Yanga itarudiana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng, huku Wanajangwani wakiwa mbele kwa mabao 2-0 waliyopata Kwa Mkapa.
Wakati ikijiandaa kwa mchezo huo kuna ujanja na mambo ambayo yakitiliwa mkazo Yanga itaandika historia ya kuvuka mtihani huo mgumu na kutinga fainali ya kwanza ya Afrika.
UKUTA WA CHUMA
Katika mechi tisa, Yanga imeruhusu mabao kwenye michezo mitatu tu za kwanza, ikifungwa manne, lakini jambo la kufurahisha ni kwamba yote manne iliyofungwa msimu huu hakuna bao la ‘open play’ (shambulizi), yaani mabao yote manne ni ya mipira iliyokufa.
Ilifungwa 2-0 na US Monastir ya Tunisia mechi ya awali ya makundi iliyopigwa ugenini, moja likiwa la frii-kiki na jingine la kona, kisha ikashinda 3-1 dhidi ya TP Mazembe jijini Dar es Salaam, bao la wageni likifungwa kwa frii-kiki, halafu ikaenda ugenini dhidi ya Real Bamako ya Mali na kulazimishwa sare ya 1-1 baada ya wenyeji kukomboa bao kwa mpira wa kona ya dakika ya mwishoni.
Tangu hapo Yanga haijaruhusu bao tena. Na hii ni baada ya kocha Nasreddine Nabi kuanza kumtumia Ibrahim Bacca kama beki wa kati akichukua nafasi ya Dickson Job.
Hii inathibitisha Yanga imetengeneza uimara katika kujilinda ndio maana katika robo fainali, iliitoa Rivers United kwa mabao 2-0, huku ikiwabana mabingwa hao wa Nigeria na kuwafanywa washindwe kupiga japo shuti moja lililolenga lango katika dakika zote 180 za mechi hizo ikianzia Nigeria kisha kumalizia kwa sare 0-0 Kwa Mkapa.
Baada ya ushindi huo wa 2-0 Kwa Mkapa, Yanga inapaswa kuendeleza ubora iliyouonyesha msimu mzima katika kujilinda ili kuhakikisha inatinga fainali kwa mara ya kwanza.
UMUHIMU WA AZIZ KI KUWA SAITI
Kiungo wa zamani wa Asec Mimosas, Stephane Aziz Ki alitua Yanga kipindi ambacho haikuchukua muda mrefu kabla ya Wanajangwani hawajapata pigo la kukimbiwa na kipenzi chao, Feisal Salum, aliyegoma kuitumikia akitaka kuondoka.
Lakini habari njema kwa Yanga ilikuwa ni kutua kwa staa huyo raia wa Burkina Faso, ambaye usajili wake uliwafanya wachambuzi wajiapize kwamba asingeweza kuja Tanzania kwa vile kiwango chake ni cha kwenda Ulaya.
Mashabiki wanampenda sana Fei, lakini vitu vya Aziz Ki vinawafanya taratibu wamsahau Zanzibar Finest.
Aziz alisajiliwa kwa pesa nyingi na amethibitisha ni ‘big match player’ (mchezaji wa mechi kubwa).
Alianza kuonyesha cheche tangu mechi kubwa ya kwanza dhidi ya Simba katika Ngao ya Hisani msimu huu. Yanga ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 la Pape Oumane Sakho. Aziz alitoa asisti matata sana kwa Fiston Mayele, aliyefunga bao la kusawazisha kabla ya Mayele tena kutupia la pili na Yanga kuanza msimu kibabe na tuzo ya kwanza ya msimu.
Katika mechi ya ligi duru la kwanza, Yanga ilitanguliwa kwa bao moja la Augustine Okrah, lakini Aziz Ki akawarudisha Wanajangwani mchezoni kwa kufunga bao moja kali sana kwa mpira wa frii-kiki iliyoenda moja kwa moja wavuni ikimshinda kipa Aishi Manula.
