Uongozi wa Klabu ya Yanga umesema hauna shida na mchezaji yoyote yule ambaye anahitaji kuondoka ndani ya timu hiyo lakini bado ana mkataba na klabu hata awe amemaliza mkataba, wataagana kwa amani.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Sheria wa Klabu ya Yanga, Wakili Simon Patrick kufuatia tetesi kuwa wapo baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo ambao wameomba kuondoka hasa wale wa kigeni.
“Sisi kama viongozi tupo tayari kukaa meza moja na timu yoyote ile kutoka hapahapa Tanzania au nje ya Tanzania kufanya mazungumzo ya biashara kwa Joyce Lomalisa Mutambala kama wanamuhitaji au mchezaji mwingine kutoka kwenye timu yetu kwa sababu mpira ni biashara.
“Joyce Lomalisa Mutambala bado ana mkataba na sisi, tumeshampa msimamo wetu sisi kama viongozi (taasisi) nini anapaswa kufanya, mpira kwa sasa ni biashara na sisi kama Yanga hatuwezi kumzuia mchezaji ambaye anataka kutafuta changamoto sehemu nyingine.
“Mfano hai tu hata ulaya tunaona wachezaji wanatoka timu moja kwenda nyingine mfano sisi Chelsea leo hii Mendy, Coulibaly, Haverts, Mount, wote wanaondoka, ila timu ambazo zimewataka zimefata utaratibu ndio maana wameondoka.
“Na ndio sisi Yanga hatupo hapa kufanya jambo la kumkomoa mchezaji hapana, sisi kama Yanga tunataka kumwona mchezaji anafanikiwa zaidi hata kama ni nje ya Yanga na ndio maana tuliweza kuuza wachezaji ambao walikuwa vipenzi vya mashabiki kama Mrisho Ngasa kwenda Azam FC, Msuva kwenda Morocco, Tuisila kwenda RS Berkane, Mukoko Tonombe kwenda TP Mazembe na wengine.
“Kwa sababu mpira ni biashara na ndio manaa hata sisi Yanga tunafanya usajili kwa kuwachukua wachezaji ambao ni vipenzi vya mashabiki timu ambazo wanatoka wachezaji hao.
“Mfano Djigui Diarra alikuwa mchezaji kipenzi cha Stade Marine na hata tulivyoenda Mali kucheza na AS Real Bamako tulipata mapokezi mazuri kutoka kwa mashabiki wake Diarra.
“Milango ipo wazi kwa Joyce Lomalisa Mutambala kuja mezani na timu yake ambayo inamtaka tufanye nao mazungumzo. Ila kwa sasa Joyce Lomalisa Mutambala ni mchezaji halali wa Yanga,” amesema Simon.