Home Habari za michezo HIYO YANGA U17 SIO POA SIMBA KIMYAA

HIYO YANGA U17 SIO POA SIMBA KIMYAA

Mabao mawili ya Mosses Samweli na Mohamed Salum dhidi ya JKU Academy juzi katika Uwanja wa Azam Complex, yamezidi kuifanya timu ya vijana ya Yanga chini ya umri wa miaka 17 izidi kuchanja mbuga kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo iliyobakiza raundi tatu kumaliza mzunguko wa kwanza.

Ushindi huo wa juzi umeifanya Yanga U17 kufikisha pointi 32 na kuendelea kuongoza ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 ikifuatiwa na Azam FC na Ihefu huku Simba ikishika nafasi ya nne.

Lakini pia mbali na kuendelea kuongoza msimamo wa ligi, timu hiyo inayonolewa na nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, inaendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo wowote kwenye mashindano hayo hadi sasa, ikiibuka na ushindi katika michezo 10 na kutoka sare mara mbili.

Akizungumzia makali ya timu yake kwenye mashindano hayo, Malima alisema kuwa yanatokana na nidhamu na juhudi za wachezaji wake kusikiliza na kufuata yale ambayo wamekuwa wakielekezwa.

“Yanga ni timu kubwa na mchezaji anapopata nafasi ya kuichezea Yanga anapaswa kuwa na juhudi na nidhamu pasipo kujali yupo katika kikosi cha wkaubwa, vijana au wanawake na hicho ndicho ambacho kinachangia vijana wangu wawe wanafanya vizuri.

“Ligi bado iko mzunguko wa kwanza lakini muelekeo wetu ni mzuri hivyo nina imani kama tutaendelea hivi, tuna nafasi ya kuchukua ubingwa ambalo ndilo lengo letu kuu,” alisema Malima.

Ukiondoa Yanga, Azam, Ihefu na Simba, timu nyingine za vijana chini ya umri wa miaka 17 zinazoshiriki mashindano hayo ni JKU Academy, Karume Youth Centre, Mbeya Kwanza, Singida Big Stars, Ruvu Shooting, African Sports, KMC, Transit Camp, African Lyon, Pan African na Green Warriors.

SOMA NA HII  NGOMA AWAPATA JEURI VIONGOZI WA SIMBA, SIRI YAFICHUKA...YANGA WAPIGWA ZA USO