Japokuwa ni suala la muda tu, Simba kumtangaza kiraka Yahya Mbegu anayekipiga Ihefu kwa sasa, klabu hiyo imeanza kutengeneza wachezaji wenye ofa nyingi uwanjani.
Tayari ndani ya kikosi hicho yupo Erasto Nyoni anayeweza kucheza beki wa kati, pembeni na kiungo mkabaji aliyocheza juzi dhidi ya Yanga akiziba nafasi ya Sadio Kanoute ambaye alikuwa anaumwa.
Kwenye mahojiano yake na gazeti la Mwanaspoti hivi karibuiĀ Mbegu, licha ya kwamba alikuwa na kigugumizi kujibu maswali ya kusaini Simba, alifunguka mambo mengi kuhusu karia yake ya soka.
Humwambii chochote kwenye kupambana kuhakikisha kazi yake anaifanya kwa usmati, jambo lililowafanya Simba kufukuzia saini yake tangu akiwa Polisi Tanzania, nyuma ya hilo kuna siri nzito.
Anafunguka “Nilifeli kidato cha nne, baadaye wazazi wakanilipia nikasome ufundi gereji, pamoja na hilo nilikuwa sijioni kama ni kazi inayoweza ikabadilisha maisha yangu, nikawaambia nahitaji kucheza soka.
“Haikuwa rahisi wazazi kunikubalia, ili kuwaonyesha kwamba sikuwa najaribu kazi hiyo, ndio maana sikubali kushindwa kwenye karia yangu, hata kama kuna ushindani kiasi gani nitapambana hadi nicheze.”
Anaulizwa ni kweli umesaini Simba SC? Kigugumizi kikaanzia hapo “Simba SC mbona hilo swali, siwezi kulizungumzia zaidi ya kukwambia kwa sasa nipo Ihefu, hilo ni swali linaloweza kujibiwa na viongozi wa klabu hiyo;
“Endapo wakija na kutoa ofa ya kutaka kuwatumikia mimi ni mchezaji lolote linaweza kutokea kila mchezaji hapa Tanzania ana ndoto ya kucheza kwenye timu kubwa Simba SC na Yanga.”
CHAMA, SAIDO, MOLOKO BALAA
Mabeki wengi hawapendi wachezaji wenye kasi kubwa kutokana na kutokutaka kutolewa jasho kwa kutumia nguvu kubwa kuwakaba hayo amethibitisha pia Mbegu ambaye amewataja mastaa watatu wanaompa shida akikutana nao.
“Kila mchezaji ninayekutana naye kwenye timu pinzani ni bora na ndio maana benchi la ufundi limeamua kumpa nafasi ya kucheza hivyo kwa asilimia kubwa nimekuwa nikipata changamoto ya ushindani na kukutana na wachezaji wengi bora kwenye nafasi ya ushambuliaji na winga;
“Lakini nikiambiwa niwataje wachezaji watatu wasumbufu siwezi kusita kumtaja Clatous Chama (Simba) ni moja ya mchezaji ambaye anakera kiwanjani kutokana na uwezo wake, Said Ntibazonkiza na Jesus Moloko ni wachezaji ambao nikijua tuna mechi nao nafanya mazoezi ya ziada.” anasema Mbegu.
Anasema ni wachezaji ambao wanajua nini wanakifanya uwanjani kuwakaba anatakiwa kutumia akili na sio nguvu huku akitaja sifa ya kila mmoja Moloko ni mtu wa kasi sana, Saido anatrumia akili na nguvu na Chama amekiri kuwa ni mchezaji ambaye anaufanya mpira kuwa mchezo mwepesi.
KUNA OKAYO HALAFU LOMALISA
Ni nadra sana wachezaji kukubali uwezo wa wachezaji ambao wanacheza wote nafasi moja lakini kwa upande wa Mbegu amekuwa muwazi huku akitoa sifa kwa mastaa wanaocheza nafasi anayocheza.
