Home CAF KENNEDY MUSONDA MBABE…YANGA SC 2-0 US MONASTIR…DONDOO MUHIMU ZA MCHEZO HUU

KENNEDY MUSONDA MBABE…YANGA SC 2-0 US MONASTIR…DONDOO MUHIMU ZA MCHEZO HUU

Habari za Yanga

KENNEDY Musonda ameivusha Yanga kwenda robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia bao na asisti aliyotoa leo, Jumapili dhidi ya Monastir kwenye Uwanja wa Mkapa.

Kitendo cha Yanga kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho kitawafanya kuvuna dola 350,000 za CAF ambazo ni zaidi ya Sh 800milioni.

Musonda aliyesajiliwa wakati wa dirisha dogo, ameendelea kuthibitisha ubora wake akiwa na vijana hao wa Jangwani kwa kuhusika kwenye matokeo muhimu ambayo yanaifanya Yanga kuwa timu ya pili msimu huu kutoka Tanzania kutinga robo fainali ya michuano Kimataifa.

Mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Zambia alifanya Yanga kwenda mapunziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 alilofunga dakika ya 33 kabla ya kutoa asisti kwa Fiston Mayele dakika ya 59.

Hizi ni dondoo muhimu za mchezo huo wa kisasi kwa Yanga kwani ilikuwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-0 nchini Tunisia kwenye mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho, mafanikio makubwa waliyokuwa nayo ilikuwa ni kuishia hatua ya makundi. Historia imeandikwa.

Bao alilofunga Musonda ni la pili kwake msimu huu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika anashika nafasi ya pili kwa ufungaji Yanga, nyuma ya Mayele mwenye mabao matatu.

Kwa mara ya kwanza Ibrahim Bacca alipata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi na Monastir kutoka Tunisia huku akicheza sambamba na Bakari Mwamnyeto.

Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza Yanga ilipiga mashuti saba kwenye lango la Monastir huku manne kati ya hayo yakilenga lango.

Yanga iliotea mara tano kwenye mchezo huo huku Monastir ikiwa haijaotea hata mara moja huku upande wa kadi za njano zikitoka tano, Wananchi wakionyeshwa nne kati ya hizo.

Yanga itamaliza mchezo wake wa hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe ikiwa ugenini huku ikisaka uongozi wa kundi lake D kwa Sasa wapo pointi sawa na Monastir wakiwa na pointi 10.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuingiza timu mbili kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF, ikumbukwe kuwa Simba ilitinga Jana, Jumamosi baada ya kuishushia mvua ya mabao 7-0 Horoya ya Guinea.

SOMA NA HII  RAIS WA YANGA AANZA MIKAKATI, BAADA YA GAMONDI KUMPA LIST HII