Wakati mashabiki wakiiwazia Geita Gold kwamba ina mlima mkubwa mbele ya Yanga kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), wao wanasema matamanio yao ni kwenda nusu fainali na kuvuka kile walichokifanya msimu uliopita pamoja na kulipa kisasi kwa wana Jangwani hao.
Geita Gold itavaana na Yanga kwenye mchezo wa robo fainali ya Shirikisho utakaopigwa Aprili 8 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ambapo msimu uliopita timu hizo zilikutana kwenye hatua kama hiyo na Yanga ikasonga mbele kwa ushindi wa penalti kisha kutwaa ubingwa.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha msaidizi wa Geita Gold, Mathias Wandiba alisema wachezaji wao wote wako fiti na wanajiandaa kwa mchezo huo isipokuwa Juma Luizio ambaye anaendelea na matibabu na ameanza mazoezi mepesi.
Alisema benchi la ufundi na wachezaji wanatambua malengo yao ni kuvuka hatua waliyofikia msimu uliopita na kwenda nusu fainali hivyo wanajiandaa vizuri kuhakikisha Aprili 8 wanafanya vizuri dhidi ya Yanga.
“Ni mechi ambayo tunaamini kwamba tutakutana na timu iliyo bora ambayo imeimarika kila mechi ikizingatiwa siku chache zilizopita tulipoteza dhidi yao katika ligi lakini hiyo haijalishi kwa sababu tunakwenda kucheza mechi nyingine na mashindano mengine,” alisema Wandiba.
“Naamini vijana wameshajua ratiba ikoje pia benchi la ufundi matayarisho tunayoyafanya tunajua tunakwenda kucheza mechi mbili ambazo zinatofautiana na zina malengo tofauti, moja ni kwenda nusu fainali na nyingine ni kuongeza pointi ili kumaliza katika nafasi nzuri msimu huu.”
Kipa wa timu hiyo, Sebusebu Samson ‘Sebunho’ alisema:“Kipindi hiki timu imepata nafasi ya kurekebisha makosa ili ikirudi iwe imara zaidi japokuwa mechi zilizo mbele yetu ni ngumu lakini na sisi tumejiandaa vyema kufanya vizuri.”