Home Habari za michezo WAKATI WASAUZI ‘WAKIPUSH’ KUMBEBA….WAARABU WATUMA OFA YA BIL 2.8 KUMNG’OA MAYELE YANGA…

WAKATI WASAUZI ‘WAKIPUSH’ KUMBEBA….WAARABU WATUMA OFA YA BIL 2.8 KUMNG’OA MAYELE YANGA…

Tetesi za Usajili Yanga

MABINGWA mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC, wanaweza kupata wakati mgumu kukataa ofa ya Dola Milioni 1 (Sawa na Sh 2,806,936,000) kwa ajili ya kumuachia mshambuliaji wao, Mkongomani, Fiston Mayele kujiunga na Sepahan SC ya nchini Iran.

Mayele amekuwa katika kiwango bora kwa misimu miwili aliyoitumikia Yanga ambapo msimu wa 2022/23, ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara.

Mkongomani huyo mbali na kuwa Mchezaji Bora, pia alitangazwa kuwa Mfungaji Bora akifikisha mabao 17 sawa na kiungo mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Said Ntibazonkiza ‘Saido’. Pia ametwaa Tuzo ya Bao Bora na kuingia katika kikosi bora cha Ligi Kuu Bara.

Mtandao mmoja kutoka Afrika Kusini, umeripoti jumla ya klabu tatu zimeonesha nia ya kuhitaji saini ya mshambuliaji huyo ikiwemo Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Mtandao huo ulizitaja klabu nyingine zinazomuhitaji Mayele ni Sepahan SC, Al Hilal ya Sudan na Hatta ya UAE ambazo zote zimemfuata meneja wa mchezaji huyo kwa ajili ya kufanya mazungumzo.

Klabu hizo zinapata ugumu kutokana na mkataba wa mwaka mmoja alionao Yanga, ambao ameusaini katikati ya msimu uliomalizika.

Licha ya mkataba huo, lakini meneja wa Mayele pamoja na uongozi wa Yanga umesema upo tayari kusikiliza ofa kutoka kwa klabu hizo.

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alibainisha kwamba: “Bado hatujapokea taarifa yoyote kutoka Afrika Kusini, na hakuna klabu hata moja iliyowasiliana nasi.”

Wakala wa Mayele, hivi karibuni alizungumzia hilo akisema klabu pekee ya Afrika Kusini iliyoonesha nia ya kumtaka mshambuliaji huyo ni Mamelodi Sundowns.

“Kwa sasa, tuna ofa mbili thabiti mezani kutoka Saudi Arabia na Afrika Kusini. Hatujazizuia klabu nyingine kuanza mazungumzo na ofa inayotuvutia zaidi ni Rand 22.2 Mil (zaidi ya Sh 2.8Bil za Kitanzania) na nyingine ni Rand 13Mil (zaidi ya Sh 1.6Bil za Kitanzania) ambazo tumezipata kutoka katika klabu hizo zilizoonyesha nia,” alisema.

CHANZO: SPOTI XTRA

SOMA NA HII  KISA SARE NA GEITA...MANARA AENDELEA 'KUISILIBA' SIMBA MITANDAONI...AIBUKA NA HILI JIPYA LINGINE...