Wakati viongozi wa Simba wakiwa katika mipango ya kuwaongezea mikataba baadhi ya wachezaji wao, siku za kipa chaguo la pili la timu hiyo, Beno Kakolanya, kuishi katika klabu hiyo zinahesabika, imefahamika.
Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema Kakolanya tayari ameshasaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Singida Big Stars na mabosi wa Simba walilazimika kumwondoa kwenye mipango ya mechi ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu iliyochezwa jana usiku.
Kakolanya alikuwa anaanza katika kikosi cha kwanza katika mechi zote za Kombe la FA lakini mapema wiki hii Simba ililazimika kusitisha ruhusa ya Aishi Manula ili arejee kukaa langoni katika mechi ya jana kwa ajili ya kukwepa hujuma.
Kakolanya amesajiliwa Singida Big Stars ili kuchukua nafasi iliyoachwa na Metacha Mnata ambaye amesajiliwa na Yanga.
Chanzo cha habari kilisema Simba ilikuwa tayari kumpa mkataba mpya wa thamani ya Sh. milioni 50 pamoja na mshahara Sh. milioni sita kwa mwezi, lakini Singida Big Stars iliingilia kati kumpa dau nono la Sh. milioni 100.
“Viongozi wa Simba wameshtukia dili baada ya kugundua kipa huyo tayari amesaini mkataba na Singida Big Stars, amewapa wakati mgumu,” kilisema chanzo chetu.
Naye Meneja wa Kakolanya, Suleiman Haroub, alisema kwa sasa anachofahamu mteja wake huyo bado anahitajika ndani ya timu hiyo na wako katika mazungumzo.
“Sina uhakika amesaini Singida Big Stars, licha ya kuwapo kwa taarifa za kutakiwa, lakini pia Simba walikuwa na mazungumzo naye ili kumwongezea mkataba mwingine,” alisema meneja huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wekundu wa Msimbazi.