Home Habari za michezo SAFISHA SAFISHA SIMBA YANUKIA….BENCHI LA UFUNDI KUSUKWA UPYA…MGUNDA HATIHATI…

SAFISHA SAFISHA SIMBA YANUKIA….BENCHI LA UFUNDI KUSUKWA UPYA…MGUNDA HATIHATI…

Habari za Simba SC

SIMBA imeanza mipango ya msimu ujao ikitaka kuboresha kila eneo ili kuhakikisha inarejea kwenye makali yake na kwa kuanzia itafanya maboresho kwenye benchi lake la ufundi kwa kuondoa baadhi ya watu na kushusha wataalamu wapya.

Inafahamika uongozi wa Simba kwa nyakati tofauti umekaa vikao na kila mtaalamu aliye katika benchi la ufundi la timu hiyo na kutathimini hatima yake ndani ya kikosi kwa kuzingatia maelewano dhidi ya wenzake, sehemu alipofaulu na alipofeli na kupata mwanga wa wapi pa kuanzia.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda, na kocha wa viungo, Kelvin Mandla kutokea Afrika Kusini ni miongoni mwa majina ambayo yapo mezani kujadiliwa kwa kina na huenda wakaondoka Msimbazi mwishoni mwa msimu huu kutokana na sababu mbalimbali.

Licha ya kwamba Mgunda amekuwa kipenzi cha mashabiki, viongozi na wadau wengi wa soka nchini tangu amejiunga Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coastal Union lakini huenda msimu ujao asiwe kwenye benchi la ufundi la Wekundu hao kutokana na kile kilichoelezwa ni maelewano hafifu na bosi wake, Mbrazil Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Taarifa zinasema kuwa hakuna mawasiliano mazuri kati ya Robertinho na Mgunda na Mbrazil huyo amekuwa akifanya maamuzi na mipango yake kwa karibu zaidi na Mtunisia Ounane Sellami ambaye alitua kikosini hapo kama kocha msaidizi wa pili baada ya Mgunda ikiwa ni pendekezo la Robertinho.

Hivyo Simba inataka kumuondoa Mgunda ili kumuachia mikoba kamili Robertinho na Ouanane lakini wamewapa nafasi ya kuongeza wataalamu kwenye bechi hilo ambao watafanya nao kazi kwa maelewano bora zaidi msimu ujao.

Kwa upande wa Mandla, inaelezwa kwamba ameshindwa kuendana na kasi wanayoitaka Simba katika eneo lake hivyo naye ataondoka msimu huu na ataletwa kocha mpya wa viungo bora zaidi na huenda akarudishwa Adel Zrane aliyewahi kufanya kazi hiyo kwa mafanikio kikosini hapo.

Lakini wakati hayo yakiendelea,  baadhi ya mastaa wa timu hiyo wameomba mapumziko ili wakapumzike na kujiandaa na msimu ujao huku wengine wakiomba kuondoka kikosini hapo na uongozi unasubiri tathimini ya kocha mkuu ili kulimaliza hilo.

Mastaa Clatous Chama (Zambia), Sadio Kanoute (Mali) na Henock Inonga (DR Congo) ni miongoni mwa wachezaji waliotajwa kuomba mapumziko wakati huu ambao timu hiyo imebakiza mechi tatu za ligi huku, Moses Phiri na Joash Onyango wakitajwa kati ya walioomba kuondoka Msimbazi.

SOMA NA HII  DK KADHAA KABLA YA YANGA KUKIPIGA NA WATUNISIA...MTOTO WA NABI AJITOKEZA NA HILI....BABA YAKE AKIFELI NDIO BASI TENA...