Mwandishi wa Habari na Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Shaffih Dauda amefuta kauli yake ya Underdog kwa Klabu ya Simba SC, baada ya klabu hiyo kupambana vilivyo dhidi ya Wydad AC katika mchezo wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC imetolewa kwenye Michuano hiyo jana ljumaa (Aprili 28) kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati, baada ya matokeo ya jumla ya 1-1, kufuatia kila timu kushinda 1-0 katika Uwanja wake wa nyumbani.
Shaffih alitoa kauli ya Underdog wakati Simba SC ilipotinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2018/19, na kuishia hatua ya Robo Fainali kwa kufungwa na TP Mazembe 4-1 katika hatua ya Robo Fainali.
Lakini usiku wa kuamkia leo Jumamosi (Aprili 29) Mwandishi na Mchambuzi huyo alitumia ukurasa wake wa Instagram kufuta kauli hiyo kwa kuandika:
“Simba siyo Underdog tena kwenye mashindano ya Afrika ngazi ya klabu. Wameimarika sana kwenye maeneo mengi hususani kwenye Uongozi.
“Kuna vitu vichache tu vya kuweka sawa, naamini next season lengo la kufika nusu fainali litawezekana. Kama taifa bado tuna nafasi ya kuifikisha timu yetu kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya Afrika ngazi ya klabu.
“Sasa sote tuungane kwenda kuishangilia Yanga ili iendelee kuipeperusha bendera yetu ya Taifa,” amesema Shaffih.