Kibu Denis, kiungo mshambuliaji wa Simba, ameingia kwenye kesi mpya na kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira kwa kutakiwa aongeze umakini zaidi ili awe bora ndani ya uwanja.
Kibu ni chaguo la kwanza la Oliveira raia wa Brazil akiwa ni miongoni mwa nyota watano wazawa walioanza kikosi cha kwanza kilichoibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya, wikiendi iliyopita.
Akizungumza nasi, Oliveira alisema umakini mkubwa unahitajika kwa wachezaji wote ikiwa ni pamoja na Kibu kwenye eneo la kutengeneza nafasi na kumalizia.
“Kwa wachezaji wa Simba wote ikiwa ni Kibu, Clatous Chama, Sadio Kanoute bado kuna makosa ambayo yanafanyika kwenye eneo la umaliziaji, hili ni lazima tuliboreshe kwenye mashindano yote hasa Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ni ngumu.
“Nafasi kutengeneza ni kazi na kuzitumia ni kazi, hivyo wachezaji wanapaswa kuwa makini kwenye kila kitu ambacho tunafanya kuanzia washambuliaji mpaka mabeki, ni muhimu kushirikiana.
“Kwa yule ambaye anapata nafasi ya kufunga ni muhimu kufanya hivyo, ikitokea anaona mwenzake yupo kwenye nafasi bora zaidi ni muhimu akatoa pia kwa ajili ya ushindi wa timu,” alisema Oliveira.