KOCHA wa Yanga SC, Nasreddine Nabi ameliambia Gazeti la Mwanaspoti kwamba kwa mkakati alioupanga na vijana wake, kuna rekodi inakuja nusufainali dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.Mechi ya kwanza itachezwa Mei 10, Kwa Mkapa.
Nabi ameweka wazi kwamba tayari wameanza kuicheza mechi hiyo kwa kukusanya taarifa za Marumo na ameona mechi moja pekee ya Wasauzi hao na kazi inaendelea.
Nabi alisema ana kiamini kikosi chake lakini anatambua kwamba Marumo ni timu isiyotabirika wakicheza soka la kasi huku akisikitika kumkosa winga wao Bernard Morrison ambaye haruhusiwi kuingia nchini Afrika Kusini.
“Niliwaona mechi yao moja ya hatua ya makundi sio timu rahisi tunatakiwa kujipanga sawasawa, tayari tumeshaanza kutafuta taarifa zao zaidi lakini niseme tunatakiwa kuiheshimu kwa kufika kwao nusu fainali, zitakuwa ni mechi mbili ngumu za nusu fainali,”alisema Nabi.
“Najivunia kikosi changu, naamini wanatambua kwamba kama watajiongeza kidogo kuna rekodi kubwa tunaweza kuiweka msimu huu lakini haitakuja kirahisi tunatakiwa kuvuija jasho zaidi ya kote tulikotoka, nasikitika tutamkosa Morrison (Bernard) kwenye mchezo wa ugenini, nitazungumza naye awaadhibu mchezo wa hapa.”
KAMATI MBILI ZA HERSI
Rais wa Yanga SC, injinia Hersi Said ameliambia Mwanaspoti kuwa kutinga nusu fainali ni mafanikio ya klabu yao na taifa kwa ujumla na sasa wanaanza mkakati wa kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi kwenye mechi mbili za nusu fainali.
Hersi alisema tayari wameshaunda kamati mbili nzito ndani ya klabu yao ambazo moja itasimamia mechi za ndani lakini pia kutakuwa na kamati nyingine itayayosimamia hesabu zote za mechi ya shirikisho.
“Hizi kamati zote mbili zinafanya kazi kwa ushirikiano kwa kuwa wanasimamia afya ya timu moja, wanafanya vikao na kuleta njia na wepesi wa kikosi chetu ili kiweze kufanya vizuri, ushirikiano ni mkubwa sana ndani ya eneo la utawala.
“Niwaombe mashabiki wetu wa Yanga SC kila mmoja aingie vitani kama tunavyofanya viongozi wao, mchezo wetu ujao utachezwa katikati ya wiki, niwaombe mashabiki wetu kila mchezo kwetu ni fainali tunatakiwa kushikamana kwani hakuna wa kututengenezea ushindi nje ya klabu yetu,” alisema.
“Niwapongeze wanachama na mashabiki, kipekee niwapongeze wachezaji, makocha na viongozi wenzangu kwa mafanikio haya ambayo tumefikia lakini bado tuna safari ya kufika na kutamani makubwa zaidi,”alisema Hersi.
Hersi alifafanua kuwa hatua ya kwanza Yanga inajua ratiba ngumu watakayotakiwa kukabiliana nao ndani ya mwezi Mei ambapo watakuwa na jumla ya mechi 7 nzito zitakazoamua mafanikio yao msimu huu.
“Timu inaelekea Singida ikipitia Dodoma kwa ratiba ya sasa ina maana kule tutakuwa na mechi mbili tutacheza na wenyeji wetu mechi ya ligi na baada ya hapo Mei 7, tutacheza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Azam.
“Tukimaliza mechi hizo mbili tutatumia siku nzima kurudi jijini Dar es Salaam, kama mnavyofahamu hakuna uwezekano wa kupata ndege ya moja kwa moja kutoka Dar kwenda Singida utalazimika kusafiri kwa basi mpaka Dodoma halafu hapo utafute ndege utaona kuna siku nzima ya tarehe nane utaitumia kusafiri, sijui utafanya mazoezi gani tarehe tisa ili kesho yake ucheze na Marumo.
“Mwezi huu huu tutakuwa na mechi tatu za ligi ambazo ni muhimu zitakazoamua ubingwa wetu wa ligi lakini pia tutakuwa na mechi mbili za nusu fainali ya Kombe la shirikisho lakini nazo kama tutafanikiwa kushinda ina maana fainali ya kwanza ya shirikisho nayo tutacheza ndani ya mwezi huu.”
Aidha Hersi alisema wameshaanza mazungumzo na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kuangalia upya ratiba ya mechi za ndani kwa kuwa ndio ratiba pekee inayoweza kutazamwa ili kuipa timu yao afya ya kufika mbali.
“Hii ni picha ngumu ambayo tunaweza kuiona kwa awali wakati huu tukianza hesabu za kucheza nusu fainali, klabu tumeanza mazungumzo na wenzetu wa bodi ya ligi kuangalia ni namna gani watatuangalia kutupunguzia ugumu wa ratiba kwenye mechi hizi za ndani, kama mnavyofahamu bodi yetu haina mamlaka ya kuingilia ratiba ya CAF.”