Beki kisiki kutoka Kenya, Joash Onyango ameiweka Simba pabaya baada ya kukomalia kutaka kuondoka baada ya kuandika barua kwa uongozi, huku mabosi hao wakimchomolea kutokana na kutokuwa na hakika ya kumpata hadi sasa mbadala kikosini.
Onyango aliyesajiliwa na Simba, Agosti mwaka 2020 kwa mkataba wa miaka miwili kisha kuongeza mwingine msimu uliopita unaomalizika katikati ya msimu ujao, ameomba kuondoka kwa madai ya kutokuwa na furaha na maisha ndani ya klabu hiyo tangu msimu uliopita.
Hata hivyo, hadi sasa mabosi wa klabu hiyo wanaendelea kujadiliana, huku wengi wao wakimzuia asiondoke kwanza hadi wapata mbadala na kama itashindikana basi atamalizia mkataba alionao kabla ya kumruhusu kwenye dirisha dogo litakalofunguliwa katikati ya Desemba mwaka huu.
Habari kutoka ndani ya Simba na kuthibitishwa na mmoja wa mabosi wa klabu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina kwa kusema, mabosi wanahaha kupata mbadala wake atakayekuwa mhimili mzuri kwenye safu ya ulinzi ila bado hajapatikana hadi sasa.
Inaelezwa, endapo hawatakapa beki imara kama Onyango au kumzidi Mkenya huyo basi wataendelea naye hadi mkataba wake utakapomalizika, kwani hawapo tayari kuona mabeki wa kati wawili akiwamo Mohamed Ouattara wanaondoka kwenye kikosi hicho.
“Msimamo wa Onyango bado ni ule ule wa kutaka kuondoka, ila hawezi kuruhusiwa kuondoka kama hatutapata beki mwingine mzuri, hivyo atasubiri hadi dirisha dogo ila akipatikana basi ataachwa kama alivyoomba,” kilisema chanzo hicho na kuongeza.
Ugumu wa kumzuia Onyango unaelezwa ni kutokana na mabosi hao kushindwa kupata mbadala wake hadi sasa ambapo wameanza usajili wa chini chini wakisubiri dirisha la usajili lifunguliwe rasmi Julai Mosi hadi Agosti 30 mwaka huu, japo hadi sasa wamesajili nyota mmoja tu, Mcameroon Leandre Onana.
Mbali na Onana ambaye ni winga aliyekuwa Rayon Sports ya Rwanza, Simba inampigia hesabu kipa Mbrazil Caique Luiz Santos da Purificacao pamoja na Mrundi Fabien Mutombola na Alfred Mudekereza waliopo Vipers waliopendekeza na kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Hata hivyo inaelezwa makipa wawili wa Vipers huenda wakapigwa chini na kubakishwa Mbrazili ambaye ataungana na kipa Ally Salim wakati Aishi Manula anasubiriwa kurejea uwanjani kutoka majeruhi, huku fagio la kuwaacha karibu wachezaji 12 ambao hawahitajiki kwa sasa kikosini.
Fagio hilo limeanza na mastaa wanane akiwamo; Jonas Mkude, Mohamed Quattara, Victor Akpan, Augustino Okrah, Nelson Okwa, Gadiel Michael, Erasto Nyoni na Beno Kakolanya, huku Ismael awadogo, John Bocco, Habib Kyombo, Nassoro Kapama na Peter Banda nao ikielezwa wapo njiani kupewa ‘Thank You’.