Home Habari za michezo HAWA HAPA MASTAA YANGA WALIOVAA MEDALI ZA CAF BILA KUTOKWA JASHO…

HAWA HAPA MASTAA YANGA WALIOVAA MEDALI ZA CAF BILA KUTOKWA JASHO…

Habari za Yanga leo

Wakati kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameshindwa kuvishwa medali ya kwanza ya michuano ya CAF kutokana na kuisusa timu, juzi usiku baadhi ya mastaa wa Yanga walipata zali na kuandika historia ya kuvaa medali hizo baada ya timu hiyo kushika nafasi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ilishinda bao 1-0 ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria katika mechi ya pili ya fainali, lakini ikashindwa kubeba ndoo kwani awali kulala nyumbani 2-1 hivyo kuwasaidia wenyeji kutwaa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini licha ya matokeo ya jumla kuwa ni sare ya 2-2.

Hata hivyo, hiyo haikuzuia baadhi ya mastaa kupata zali la kuvishwa medali na Rais wa CAF Patrice Motsepe jijini Algers, licha ya kutotokwa jasho kivile kulinganisha na nyota wengine akiwamo Fiston Mayele, Djigui Diarra ama Dickson Job waliopigika mwanzo mwisho.

Fei Toto ni mmoja ya mastaa walioivusha Yanga kutinga makundi ya Shirikisho kabla ya kuibua sakata la kuvunja mkataba na kuilipa klabu hiyo kiasi cha Sh112 milioni ikiwamo mishahara ya miezi mitatu zilizorudishwa, kisha kiungo huyo kuisusa timu tangu Desemba mwaka jana.

Hata hivyo, wakati yeye akisusa, wenzake ambao baadhi hawakutoka jasho kabisa kikosini na hata wale waliongia kwenye dirisha dogo wamejikuta wakiangukiwa na zali la kuvaa medali hizo za CAF ikiwa ni historia kwao katika maisha ya soka.

Hapa chini ni wachezaji wanane walioangukiwa na zali hilo la kuvaa medali hizo za CAF mbali na timu hiyo kujihakikishia kuvuna Dola 1 Milioni (zaidi ya Sh2.3 Bilioni).

Feisal Salum, medali yake ya CAF inategemea busara za mabosi wa Yanga kama wataamua kumpa kutokana kiungo huyo kuwatibua kwa kuwashambulia baadhi yao, kwani ndani ya usajili wa msimu huu alicheza na kuivusha timu hadi makundi kabla ya kujiweka kando.

Winga Dickson Ambundo, msimu huu hakuonekana kabisa katika mechi nyingi za Yanga na hakuwa kabisa kwenye kikosi chao, alikuwa kwenye matumizi ya mikutano ya waandishi wa habari pekee lakini katika msafara wa kwenda kwenye fainali ya pili alijumuishwa na medali akavaa.

Beki wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, msimu huu wakati unaanza alitua kwa mkopo Dodoma Jiji, baadaye Geita Gold walipomtaka akachomoa dakika za mwisho uamuzi wake ukamsaidia kuvaa medali licha ya kwamba msimu huu hakucheza mechi yoyote ya timu hiyo akitumia muda mwingi kufanya mazoezi na kukaa jukwaani.

Chrispin Ngushi, naye hjakutumik sana Yanga kwani aliishia sana mazoezini kuliko kwenye mechi naye ana medali yake shingoni bila kucheza mechi yoyote ya CAF msimu huu kama ilivyo kwa kipa

Abuutwalib Mshery, aliyeanza vizuri kama kipa namba mbili kisha akaumia na kuwa nje hadi sasa.

Kipa mwingine, ambaye hajatumika kabisa tangu msimu uliopita ametwaa medali bila kutokwa jasho, huku Mudathir Yahya, beki Mamodou Doumbia, kipa Metacha Mnata na Mzambia Kennedy Musonda waliosajiliwa dirisha dogo nao wamevaa medali kama masihara, ingawa hawa wametokwa jasho kwenye baadhi ya mechi za michuano hiyo.

Mwingine aliyepata zali hilo ni Denis Nkane, winga ambaye alianza akiwa majeruhi naye ameva medali na jambo hilo limemfanya beki na nahodha wa zamani wa Yanga, Fred Mbuna kufunguka.

Mbuna aliyesifika enzi zake kwa mipira ya kurusha mbali na kukaba na kushambulia kwa kasi akipiga krosi matata, alisema hatua ya wachezaji hao kuna elimu kubwa ya kujifunza katika maisha yao ya soka kupitia mafanikio waliyoyapata kupitia Yanga, akiwataka kutumia hatua hiyo kujituma zaidi.

“Ni kweli kuna hilo kundi kwanza niseme hiyo ni bahati kwao na ni mafanikio ambayo wanastahili kwa kuwa walikuwepo ndani ya kikosi cha timu kwa msimu huu husika ambao Yanga imefikia hapo kwa hiyo wakipata medali wanastahili,” alisema Mbuna na kuongeza;

“Pia hatua hii itakuwa ni matumizi katika wasifu wao hata baadaye watakapostaafu, kila mchezaji hutamani kuitumikia timu iliyofikia mafanikio kama ya Yanga, lakini kubwa zaidi ni elimu na hatua hiyo iwaamshe wale waliokuwa wakikosa nafasi ya kucheza kwa kujua kila kitu kinawezekana.”

SOMA NA HII  REFA ALIYESHTAKIWA KWA KUIBEBA SIMBA KWA MKAPA AULA KOMBE LA DUNIA....CAF WAZIBA MASIKIO...

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here