Home Habari za michezo MAYELE ATOBOA SIRI ZA MAZEMBE…KOCHA YANGA ALIMTUMA MISHENI YA SIRI

MAYELE ATOBOA SIRI ZA MAZEMBE…KOCHA YANGA ALIMTUMA MISHENI YA SIRI

MAYELE ATOBOA SIRI ZA MAZEMBE...KOCHA YANGA ALIMTUMA MISHENI YA SIRI

KIKOSI cha Yanga tayari kipo Lubumbashi, DR Congo kucheza mechi ya mwisho ya Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe, lakini kubwa zaidi ni namna straika hatari wa timu hiyo, Fiston Mayele alivyocheza na mafaili ya wenyeji kwa lengo la kuwabeba Wanajangwani.

Ipo hivi. Wakati baadhi ya mastaa, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki wa Yanga wakitokea Tanzania kwenda Lubumbashi kuikabili Mazembe, Mayele alikuwa kwenye ndege nyingine akitokea Mauritania alikokuwa na timu ya taifa ya DR Congo iliyotoka sare ya 1-1 ugenini kwenye mechi za kufuzu Afcon akiingia kutoka benchi dakika ya 58 kwa kuchukua nafasi ya Aldo Kalulu.

Yanga imepania kushinda mechi hiyo ili iongoze kundi hilo na katika kuhakikisha Mayele anaendelea kuitesa Mazembe kama alivyofanya katika mechi ya kwanza iliyoisha kwa Yanga kushinda 3-1 jijini Dar licha ya kutofunga na straika huyo alipewa kazi maalumu na kocha Nasreddine Nabi ili aisome mapema kabla ya kuungana na timu nchini humo.

Wakati kocha Nabi akiendelea kuwanoa wachezaji wengine kambini Avic, Kigamboni, aliamua kumtumia Mayele video clip za mabeki na viungo wa Mazembe ili awasome kwa umakini akiwa angani ili kujua namna ya kuwavuruga kabla ya kukutana nao Jumapili jijini Lubumbashi.

Inaelezwa Yanga haina mpango wa kubadili sana wachezaji wa kikosi cha kwanza, tofauti na kipa Djigui Diarra na kiungo Khalid Aucho wenye kadi za njano, hivyo Mayele mwenye mabao matatu hadi sasa kwenye michuano hiyo ataendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ambayo amepania kufunga katika mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Akizungumza na SOKA LA BONGO, Mayele ameweka wazi kiu yake ya kuifunga Mazembe nyumbani kwao baada ya kuwakosa Kwa Mkapa katika mechi iliyomalizika kwa Yanga kushinda 3-1 kwa mabao ya Keneddy Musonda, Mudathir Yahya na Tuisila Kisinda, huku akifafanua alivyojiandaa kutimiza hilo.

“Nimekutana na Mazembe mara kadhaa nikiwa AS Vita na sasa Yanga, huwa ni wapinzani wagumu lakini natamani kuwafunga na kuisaidia timu yangu kushinda mechi hii,” alisema Mayele na kuongeza;

“Pamoja na kwamba wachezaji wengi wa Mazembe tunafahamiana lakini nimejitahidi kuwafuatilia kwa karibu kujua wanachezaje. Kuna baadhi ya video zao nimepewa na viongozi wangu, naziangalia mara kwa mara kuhakikisha nawasoma vyema na najua aina yao ya kucheza ili kama nikipata nafasi nisisumbuke kufunga, ila naamini Yanga ni timu kubwa na tutashinda mechi hii yenye ushindani mkubwa,” alisema.

Yanga imeshafuzu robo fainali ikiwa na pointi 10 sawa na Monastir ya Tunisia itakayomalizana na Real Bamako, japo zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa na mechi ya Mazembe ni kusaka heshima kwani ikishinda itaganda kileleni na kukwepa kukutana na vigogo hatua inayofuata.

Droo ya robo fainali inatarajiwa kuchezeshwa Jumatano ijayo jijini Cairo Misri baada ya mechi zote za makundi kumalizika ambapo Yanga itajua inakutana na timu gani katika hatua hiyo ya mtoano na mechi za kwanza zinatarajiwa kupigwa kati ya April 21-22 huku marudiano yakitazamiwa kuwa kati ya Aprili 28-29 mwaka huu na timu zitakazindiana kwa matokeo ya jumla zitatinga nusu fainali.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA KESHO.....MAMELOD WASHTUKIA JANJA JANJA YA YANGA....KOCHA WAO KAIBUKA NA HILI...