Home Habari za Yanga WAKONGO WAMGOMBEA NABI….AITELEKEZA YANGA UWANJA WA NDEGE

WAKONGO WAMGOMBEA NABI….AITELEKEZA YANGA UWANJA WA NDEGE

NABI AONGEZEWA MKATABA YANGA...

KESHO kabla ya Mashetani Wekundu, Man United haijashuka Uwanja wa St James Park kuvaana na Newcastle United, mashabiki wa Yanga tayari watakuwa na matokeo ya pambano la timu hiyo dhidi ya TP Mazembe, lakini kuna jambo limeshtua wadau na kujikuta wakisema ‘Yanga hii kweli imepania’.

Juzi wakati ikiondoka jijini Dar es Salaam, msafara wa Yanga ulishtua kwa kuwa na vigogo kadhaa, lakini sura mbili zilishtua zaidi za Tarimba Abbas na bilionea wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed ‘GSM‘ kutokana kilichokuwa kikielezwa mtaani baada ya kutua kwa udhamini wa Haier klabuni hapo.

Tarimba ndiye kigogo wa Wadhamini Wakuu wa Yanga, SportPesa, hivyo ilidhaniwa kwa GSM kuruhusu kampuni ya Haier kuingia Yanga kuidhamini kwenye michuano ya CAF kungeibua ‘bifu‘ kubwa na pengine wawili hao kwa sasa wasingekuwa wakiiva chungu kimoja, lakini mambo sivyo.

Wawili hao kwa pamoja walikuwa sambamba na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na makamu wake, Arafat Haji mbali na Geofrey Mwambe ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Yanga na Mbunge kama ilivyo kwa Tarimba, mbali na Lameck Nyambaya Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) akiwa ndiye mkuu wa msafara wa timu hiyo jijini Lubumbashi.

Uwepo wa watu hao wazito kwenye msafara imeelezwa ni moja ya mkakati wa Yanga wa kuhakikisha kesho wanaimaliza Mazembe kama ilivyofanya katika mechi ya kwanza iliyopigwa Kwa Mkapa na Wakongo hao kulala mbao 3-1.

Kilichowapa raha zaidi mashabiki wa klabu hiyo ni hashtag iliyoambatana na video ya GSM ikieleza; ‘Tunasafiri kwenda Congo na Boss #GSM je tutarudi na nani?’, ambapo washangiaji walijibu swali hilo kuonyesha furaha yao na kumkubali bilionea huyo, aliyeisajilia timu mastaa walioibeba hadi sasa.

Taarifa kutoka kwenye msafara na katika kambi ya timu hiyo iliyopo Lubumbashi, zinasema kuwa, imeongeza mzuka kwa mastaa ambao inadaiwa pia wameahidiwa donge nono wakishinda kesho.

Licha ya hamasa hiyo, ikijumuishwa na mashabiki waliosafiri kwa mabasi kwenda kuamsha shangwe DR Congo, lakini uwepo wa baadhi ya wachezaji kutoka nchini humo wenye uzoefu dhidi ya Mazembe kama kina Fiston Mayele, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Joyce Lomalisa, Tuisila Kisinda na Djuma Shaban waliowahi kukipiga AS Vita inaelezwa ni faida nyingine ya kuibeba Yanga.

WAKONGO WAMGOMEA NABI
Katika hatua nyingine Yanga imetua jijini Lubumbashi kwa mchezo wa kesho lakini haitakuwa na kocha mkuu, Nasreddine Nabi.

Kocha huyo hakusafiri na timu kama ilivyoripotiwa na SOKA LA BONGO katika gazeti la jana na ishu kubwa ni pasi yake ya kusafiria kubakiza eneo moja tu la kupigwa muhuri, lakini juhudi za mabosi wa Yanga kupambana ili agongewe visa iligonga mwamba wakiambiwa pasi yake hiyo imejaa.
Hatua hiyo inamfanya Nabi rasmi hataweza kuingia nchini DR Congo na kwamba mchezo huo utasimamiwa na msaidizi wake Cedric Kaze.

Ingawa, hakuna bosi wa Yanga aliyeweza kufafanua hilo, lakini Nabi amelithibitishia SOKA LA BONGO kuwa hataweza kuungana na kikosi chake nchini humo kufuatia tatizo hilo.

“Nilitamani sana kwenda na timu yangu Lubumbashi,unajua malengo ya klabu yalikuwa sawa na yangu kwamba tushinde ili tuiongoze kundi lakini bado naamini tunaweza kufanikisha kwa kuwa kila kitu kitakuwa chini ya Kaze ni mtu sahihi tu kama mimi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Kwangu kuifunga mara mbili Mazembe ilikuwa ni kiu yangu kubwa lakini nawaamini wenzangu wataweza tu bila mimi,mambo mengi tulishayafanya hapa,hata viongozi wangu walipambana sana ili nisafiri lakini imeshindikana.

“Tunataka sana kuongoza hili kundi kwa faida ya hatua ya robo fainali nawaamini sana wachezaji ni wangu na wasaidizi wangu naamini watashirikiana vizuri na Cedric,Mimi nitakuwa nawasiliana nao pia kwa simu siku ya mchezo.

Nabi aliongeza tayari alishaanza taratibu za kupata pasi mpya ya kusafiria kutoka Ubelgiji anakoishi lakini muda haikutosha na kwamba Sasa anarudi tena nchini humo kuhakikisha anaipata haraka.

Alisema mabosi wa Yanga wamemtaka arudi Ubelgiji haraka kuhangaikia pasi hiyo kabla ya safari ijayo ya hatua ya robo fainali kutokana tayari Yanga imeshafuzu hatua hiyo.

“Narudi Ubelgiji leo (jana), unajua kule kupata pasi mpya unahitaji muda zaidi, nilishaanza hizo taratibu niliporudi kule wiki moja iliyopita lakini muda haukutosha, klabu imetaka nirudi haraka nihakikishe naipata nyingine.

SOMA NA HII  NABI AWANYOOSHEA KIDOLE MAYELE,MUSONDA...ROBERTINHO AHAMISHIA NGUVU YANGA, AZAM