ambao wapo nao kundi moja kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Morali naona ipo juu, kila mchezaji anaonekana kuwa tayari kutoa alichonacho kwa ajili ya mchezo, mwalimu amekuwa akitufanya tujisikie raha kwenye programu zake mbalimbali za mazoezi, naiona nafasi ya kufanya vizuri dhidi ya Uganda,” alisema.
Upande wake nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta alisema Uganda wamekuwa wapinzani wagumu ambao wamekuwa wakiwasumbua kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki lakini kama wachezaji wapo tayari kukabiliana nao maana mechi hizi mbili
we lucru Const zilizopo mbele yao zimebeba hatma ya Tanzania kwenda Ivory Coast.
“Lazima tukubali kuwa Uganda wamekuwa wakitusumbua lakini hilo haliwezi kutukwamisha kufanikisha kile ambacho tumepanga kufanya ila hata sisi nao hatupo nyuma maana mara ya mwisho tulicheza nao mchezo wa kirafiki Libya na tuliwafunga (1-0),” alisema.
Kuhusu mbinu za kocha mpya, Adel Amrouche kwenye kikosi hicho, Samatta alisema, “Amekuwa muwazi kwa kueleza namna gani anataka kuona timu ikicheza hivyo ni jukumu lao wachezaji kuhakikisha wanafanyia kazi ili kufikia malengo kwa pamoja.”