Home Habari za michezo MAYELE AWA GUMZO AFRIKA LIPO LA KUJIFUNZA

MAYELE AWA GUMZO AFRIKA LIPO LA KUJIFUNZA

Habari za Yanga

Hapana shaka yoyote kuwa Fiston Mayele ni miongoni mwa washambuliaji bora kwa sasa hapa nchini na kuna kundi kubwa la wachezaji wa nafasi yake wanaotamani kuwa kama yeye.

Uwezo wake wa kufumania nyavu, kasi, uamuzi wa haraka pindi awapo na mpira miguuni pamoja na hesabu sahihi za kujua awe wapi pindi mpira unapoelekezwa langoni mwa timu pinzani umemfanya awe tishio la safu nyingi za ulinzi hapa nchini.

Ni faida kwa nchi kuwa na mshambuliaji kama Mayele kwani uwapo wake unasaidia kuwapa ushawishi vijana wadogo na kiu ya kufika pale ambako yeye amefikia au juu ya hapo.

Kiwango chake bora ambacho amekuwa akikionyesha kimemuweka katika nafasi nzuri ya kuboresha maisha yake kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya ofa kutoka kwa timu mbalimbali ambazo zinahitaji huduma yake msimu ujao.

Yanga ambayo anaitumikia kwa sasa, tayari imemuwekea ofa nono ya kumshawishi aendelee kubakia ikijumuisha dau la kusaini mkataba mpya, mishahara pamoja na stahiki nyingine na kwa sasa inaendelea na mazungumzo naye kuona kama inaweza kufanikiwa katika hilo.

Ukiondoa Yanga, zipo pia timu kutoka Afrika Kusini, Kaskazini mwa Afrika pamoja na Mashariki ya Kati ambazo nazo inaripotiwa zimetenga mamilioni ya fedha ili kuhakikisha zinamng’oa Mayele ndani ya kikosi cha Yanga na kumfanya kuwa sehemu ya vikosi vyao msimu ujao.

Hata hivyo pamoja na uwepo wa ofa nyingi mezani na sifa nyingi ambazo amekuwa akizipata kwa mashabiki na wadau wa mpira wa miguu nchini na nje ya Tanzania, Mayele ameonekana kufuata msingi ya weledi katika kushughulikia hatima yake ya baadaye.

Imekuwa ikiripotiwa kuwa mshambuliaji huyo anatamani kutafuta changamoto mpya nje ya Yanga na kupata malisho ya kijani zaidi kwingine lakini ameonekana kuwapa heshima waajiri wake wa sasa kwa kuwasilisha ombi hilo kwa njia za kistaraabu badala ya kulazimisha.

Mayele anafahamu kuwa ana mkataba wa mwaka mmoja umebakia kati yake na Yanga na ni klabu hiyo ina mamlaka makubwa kwa sasa ya kuamua kama itamuuza au itambakisha kikosini kutumikia muda uliobaki wa mkataba hivyo hataki kuwalazimisha wafanye kile ambacho anakihitaji yeye.

Ni jambo lililo wazi kwamba akilazimisha Yanga imuuze, klabu hiyo inaweza kuamua kumkomoa kwa kumtaka amalizie muda wa mwaka mmoja uliobaki katika mkataba baina yao jambo ambalo litamuathiri yeye mwenyewe kwa vile timu hizo zinazomhitaji kiuhalisia haziwezi kukubali kucheza msimu mzima zikimsubiria yeye.

Lakini pia kama akilazimisha, Yanga inaweza kumuuza kwenda katika timu ambayo yeye sio chaguo lake tofauti na ikiwa ataondoka kistaarabu.

Ukiondoa hivyo, anafahamu fika kuwa mchezo wa soka huwa hautabiriki na huenda siku moja mambo yakamuendea ndivyo sivyo hivyo anaweza kurudi yanga au tanzania siku moja ikiwa huko aendako atashindwa kufanya vyema.

Hili ni darasa ambalo wachezaji wengi hasa wale wanaocheza katika Ligi Kuu ya NBC wanapaswa kujifunza kwanimara nyingi wamekuwa hawatumii njia sahihi za kudai masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na stahiki zao.

Baadhi yao hulazimisha kushinikiza uongozi wa timu zao kwa kugoma kufanya mazoezi au hata kucheza mechi na wengine kuamua kusaini mikataba katika timu nyingine huku wakiwa na mikataba ambayo haijamalizika mahali waliko.

Matokeo yake ni kuibuka kwa migogoro ambayo mwisho wa siku huathiri safari ya mchezaji kisoka na maisha yake kiujumla.
Iko mifano ya wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa vya soka ambao tuliwashuhudia katika ligi yetu lakini hadithi yao ilikuwa fupi kwa kujiingiza katika migogoro isiyo ya lazima ya kimkataba na klabu zao.

Kukosa uvumilivu na kutoheshimu mikataba waliyonayo, kuliwafanya watumie muda mwingi wakiwa hawachezi badala ya kuwepo ndani ya uwanja ambako kungewapandisha thamani zaidi na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuvuna fedha nyingi kupitia soka.

Kitendo cha Mayele kujitofautisha nao na kuonyesha ni njia gani sahihi ambayo mcezaji anapaswa kupita katika kupigania maslahi yake, kinasaidia kuwafungua wengine ambao bado hawajakutana na mazingira kama hayo.

Wachezaji wanapaswa kuelewa kwamba sio kila kitu watakifahamu pale watakapoenda darasani. Wanaweza kujifunza kwa kuona na kusikia kwa yale yanayofanywa na wenzao kama Fiston Mayele,
Badala ya kutumia njia zisizo za kiweledi, pengine kuanzia sasa wataanza kuongozwa zaidi na heika na busara.

SOMA NA HII  SIMBA, YANGA WAWEKA WAZI MALENGO YA USAJILI WAO DIRISHA KUBWA LA USAJILI