MBEYA. KIKOSI cha Ihefu tayari kimetua Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa robo fainali Kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Simba utakaochezwa kesho ikiwa ni maadhimisho ya Karume Day.
Licha ya rekodi kutoibeba Ihefu mbele ya Simba, lakini benchi la ufundi limeapa kuvunja mwiko huo kwa kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo huo.
Ihefu haijawahi kupata ushindi mbele ya Simba tangu ilipopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2020/21 na kushuka kisha kurejea tena msimu huu.
Hata hivyo, msimu huu Ihefu ndio imeonekana kuwa bora zaidi kuliko kipindi chote kutokana na uimara wake baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na benchi la ufundi wakati wa dirisha dogo la Januari.
Kocha msaidizi wa kikosi hicho, Zubery Katwila alisema imekuwa fahali kubwa kwao kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo kila mmoja anasaka ubingwa kwa aina yake.
“Tumejiandaa vizuri kukabiliana na Simba ambayo ni timu bora lakini kikubwa ni maandalizi yetu yamekuwa bora kwa muda wote ambao ligi imesimama.
“Tunaamini mchezo utakuwa mzuri na wenye upinzani kwa kila upande kutokana na umuhimu wa mchezo huo unavyochukuliwa,” alisema Katwila.