“Kuna wachezaji wengi wanaocheza beki namba tatu na wanafanya vizuri kwenye ligi kwa sasa lakini ukiniambia nikutajie wawili kwangu ni Deusdedith Okoyo ambaye (Geita Gold) na Joyce Lomalisa (Yanga) ni miongoni mwa wachezaji bora wanaocheza nawasi yangu;
“Kwasababu ni wachezaji ambao wanakuofa vitu vingi uwanjani wanajua kukaba na wanatengeneza mashambulizi wana pumzi ya kupanda haraka na kushuka ni wachezaji wachache wanaocheza nafasi hiyo wanaweza kufanya hivyo.” anasema Mbegu.
SIRI JEZI NAMBA TANO
Jezi namba tano imekuwa maarufu kutokana na kuvaliwa na mkongwe Kelvin Yondani ambaye anakipiga Geita Gold na imekuwa maarufu zaidi huku chipukizi wengi wakiivaa na kukiri kuvutiwa na uwezo wa mkongwe huyo.
“Navaa jezi namba tano kwasababu namkubali Kelvin Yondani na amekuwa niongoni mwa wakongwe ambao wamekuwa wakiniongoza na kunifanya nipambane na kuwa bora;
“Nimecheza naye nilipopita Geita Gold kabla sijatimkia Polisi Tanzania ni moja ya wachezaji ambao wanafundisha uwanjani anatamani na sisi tufike mbali kama yeye alivyofika hapo alipo sasa amekuwa akinielekeza mambo mengi pia aliniambia kuwa alikuwa anafurahi tulipokuwa tunatengeneza ukuta pamoja huku akiniambia kuwa ni mchezaji ambaye ni muelewa na msikivu ndio maana alikuwa ananipenda na kuona nafika mbali.” anasema Mbegu.
UBORA WA IHEFU
Ihefu FC ni miongoni mwa timu ambazo zilikuwa nafasi mbaya na kutajwa kushuka daraja msimu huu lakini sasa ipo nafasi ya saba baada ya kucheza mechi 26 ikishinda mechi 10, imefungwa tatu, imetoka sare 13 imefunga mabao 25 imefungwa 28 na imekusanya pointi 33.
“Tulikuwa na hali ngumu sana lakini uongozi ulishtuka na kufanya mambo muhimu kwa kusajili wachezaji ambao wameongeza nguvu na kuipambania timu kufika hapo ilipo sasa japo pia Mungu alikuwa upande wetu hadi hapa tulipofikia;
“Hatuna presha tupo imara hatuwazi kushuka daraja tunapambana kusonga hatua za juu zaidi kitu ambacho kinawezekana pamoja na kutoka kupoteza mechi mfululizo lakibni Ihefu FC imeingia kwenye ushindani na kuwa miongoni mwa timu zinazotoa changamoto kwa wapinzani haikuwa rahisi.” anasema Mbegu.
TUKIO POLISI
Kila mwanadamu anatukio lake zuri na baya kwenye maisha yake ambalo hawezi kulisahau kutokana na namna alivyokuitana nalo anaweza kufanya mengi lakini asiache kusahau lile ambaloa anaamini ni bora au baya kwake.
Beki wa Ihefu Mbegu anagema kwenye maisha yake ya soka alishawahi kufanya tukio la kizembe ambalo analijutia hadi sasa na kukiri kuwa hata kaa akalisahau.
“Nikiwa Polisi Tanzania nakumbuka tulikuwa tunacheza na Mbeya City niliwasawazishia bao wapinzani wetu kwa kujifyunga na mchezo uliisha kwa sare ya mabao 2-2 nilijisikia maumivu makali sana ni moja ya tukio la kizembe ambalo sitakaa nikalisahau kwasababu niliighalimu timu kuambulia pointi moja nyumbani,” anasema Mbegu ambaye amepata kadi za njano mbili ndani ya misimu minne aliyocheza soka Ligi Kuu Bara.