Home Habari za michezo EDO :- KWA SIMBA HII INAYOJITAFUTA…WAKIITOA WYDAD ITAKUWA NI NDOTO YA KUTISHA…

EDO :- KWA SIMBA HII INAYOJITAFUTA…WAKIITOA WYDAD ITAKUWA NI NDOTO YA KUTISHA…

Habari za Simba SC

Tuanze na mechi ya Simba. Sioni nafuu. Ni ndoto inayotisha. Ninachoamini ni kwamba ikitokea Simba wakaitoa Wydad basi wataenda kuchukua taji lenyewe. Ni ngumu Simba kuwatoa Wydad kwa sababu tatu kuu.

Simba watahitaji maajabu. Ukitazama namna ambavyo walitawaliwa na Raja katika mechi zote mbili kisha ukaenda kutazama msimamo wa Ligi Kuu ya Morocco utajua mazingira ya hatari ambayo Simba wapo.

Katika uhalisia wa kawaida Wydad ni timu kali kuliko Raja. Na katika uhalisia wa nje tu Wydad imeizidi Raja pointi 12 katika Ligi yao. Raja inashika nafasi ya tano wakati Wydad inashika nafasi ya pili.

Inakuonyesha tu kwamba hata katika Ligi yao ya Morocco kwa sasa Wydad ni wakali kuliko Raja achilia mbali kwamba wao ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini kuna ukweli kwamba Wydad wanacheza na Simba hii ambayo imeendelea kujitafuta. Simba ambayo haijafikia bado makali ya ile ya kina Louis Miquissone, Clatous Chama, Hassan Dilunga, Rally Bwalya. Simba hii ambayo viwango vya kina Josh Onyango vimeanza kuwatia shaka mashabiki. Wataiweza kasi ya Wydad kama walishindwa kuendana na kasi ya Raja?

Sababu ya tatu ni ukweli kwamba mechi ya kwanza itachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa pale Temeke. Simba sio tu watahitaji kushinda, lakini watahitaji kushinda mabao mengi. Hili la kushinda mabao mengi dhidi ya Wydad ni jambo ambalo litawastaajabisha watu wengi. Kuifunga Wydad ni jambo moja, kuifunga mabao mengi ni jambo jingine ambalo litastaajabisha. Simba wataweza kweli?

Ni wazi kwamba kule Casablanca Simba wanaweza kupewa ubatizo wa moto. Kama wanatamani kujaribu kupita basi kila kitu kimalizike kwa Mkapa. Kinachoweza kuwapitisha ni kufungwa idadi ndogo ya mabao kuliko ambayo wao watakuwa wamefunga Dar es Salaam. Hili litawezekana? Naona ni jambo gumu. Casablanca Simba watakutana na mashabiki wenye mzuka wa Wydad.

SOMA NA HII  MABOSI SIMBA WAANZA KUYAPANGIA BAJETI MABILIONI YA CAF SUPER LEAGUE...BAJANA ATAJWA...