Yanga kwa sasa iko kwenye ubora kila eneo ikiwa imeimarika zaidi na hata mastaa wao wapo moto, lakini hilo halijawapa presha wachezaji wa Kagera Sugar ambao wanajiandaa kushuka uwanjani leo katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu inayoelekea ukingoni.
Kagera itakuwa wageni wa Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa 1-0 katika mechi ya mkondo wa nyumbani iliyopigwa Novemba 13, mwaka jana kwa bao la Clement Mzize ambaye kocha Nasreddine Nabi amekuwa akimwamini na kumpa nafasi.
Licha ya kukiri ugumu wa pambano hilo, mastaa wa Kagera wamesema hawatishiwi na mziki wa Yanga na hata akipangwa mchezaji gani dhidi yao, bado watakomaa nao ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Kiungo wa Kagera, Ally Ramadhan ‘Kagawa’ aliyefunga bao moja juzi kwenye sare ya 2-2 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Dodoma Jiji, alisema viungo wote wa Yanga ni wazuri hivyo yeyote
atakayepangwa siku hiyo watakuwa naye makini bila kumpa nafasi ya kuwaadhibu.
Kagawa anayeongozwa kwa asisti kwa timu hiyo akitoa pasi tano, alisema maandalizi yao yanakwenda vyema na wanaingia kwenye mtanange huo kwa kuiheshimu Yanga na kuchukua tahadhari zote kwani wanatambua kosa dogo linaweza kuwamaliza.
“Mchezo uliopita tulipoteza lakini mwalimu aliona makosa yalikuwa wapi na kuyafanyia kazi kwa hiyo tumejiandaa vizuri kumalizia mechi tano zilizobaki ili kujihakikishia tunabaki kwenye ligi,” alisema Kagawa na kuongeza;
“Viungo wote wa Yanga ni wazuri kwahiyo yoyote atakaepata nafasi tutakuwa naye makini tu tunajua hatupo kwenye nafasi nzuri sana kwenye msimamo kwahiyo tutapambana kadri ya uwezo wetu tuweze kuondoka na pointi tatu.”
Afisa Habari wa Kagera Sugar, Hamis Mazanzala alisema kikosi cha timu hiyo kinaendelea vizuri na kinajiweka sawa na kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Yanga na kwamba waliondoka mjini Kagera tangu Jumatano na kuweka kambi ya muda mfupi jijini Dodoma ilipocheza mechi ya kujipima nguvu.
“Kila kitu kinaenda sawa na mipango yetu ni kuona tunapata ushindi ugenini, ndio maana tumeweka kambi ya muda jijini Dodoma na tumeanza safari ya kuja huko (Dar es Salaam),” alisema Mazanzala.
Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2010, timu hizo zimekutana mara 25, huku Yanga iking’ara kwa kushinda michezo 20 dhidi ya minne ya wapinzani wao na mechi moja tu ikiisha kwa sare, huku vijana hao wa Jangwani wakifunga jumla ya mabao 44 na kufungwa 17 ikivuna pointi 61 dhidi ya 13 za wana Nkurukumbi, ambayo ni moja ya timu chache ambazo tangu zipande Ligi Kuu hazijashuka.
SOMA NA HII PANGA LA AZAM FC KUPITA NA MASTAA HAWA CHAMAZI...MABOSI 'WAKUNJANA SHATI' KISA KANGWA...