Home Habari za michezo CHAMA AWACHAMBUA WACHAMBUZI WA SOKA…MFUNGAJI BORA WA MUDA WOTE CAF

CHAMA AWACHAMBUA WACHAMBUZI WA SOKA…MFUNGAJI BORA WA MUDA WOTE CAF

Habari za Simba SC

KILA shetani na mbuyu wake bwana na mbuyu wa Simba ni yule kiungo wao kutoka Zambia, Clatous Chota Chama ama ukipenda muite Triple C au Mwamba wa Lusaka.

Huyu anaweza kuwa mchezaji anayezungumzwa zaidi katika soka la Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni pengine kuzidi mchezaji yeyote.

Watu wa Simba wanamzungumza Chama na watu wa Yanga nao wanamzungumza. Akifanya vizuri anazungumzwa na hata asipofanya vizuri huwa anazungumzwa.

Baada ya ujio wa kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ndani ya Simba, Chama aliibua mijadala baada ya kuripotiwa kuwa kocha huyo hafurahishwi na staili ya uchezaji ya Chama na anahitaji nyota huyo kuipa timu yake vitu vingi ndani ya uwanja kama vile kukaba pindi wakipoteza mpira lakini pia kurudi nyuma kuzuia pindi wanaposhambuliwa.

Na suala la Robertinho ni kama lilimchongea mbele ya vinywa na maandiko ya baadhi ya wachambuzi wa soka nchini ambao wengine walifikia hadi kutoa kauli zilizombeza kupitiliza Clatous Chama utadhani walisahau vile ambavyo amekuwa akivifanya ndani ya Simba.

Chama alitajwa kama mchezaji mvivu, hawezi kukaba, hana faida kwa timu pale inapopoteza mpira na pia amekuwa akitamba dhidi ya timu ndogo huku wakijaribu kuhalalisha na maneno meengi ya Kiingereza kama pressing, workrate, pace, speed na commitment.

Walisahau huyu Chama ndiye alikuwa mchezaji muhimu na tegemeo wakati Simba inafika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018/2019 na msimu ule wa 2020/2021 akifunga mabao katika mechi muhimu za kuisogeza katika hatua inayofuata kama katika mechi dhidi ya Nkana FC na AS Vita Club au FC Platinum na Plateau United.

Baada ya kuchambuliwa kwa muda mrefu, Jumamosi iliyopita, Chama aliamua kuwachambua yeye wale wachambuzi waliokuwa wakimkejeli baada ya kufunga mabao matatu katika ushindi wa mabao 7-0 ambao Simba waliupata dhidi ya Horoya ambao uliwawezesha kutinga robo fainali huku pia akitoa asisti ya bao jingine moja.

Ni mabao matatu ambayo yamemfanya Chama kuwa mchezaji pekee kufunga ‘hat-trick’ katika mchezo mmoja wa hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu huu lakini pia yamemfanya aongoze kwa ufungaji akifikisha mabao manne.

Kana kwamba haitoshi yamemfanya afikishe mabao 19 ambayo yamemsogeza hadi nafasi ya tisa katika chati ya wafungaji bora wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Afrika lakini pia yamefanya aongoze orodha ya wachezaji waliohusika na idadi kubwa ya mabao katika hatua hiyo ya makundi.

Chama amewapa wachambuzi na watu waliombeza kazi ngumu ya kumjadili kwa sasa baada ya vitu vikubwa alivyovifanya dhidi ya Horoya.

Ugumu wanaoupata ni kwa sababu wakati alipokuwa hafanyi vizuri, walimaliza maneno kwa kumponda pasipo kukumbuka kuwa Chama ni mchezaji mwenye kipaji ambaye amekuwa akifanya vitu vikubwa pale ambapo wengine hawategemei.
Leo kawashika pabaya.

SOMA NA HII  YANGA YAHAMIA KWA STRAIKA WA ORLANDO PIRATES...JINA NI HILI