Home Habari za michezo KOCHA SIMBA AKWAMISHA DILI LA MKUDE…”YUPO NA ATAKUWEPO HAONDOKI….AMEZUNGUMZA HAYA

KOCHA SIMBA AKWAMISHA DILI LA MKUDE…”YUPO NA ATAKUWEPO HAONDOKI….AMEZUNGUMZA HAYA

KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amekata mzizi wa fitina kwa kuweka bayana hana shida na kiungo, Jonas Mkude tofauti na uzushi uliopo mtandaoni kwamba wawili hao picha haziivi.

Siku za hivi karibuni mashabiki na wadau wa soka nchini wamekuwa wakihoji uwepo wa Mkude ndani ya Simba kutokana na kutoonekana mara kwa mara na timu inaposafiri kucheza mechi jambo ambalo wengi walilitafsiri kama kutoelewana na Robertinho lakini kocha huyo ameweka wazi kuwa hana shida na Mkude na wanaendelea kufanya kazi pamoja kama timu.

“Wapo wachezaji wengi ambao hawajacheza mechi hivi karibuni na sio Mkude tu, natambua ni mchezaji mzuri na pendwa na amekuwa katika kiwango bora ndani ya Simba kwa muda mrefu.

Sina tatizo naye hata kidogo lakini kinachotokea ni aina ya mechi tulizokuwa nazo hivi karibuni na namna tulitaka kuzicheza ndio maana hamjamuona katika orodha,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Kama nilivyosema mwanzo, Mkude yupo hapa na umemuona na amekuwa akifanya mazoezi na timu, kinachotokea ni muda kuwa mfinyu wa kuandaa timu na tayari katika eneo lake kuna watu wamecheza kwa ubora na kwa bahatu mbaya zaidi hauwezi kuwatumia wote kwenye mchezo mmoja.”

Tofauti na Mkude, Robertinho amesisitiza kuwa anafanya kazi yake kwa kufuata taaluma, na misingi yake na yeye amechagua kuwatumia wachezaji wanaojituma na kufanya vizuri mazoezini.

“Kila mchezaji ndani ya Simba anauwezo na uhitaji wa kucheza mechi, lakini mimi naamini katika kile wanachokionyesha mazoezini, sina mchezaji ambaye naweza kumuhakikishia nafasi lakini atakayefanya vizuri mazoezi basi atapata muda wa kucheza.”

SOKA LA BONGO lilikuwepo katika mazoezi ya Simba ya juzi asubuhi yaliyofanyika uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju Dar es Salaam na kumshuhudia Mkude akifanya mazoezi na wenzake kama kawaida.

Simba kesho Ijumaa kuanzia saa 1:00 usiku itajitupa uwanja wa Uhuru, kucheza mechi ya robo fainali ya Kombe la TFF (ASFC), dhidhi ya Mtibwa Sugar na mshindi wa mechi hiyo atakutana na Azam FC katika nusu fainali.

SOMA NA HII  KOCHA SIMBA ALINOLEWA NA PELE...WALICHEZA TIMU MOJA...ALIMPASIA PASI YA GOLI