Kwa kuwa bingwa wa msimu uliopita, Yanga ilianzia raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa, ikaifunga Zalan ya Sudan Kusini (5-0 kisha 4-0) katika mechi zote zilizochezwa Dar es Salaam, Mayele akifunga hat-trick mbili, Aziz Ki akafunga moja sawa na Farid Musa na Fei Toto.
Yanga ikafuzu raundi ya kwanza na kutolewa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya sare ya 1-1 Kwa Mkapa kisha kulala 1-0 ugenini na kuangukia hatua ya mchujo wa kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho ikapangiwa Club Africain ya Tunisia. Ikatoka sare ya 0-0 kwa Mkapa.
Presha ikawa kubwa kwa kocha Nasreddine Nabi, iliaminika angefutwa kazi endapo angeshindwa kuivusha timu makundi ya Shirikisho na zaidi kila mmoja alitarajia Yanga ingefungwa kwa sababu hapakuwa na timu ya Tanzania iliyowahi kushinda ugenini kule Tunisia.
Wakati huo, kocha Nabi alikuwa na wakati mgumu wa kuwatumia Fei na Aziz Ki kwa sababu wote wanacheza nafasi moja. Aziz Ki alisajiliwa kwa pesa ndefu na Fei ni kipenzi cha Wanayanga, na wakicheza pamoja timu ilionekana haitembei, inakosa mizania.
Katika presha hiyo kubwa, kwenye uwanja wa ugenini kule Tunisia, Nabi alimuanzisha Fei, alipochemka akamwita nje. Akampa nafasi ‘big match player’ Aziz Ki na kiungo huyo mwenye msuli mnene hakumuangusha Nabi. Akafunga bao kali la shuti la nje ya boksi, lililomfanya Nabi kuondoka kibabe katika ardhi ya nyumbani kwake.
Hapo katikati, Aziz Ki alikuwa na panda shuka ya kiwango, lakini aliendelea kuibeba timu kwa mabao muhimu akitupia 10 na asisti saba hadi sasa katika Ligi Kuu ikiwamo kufunga hat-trick katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Kagera Sugar Aprili 11, 2023.
Na bao lake la juzi katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Marumo limeweka Yanga katika mazingira mazuri kwa mechi ya marudiano kule Kwa Madiba na kuinua matumaini ya kucheza fainali yao ya kwanza ya Afrika.
CHIVAVIRO, WASHINGTON
Marumo inafungika. Kufikia sasa katika Kombe la Shirikisho kuanzia makundi hadi nusu fainali, Marumo imefunga mabao 14, ila imeruhusu mabao 13 katika mechi tisa.
Hii ni tofauti na Yanga ambayo katika mechi tisa imefunga mabao 13 na kuruhusu manne tu. Na katika mechi hizo tisa, sita Yanga haijaruhusu bao, wakati Marumo ni katika mechi mbili tu ndio haijaruhusu bao (clean sheet).
Kama ilivyojionyesha katika mechi iliyopita, Yanga inapaswa kujichunga na kinara wa mabao wa michuano hii, Ranga Chivaviro, mwenye matano, sawa na Mayele.
Chivaviro mara kadhaa alikaribia kuifunga Yanga juzi lakini alipoteza nafasi kwa kubanwa na kina Bacca au kupoteza umakini, huku pia Marumo ikimtegemea kipa wao na nahodha Washington Arubi, ambaye ana rekodi bora za kuokoa na pia kupiga pasi za kuanzisha mashambulizi kama alivyotisha Kwa Mkapa.
SABU ZA NABI
Tangu Yanga imekuwa chini Nabi, imekuwa ikifanya vyema na zaidi anapofanya mabadiliko ya wachezaji. Kocha huyo amekuwa na uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo na kubadili mambo kama alivyofanya juzi na katika mechi nyingi huko nyuma.
Hii ni karata nyingine inayoweza kuwabeba Yanga kule kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng Jumatano dhidi ya Marumo ya kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr, ambaye hajawahi kuifunga hata bao moja Yanga alipokuwa Simba msimu wa 2015/16 akifungwa 2-0, 2-0 mara zote walizokutana.